Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammed Javad Zarif alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo akiwa na ujumbe aliofuatana nao
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammed Javad Zarif (wa pili kulia) alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo akiwa na ujumbe aliofuatana nao
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammed Javad Zarif (kulia kwa Rais ) alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo akiwa na ujumbe aliofuatana nao,[Picha na Ikulu.]
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
5.2.2015
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeeleza azma
yake ya kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria kati yake na
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo inaiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha
sekta mbali mbali za maendeleo.
Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo
wakati alipofanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu
ya Iran, Mheshimiwa Javad Zarif, Ikulu mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo
hayo, Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka kwa ndugu
zao wa Iran na kutoa pongezi kwa nchi
hiyo kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta za maendeleo ikiwemo
sekta ya elimu, afya na nyenginezo.
Dk. Shein
alieleza kuwa Zanzibar inathamini uhusiano na ushirikiano wa kihistoria kati ya
nchi bili hizo na kusisitiza kuwa nchi hiyo imekuwa ikitoa ushirikiano mkubwa
katika sekta ya elimu kwa kutoa nafasi za mafunzo kwa vijana wa Zanzibar kwenda
kusoma nchini humo.
Alisema kuwa Zanzibar
imekuwa na mabadiliko makubwa ya kimaendeleo hivyo kuimarishwa kwa uhusiano kati
yake na Iran kutazidi kukuza maendeleo
hayo hasa katika sekta ya kilimo mafunzo ya ufundi na afya ambapo Iran imeahidi
kuiunga mkono Zanzibar.
Dk. Shein alisema
kuwa katika sekta ya kilimo, hatua kubwa zinazochukuliwa hivi sasa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ni kuimarisha Chuo chake cha utafiti ili kuweza kufanya
tafiti mbali mbali za kilimo hasa tafiti za mbegu bora, hivyo hatua hiyo ya
Iran itasaidia kukuza sekta ya kilimo hapa nchini.
Aidha, Dk. Shein
alisema kuwa mbali na hatua hiyo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa
ikifanya juhudi kubwa katika kuimarisha kilimo cha umwagiliaji maji ikiwa na
lengo la kuhakikisha Zanzibar inazalisha kiwango kikubwa cha chakula ili
kupunguza uagiziaji mkubwa wa chakula kutoka nje ya nchi.
Kwa upande wa
sekta ya kilimo, Dk. Shein alitoa shukurani zake kwa ahadi za Serikali ya Iran
ya kuisaidia Zanzibar vifaa ambavyo vitaingia nchini hivi karibuni, kwa ajili
ya uimarishaji wa Vyuo vyake vya Amali vya Unguja na Pemba kwa lengo la kuinua
sekta hiyo na hatimae kuwasaidia vijana katika kukabiliana na soko la ajira.
Pamoja na hayo,
Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikitilia mkazo
kwa kiasi kikubwa na tayari imeweka mikakati yake katika uimarishaji wa sekta
ya uvuvi hasa ule wa bahari kuu.
Kutokana na hatua
hiyo, Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nafasi nzuri ya kuiunga mkono
Zanzibar katika juhudi hizo hasa ikizingatiwa kuwa nchi hiyo imepiga hatua
kubwa katika sekta ya uvuvi.
Akizungumzia
juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya,
Dk. Shein alisema kuwa tayari hatua nzuri za matibabu ya maradhi yakiwemo
upasuaji wa maradhi ya ubongo na uti wa mgongo zimeshafikiwa hapa Zanzibar huku
juhudi zikiendelea za kuhakikisha maradhi ya mfumo wa utoaji wa haja ndogo nao tiba
yake inaendelea kupatikana hapa nchini.
Kwa kuzingatia
hilo, Dk. Shein alisema kuwa hivi sasa Serikali kupitia Wizara ya Afya imo
katika mikakati ya kuhakikisha tiba ya maradhi ya Saratani pamoja na maradhi ya
Ini nayo inapatikana hapa Zanzibar, juhudi ambazo zinahitaji kuungwa mkono na
nchi wahisani pamoja na washirikika wa maendeleo ikiwemo Iran.
Alisema kuwa tayari
Serikali imeshawapeleka vijana nchini Norway pamoja na Tanzania Bara kwa ajili
ya kujifunza juu ya maradhi ya Saratani na kueleza kuwa kwa matibabu hayo hapa
Zanzibar kutaipunguzia Serikali gharama kubwa za fedha inazotoa kwa ajili ya
wagonjwa ambao huwapeleka nchini India ama Afrika ya Kusini.
Nae Waziri wa
Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mheshimiwa Javad Zarif aliupongeza
uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya nchi hiyo na Zanzibar na
kusisitiza kuwa ziara yake ni miongoni mwa hatua za kukuza uhusiano huo.
Waziri Zarif
alimueleza Dk. Shein kuwa Iran itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika
kuimarisha sekta za maendeleo zikiwemo elimu, afya, uvuvi, kilimo na nyenginezo
huku akisisitiza haja ya kukuza mahusiano kati ya Wizara ya Kilimo ya Zanzibar
na ile ya Iran kwa lengo la kuinua sekta hiyo kwa pande zote mbili.
Pamoja na hayo,
Waziri huyo alimuhakikishia Dk. Shein kuwa Serikali ya Iran itahakikisha
inaendelea kuiunga mkono Elimu ya Vyuo vya Amali na kuahidi kusaidia vifaa kwa
ajili ya vyuo hivyo ambavyo vitawasili hivi karibuni kutokea nchini humo.
Aidha, Waziri
Zarif aliahidi kukuza ushirikiano na Zanzibar katika kuimarisha sekta ya utamaduni na kuahidi kuwa Jumuiya
inayohusiana na Urithi wa Utamaduni ya Iran itakuja Zanzibar kwa lengo la
kukuza uhusiano.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment