Habari za Punde

Waziri Mkuu Mhe.Pinda Asisitiza Uwazi katika Matumizi ya Takwimu Sahihi.

Na. Aron Msigwa  – Dar es salaam.
Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda amesema kuwa Serikali itaendelea  kutoa kipaumbele katika matumizi ya takwimu sahihi na kuweka mifumo mizuri ya kuwarahisishia  wananchi na taasisi mbalimbali kupata takwimu sahihi za masuala mbalimbali kutoka Serikalini ili waweze kupanga mpango ya maendeleo.

Akifungua  Kongamano la Kimataifa la Siku 3 la Wakuu wa Taasisi za Takwimu wa nchi 32 za Afrika na 18 kutoka nje ya Bara la Afrika leo jijini Dar es salaam Mhe. Pinda amesema kuwa nchi za Bara la Afrika ili ziweze kuwa na maendeleo endelevu yanayotafsiriwa lazima zitoe kipaumbele katika matumizi ya Takwimu sahihi. 

Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi za Bara la Afrika zilizopiga hatua kubwa katika kuweka mifumo ya kurahisisha upatikanaji wa takwimu za masuala mbalimbali yakiwemo ya Idadi ya watu, takwimu za masuala ya Afya na masuala mbalimbali yanayohusu shughuli mbalimbali za uchumi wa Kaya binafsi.

“ Mpango wowote ambao hautumii takwimu sahihi  hauwezi kuzaa matunda, Lengo letu Serikali ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na takwimu sahihi kuhusu idadi ya wananchi wetu, sekta ya afya, Elimu, Biashara, Kilimo na mifugo yetu ili tuweze kutatua changamoto mbalimbali zinazotukabili” Amesisitiza.


Ameeleza kuwa upatikanaji wa Takwimu sahihi katika Bara la Afrika hususani nchini Tanzania  katika masuala ya Kilimo, Chakula na Mifugo kutasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima na wafugaji  na kuwawezesha kupunguza idadi ya mifugo waliyonayo kwa  kuwa na ufugaji wenye manufaa na endelevu.

Ametoa wito kwa nchi za Afrika kuendelea kujenga taasisi imara za Takwimu na kuongeza bajeti za kugharamia uwekaji wa mifumo rafiki ya upataji wa takwimu za masuala mbalimbali ili kuwawezesha wananchi  kupata takwimu bila vikwazo na kuweka wazi kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuijengea uwezo Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ili iweze kutekeleza kikamilifu majukumu yake.

Aidha, ameitaka Ofisi ya Taifa ya Takwimu kutoa takwimu rahisi zinazoeleweka na kundi kubwa la watumiaji na kutoa wito kwa  wadau mbalimbali kutoka sekta ya Umma na Binafsi, viongozi  na wanasiasa kujenga utamaduni wa kutumia takwimu kutoka vyanzo sahihi ili taasisi wanazoziongoza ziwe imara na zenye matokeo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.