Na Juma Khamis
Chuo Kikuu cha Taifa cha
Zanzibar (SUZA) kinatarajia kuanzisha skuli nyengine tano kikianzia na mwaka wa
masomo 2015/2016.
Akitoa muhtasari wa mipango ya
baadae ya chuo hicho kwa wajumbe wa Baraza la Ushauri la chuo hicho jana, Naibu
Makamu Mkuu wa chuo hicho (Fedha, Utawala), Dk. Zakia Aboubakary, alisema skuli
hizo ni pamoja na skuli ya Kompyuta,
Mawasiliano na Habari (SCCM) itakayoanza mwaka ujao wa
masomo.
Alisema skuli nyengine ni
Uhandisi wa mafuta, Biashara, Utalii na Kilimo.
Hata hivyo, uanzishwaji wa
skuli hizo mpya unakabiliwa na changamoto kubwa ikiwemo ufinyu wa miundombinu
hasa majengo na kwamba chuo kinahitaji dola za Marekani milioni 64 kumaliza
changamoto za miundombinu.
Wakati huo huo, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais,
Dk. Islam Seif, amekitaka Chuo hicho, kupeleka matokeo ya utafiti zinazofanywa
kwa wananchi.
Alisema hayo kampasi ya SUZA
Vuga katika maonesho ya utafiti, yanayokwenda sambamba na maadhimisho ya mahafali
ya 10 ya chuo hicho, yanayotarajiwa kufanyika Disemba 20.
Alisema utafiti ndio unaoweza
kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii na kuwataka wanafunzi na wasomi kujikita
katika kufanya tafiti zitakazojibu changamoto zinazowakabili wananchi.
Alikipongeza chuo hicho kwa
juhudi inazochukua katika kufundisha na kufanya tafiti na kwamba kimejibu kilio
cha muda mrefu cha Zanzibar kukosa chuo kikuu chake cha taifa.
Mapema Makamu Mkuu wa SUZA,
Prof. Idris Rai, alisema chuo kitaendelea kutoa mchango wake katika kusaidia
maendeleo ya taifa na jamii.
Maonesho hayo yalivutia idadi
kubwa ya wanafunzi na wananchi yaliyonesha tafiti mbali mbali zilizofanywa na
chuo hicho hasa katika masuala ya sayansi ya mazingira na bahari.
Kwa upande mwengine SUZA kimetiliana saini ya mkataba wa
maelewano (MoU) na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Viumbe (NMBU) cha Norway.
Hafla ya utiaji saini hiyo ilifanyika
kampasi ya SUZA Vuga ambapo Makamu Mkuu wa SUZA, Prof. Idris Rai, alisaini kwa
niaba ya chuo chake na Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Mazingira na Teknolojia wa
NMBU, Prof. Oystein Johnsen, alisaini kwa niaba ya chuo hicho.
Akizungumza katika hafla hiyo,
Prof. Rai alisema SUZA inaendelea kuimarisha ushirikiano na vyuo vikuu mbali
mbali duniani na vimefika vyuo vikuu 32.
Alisema kwa kuwa SUZA ni chuo
kichanga kitaendelea kujifunza kutoka kwa vyuo vyenye uzoefu kikiwemo chuo
hicho na kusema ni matarajio ya chuo kwamba ushirikiano huo utadumu kwa muda
mrefu.
No comments:
Post a Comment