Na Mwanajuma Abdi, Dar es
Salaam
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya
Salum, amesema pato la taifa la bei za
bidhaa na huduma limekua hadi kufikia shilingi trilioni 26.8 kwa mwaka 2007
ikilinganishwa na shilingi trilioni 20.9 mwaka 2001.
Hayo aliyasema jana wakati
akizindua usambaji wa takwimu za pato la taifa zilizorekebishwa kwa mwaka wa
2007 Tanzania Bara, uzinduzi ambao ulifanyika ukumbi wa Karimjee, Dar es
Salaam.
Alisema takwimu hizo zitatumika
katika bajeti kuu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania ya mwaka
2015-2016.
Alisema ukuaji huo ni sawa na
ongezeko la ukubwa wa pato la taifa kwa kiasi cha asilimia 27.8 ambapo ni
wastani wa pato la mwananchi kwa mwaka 2013 kwa kutumia takwimu zilizorekebishwa
ni shilingi 1,561,050, ambazo ni sawa na dola za Marekani 977 ikilinganishwa na
shilingi 1,186,200 kwa kutumia takwimu za pato la taifa za bei kwa mwaka 2001.
Alisema ukubwa wa pato hilo ni
juhudi za serikali za kutengeneza fursa kwa wananchi za kukuza uchumi wa
mwananchi mmoja mmoja, ambapo alisisitiza kwamba kuongezeka kwa pato la taifa
haina maana kuwa Serikali ina uwezo wa kuwajaza wananchi fedha mifukoni mwao
bila ya wao kufanya kazi.
Alisema kwa mujibu wa sensa ya
watu na makazi ya mwaka 2012 zaidi ya asilimia 63 ya wananchi wa Tanzania Bara
wanamiliki simu za kiganjani, hivyo ukuaji wa sayansi na teknologia umetoa
fursa kwa wananchi kujiongezea kipato kutokana kurahisisha mawasiliano.
Aidha alifahamisha kuwa,
kuongezeka thamani ya pato la Taifa kunaiongezea Serikali uwezo wa kimapato
kupitia kodi, hivyo inasaidia kugharamia ujenzi wa miundombinu na utoaji wa
huduma mbali mbali za wananchi ikiwemo ujenzi wa barabara, huduma za maji safi
na salama ambapo zaidi ya asilimia 60 ya kaya zote nchini zinapata huduma.
Alisema hayo ni baadhi ya
matokeo na fursa ya ukuaji wa uchumi ambao umepelekea umasikini wa kipato
kupungua kutoka asilimia 35 mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 28.2 mwaka 2012.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi
ya Taifa ya Takwimu, Dk. Albina Chuwa, alisema kazi za marekebisho ya takwimu
za pato la Taifa kwa Tanzania Bara imetumia tafiti za taifa zilizofanyika kwa
kipindi cha mwaka 2001 hadi mwaka 2007.
Alisema takwimu hizo ni pamoja na utafiti wa mapato ya matumizi ya
kaya, sensa ya kilimo iliyofanyika mwaka 2008 na takwimu nyengine za utawala
kutoka wizara na idara za serikali.
Akitoa shukurani, Naibu Gavana
wa Benki Kuu ya Tanzania, Juma Reli, alipongeza uzinduzi akisema huo ni muhimu
katika kukuza maendeleo ya uchumi wa taifa sambamba na kuishukuru Benki ya
Dunia na IMF kwa kusaidia mafunzo ya marekebisho hayo.
Uzinduzi kama huo utafanyika
Januari mwakani Zanzibar.
wewe zitangazie tu, mpaka wajanja waje kuzichota
ReplyDelete