Habari za Punde

Hotuba ya Waziri wa Katiba na Sheria kwenye makabidhiano ya katiba inayopendekezwa

HOTUBA YA MHE. DKT. ASHA-ROSE MIGIRO (MB), WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA KATIKA HAFLA FUPI YA KUKABIDHI NAKALA ZA KATIBA INAYOPENDEKEZWA KWA TAASISI MBALIMBALI KATIKA UKUMBI WA KARIMJEE, TAREHE 16 MACHI, 2015

Mhe. Ummy Mwalimu (Mb.), Naibu Waziri wa Katiba na Sheria;
Bi. Maimuna Tarishi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria;
Dkt. Florens Turuka, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu;
Mheshimiwa Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa;
Ndugu Viongozi wote wa Serikali, Vyama Vya Siasa na Taasisi mbalimbali;
Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo wa Wizara ya Katiba na Sheria;
Ndugu Wahariri na wanahabari;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;

As-salamu alaykum

Awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mwingi wa rehema kwa kutujalia kuwa wenye siha njema siku hii ya leo. Pili, Niwashukuru wote kwa kukubali mwaliko wetu wa kuhudhuria hafla hii fupi ya kukabidhi nakala za Katiba Inayopendekezwa. Nakala hizi zitakabidhiwa kwa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, taasisi za elimu ya juu, taasisi za kidini na asasi za kiraia. Kufika kwenu katika hafla hii ni ishara kuwa mnatambua umuhimu wa Katiba kwa mustakabali mwema wa Taifa letu. Pia ni ishara kwamba mmedhamiria kushiriki kikamilifu katika zoezi zima la upatikanaji wa Katiba Mpya ya nchi yetu.

Mabibi na Mabwana,
Kabla ya kukabidhi nakala za Katiba Inayopendekezwa, nichukue fursa hii kueleza kwa kifupi kuhusu hatua iliyofikiwa katika zoezi la kuchapa na kusambaza nakala za Katiba Inayopendekezwa. Kama nilivyosema wiki kadhaa zilizopita, jumla ya nakala milioni 2 za Katiba Inayopendekezwa zimechapishwa na kusambazawa katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Kwa upande wa Zanzibar, nakala laki mbili (200,000) zilisambazwa kwa wananchi kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais. Kwa upande Tanzania Bara, jumla ya nakala 1,141,300 zimesambazwa ambapo kila kata imepelekewa nakala mia tatu (300) chini ya uratibu wa uongozi wa mikoa na wilaya. Nakala 658,700 zilizobaki ndiyo zinasambazwa kwa Wizara, Taasisi za Serikali, asasi za kiraia na makundi mbalimbali. Ni matumaini yangu kuwa wananchi wengi wamepata nakala hizo ambazo zimesambazwa katika maeneo yao. Napenda kuwashukuru viongozi wa mikoa na wilaya waliofanikisha zoezi hili hadi sasa.
Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana

Pamoja na kusambaza nakala za Katiba Inayopendekezwa kwa wananchi kupitia mikoa, wilaya na kata zao, Serikali pia ilichapisha Katiba Inayopendekezwa katika magazeti mbalimbali nchini na kuweka katika tovuti za taasisi zake ikiwemo tovuti ya Wizara ya Katiba na Sheria (www.sheria.go.tz); tovuti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (www.agctz.go.tz) na tovuti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo (www.habari.go.tz). Aidha, baadhi ya vyombo vya habari ikiwemo TBC1 na TBC Taifa vimekuwa vikirusha matangazo mbambali kuhusu Ibara za Katiba Inayopendekezwa. Jitihada zote hizi zinalenga kuwawezesha wananchi kupata fursa za kuielewa Katiba Inayopendekezwa. Kwa niaba ya Serikali, nichukue fursa hii kuvipongeza vyombo vya habari kwa kutekeleza jukumu hili muhimu la taaluma ya habari la kuelimisha umma.

Mabibi na Mabwana,
Baada ya maelezo hayo, niruhusuni niseme machache kuhusu hafla yetu ya leo. Mchakato wa kuandika Katiba Mpya unamhusu kila mwananchi. Ni kutokana na sababu hii, Serikali imesambaza nakala za Katiba Inayopendekezwa moja kwa moja kwa wananchi. Hata hivyo, Serikali inatambua umuhimu na mchango wa taasisi mbalimbali katika kuongeza uelewa wa wananchi wa maudhui ya Katiba Inayopendekezwa.

Hivyo, tumekutana hapa ili Serikali iwakabidhi nakala za Katiba Inayopendekezwa ambazo mtazigawa kwa wadau wenu. Wito wangu kwenu ni kuwasihi wadau wenu waisome kwa makini Katiba Inayopendekezwa ili kuielewa vizuri na hatimaye kushiriki katika Kura ya Maoni muda utakapowadia.

Kwa upande wa Zanzibar, nakala za Katiba Inayopendekezwa kwa ajili ya Wizara, Taasisi za Umma na binafsi, asasi za kiraia na makundi ya kijamii zitasambazwa kwa uratibu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Mabibi na Mabwana,
Pamoja na kukabidhi nakala za Katiba Inayopendekezwa ambazo zimechapishwa katika maandishi ya kawaida, leo pia tutakabidhi nakala za Katiba Inayopendekezwa zilizochapishwa katika maandishi ya nukta nundu na maandishi yaliyokuzwa kwa ajili ya ndugu zetu wenye mahitaji maalum. Lengo la kuchapisha nakala hizi ni kuwawezesha watu wenye mahitaji maalum kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kupata Katiba Mpya. Wito wangu kwa viongozi wao ni kuwa wahakikishe nakala hizi zinawanufaisha wenzao wengi kadri iwezekanavyo.

Mwisho, kupitia kwenu na hadhara hii, ninawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi katika zoezi la kujiandikisha katika Daftari la Wapiga Kura linaloendelea ili watumie haki yao ya kidemokrasia ya kupiga Kura ya Maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa muda utakapowadia.

Asanteni kwa kunisikiliza

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.