Na Khamis Amani
Mahakama ya Rufaa Tanzania kanda ya Zanzibar,
imeanza rasmi kikao chake cha wiki mbili kwa kusikiliza mashauri mbali mbali ya
jinai na madai yaliyowasililishwa mahakamani hapo.
Mahakama hiyo yenye jopo la Majaji watatu,
inatarajia kusikiliza rufaa na maombi 21 ambayo maamuzi na hukumu zake
zinatarajiwa kutolewa Disemba12 mwaka huu.
Kikao hicho kinachofanyika mahakama kuu Zanzibar
iliyopo Vuga mjini Unguja, ambapo kabla ya kuanza rasmi kazi zake kimefunguliwa
kwa gwaride kutoka kwa askari wa jeshi la Polisi wa kitengo cha kutuliza ghasia
(FFU) lililofanyika nje ya jengo la mahakama kuu.
Majaji wanaotarajia kusikiliza kesi hizo ni Jaji
Kimaro, Jaji Luanda pamoja na Jaji Mjasiri ambao kwa pamoja walianza kusikiliza
shauri la madai lililofunguliwa na Machano Khamis Ali pamoja na wenzake 17
dhidi ya Kamishna wa Polisi Zanzibar.
Kwa mujibu wa Francis Jacob Kabwe, Naibu Msajili
wa mahakama ya Rufaani Tanzania, jumla ya mashauri 21 yamewasilishwa mahakamani
hapo yakiwemo maombi manane ya madai, rufaa nane za madai, ombi moja la jinai
pamoja na rufaa nne za jinai.
Mashauri yote hayo yamewasilishwa mahakamani
hapo baada ya wahusika wake kutoridhika na maamuzi yaliyotolewa na mahakama kuu
ya Zanzibar na kuamua kupanda ngazi katika mahakama hiyo kwa mujibu wa sheria
ili kuona haki inatendeka.
Kikao cha mahakama ya rufaa kanda ya Zanzibar
kinafanyika mara moja kwa mwaka kwa kusikiliza na kutoa maamuzi ya kesi na
maombi mbali mbali ya jinai na madai baada kutoridhika na maamuzi yanayotolewa
na mahakama kuu ya Zanzibar.
No comments:
Post a Comment