
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
6.12.2014

WITO umetolewa kwa wananchi kuwa sasa iwe basi kwa
maneno na vitendo katika kuwafanyia ukatili na udhalilishaji wanawake na watoto
na watu wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo wapelekwe kwenye
vyombo vya sheria sambamba na kuwepo mashirikiano katika kutoa ushahidi bila ya
kumuonea mtu.
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito huo leo huko
katika ukumbi wa Salama, Bwawani mjini Zanzibar katika hotuba yake aliyoitoa
kwenye uzinduzi wa Kampeni ya miaka
miwili ya Kupiga Vita Ukatili na Udhalilishaji wa Wanawake na Watoto Zanzibar.
Katika hotuba
yake hiyo Dk. Shein alisema kuwa jambo ambalo linampa huzuni na kumsikitisha ni
kuendelea kusikia kila uchao kushamiri kwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji
dhidi ya wanawake na watoto katika jamii.
Alisema kuwa hili
ni suala ambalo linatokea katika jamii mbali mbali duniani, lakini kwa silka,
mila, utamaduni, dini na historia ya jamii ya Kizanzibari tatizo hilo
halikustahili kufikia katika kiwango kilichopo sasa nchini.
“Lazima sote
tulionee aibu jambo hili ambalo siyo tu linaipa taswira mbaya jamii yetu lakini
vile vile, lina athari kubwa kijamii na hasa wanawake na watoto wanaoishi kwa
hofu, kwa wasiwasi na kwa masikitiko makubwa pamoja na kukosa raha na
furaha”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein
alisema kuwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto
ni uvunjaji wa haki za binadamu na haki za kikatiba kwa hivyo ni lazima jamii
yote ichukue hatua madhubuti na kutekeleza dhamira ya kuendeleza utawala bora
ulioipa nchi hii heshima kubwa.
Dk. Shein alisema
kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa upande wake itaendelea kuchukua hatua
za kuzirekebisha sheria kila inapobidi kwa lengo la kuhakikisha kuwa vitendo
vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto vinadhibitiwa.
Alisema kuwa taarifa
kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali zinaeleza kuwa zimeripotiwa kesi 149
za wanafunzi waliopewa ujauzito kati ya mwaka 2010 hadi 2014 kutoka Wilaya kumi
za Zanzibar ambapo pia katika kipindi hicho kuna matukio 229 ya wanafunzi
waliokatishwa masomo yao na kuozeshwa waume wengine bila ya ridhaa zao.
Akitoa nasaha
zake Dk. Shein aliitaka jamii kurudi katika misingi ya maadili mema na malezi
bora ya watoto kwa mujibu wa utamaduni wa Kizanzibari na mafundisho ya dini na
kuwataka wazazi kufuatilia nyendo za watoto wao hasa katika matumizi ya
mitandao ambao watoto hujifunza mienendo isiyokubalika katika utamaduni na
maadili ya Kizanzibari.
Dk. Shein alitoa
wito kwa viongozi wa dini, wanasiasa, viongozi wa vyombo vya habari na viongozi
wa taasisi za kiraia na jumuiya zisizo za kiserikali, kuzidi kuelimisha
wananchi kwa njia mbali mbali juu ya athari na ubaya wa vitendo vya ukatili na
udhalilishaji wa wananwake na watoto kwa mujibu wa dini, sheria na tamaduni
ziliopo.
Sambamba na hayo,
Dk. Shein alisema kuwa kufanikiwa kwa Kampeni hiyo kunategemea sana juhudi za
pamoja na kuimarishwa kwa mikakati inayotumiwa katika kukabiliana na suala hilo
ikiwa ni pamoja na kuifanyia kazi Sheria ya Mtoto namba 6 ya mwaka 2011 ikiwa
muongozo mkuu wa kusimamia haki za watoto.
Dk. Shein alisema
kuwa Serikali itafanya kila jitihada, ili Mkakati wa Mageuzi ya Mfumo wa Sheria
kwa watoto unafanikiwa ikiwa ni hatua muhimu ya kuipa nguvu kampeni hiyo ya
kupambana na ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto.
Alieleza kuwa kwa
bahati mbaya sana baadhi ya kinababa huwaachia sana ulezi kina mama peke yao,
jambo ambalo baadhi ya wakati matokeo yake huwa si mazuri na matokeo yake
wanaume huanza kuwalaumu wanawake na wakati mwengine kuonesha kiburi.
Pia, Dk. Shein
alikemea tabia ya kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili ikiwemo kupigwa
kwani haitoa taswira nzuri hasa kwa wanaume na kusisitiza kuwa mke hapigwi na
badala yake huengwa engwa “Mke hapigwi kwa fimbo hupigwa kwa ncha ya
kanga”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein
alisema kuwa ongezeko la talaka nalo limekuwa likichangia sana kuleta matokeo
mabaya ya malezi kwa watoto na wakati mwengine kuwa chanzo cha vitendo vya
udhalilishaji dhidi yao na kuwataka wanandoa kustahamiliana, kupendana na
kumuomba Mungu alete baraka na kuzidumisha ndoa.
Mapema Dk. Shein
alipokea matembezi ya hiyari yaliozishirikisha Wizara za Serikali pamoja na
taasisi binafsi pamoja na wananchi kutoka sehemu mbali mbali ambazo zilipeba
ujumbe mbali mbali katika kupiga vita vitendo vya udhalilishaji na ukatili kwa
watoto na wanawake na baadae alikagua mabanda ya maonesho yaliofanyika katika
viwanja vya hoteli ya Bwawani na kupata maelezo kutoka kwa wahusika.
Akitoa maelezo yake Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii,
Vijana, Wanawake na Watoto Mhe. Zainab Omar Mohammed alisisitiza haja ya kuwepo
mashirikiano ya pamoja katika kupiga vita udhalilishaji na ukatili wa watoto na
wanawake.
Nae Mwakilishi wa
Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Umoja
wa Ulaya kwa nyakati tofauti katika maelezo yao walieleza kusikitishwa na hali
hiyo na kuahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kupambana na ukatili na
udhalilishaji wa wanawake na watoto.
Nayo risala ya
Wanawake na Watoto iliyosomwa na Bi Hidaya
Makame ilieleleza kuwa miongonim mwa sababu zinazopelekea ukatili na
udhalilishaji wa wanawake ni pamoja na mila na desturi potofu katika jamii za
kumuona mwanamke kuwa ni kiumbe dhalili, mwenye hali duni ya kiuchumi pamoja na
kuporomoka kwa maadili.
Alidha risala
hiyo ilieleza kuwa watoto wanakabiliwa na mazingira magumu zaidi kutokana na
kukosa uwezo wa kujitetea, pia, risala hiyo ilieleza changamoto zinazowakabili
wanawake na watoto wenye ulemavu na wanaoishi na virusi vya UKIMWI.
Risala hiyo
ilieleza kuwa baadhi yao wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji,
ikiwa pamoja na kubakwa, kukosa matunzo stahiki, kunyanyapaliwa, kufanyiwa
mambo mabaya kinyume na maadhili na kuishi katikamazingira magumu.
Katika uzinduzi
huo ambao ulizinduliwa kwa maelezo yaliotolewa na viongozi wa dini ya Kiislamu
na Kikiristo juu ya udhalilishaji wa watoto na wanawake ambapo viongozi hao
walieleza kuwa dini zote hizo zinakataza udhalilishaji huo na ukatili.
Viongozi mbali
mbali walihudhuria katika uzinduzi huo akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Mama Pili Balozi, Mawaziri, na viongozi wengine
wa serikali, dini na kisiasa, taasisi binafsi, Mashirika ya Kimataifa pamoja na
wanachi mbali mbali.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment