Habari za Punde

DK.SHEIN Ahudhuria Mazishi ya Wanachama CCM Waliofariki kwa Ajali ya Gari.

STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                                        10 Mei, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amehudhuria mazishi ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi-CCM Wilaya ya Mjini waliofariki kwa ajali ya gari iliyotokea jana huko Mkototoni, Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Wanachama hao walikuwa wakitokea kijiji cha Nungwi ambako walikwenda kufanya mafunzo kwa vitendo ikiwa ni sehemu ya Mafunzo ya Darasa la Itikadi ambayo wamekuwa wakihudhuria.
Katika ajali hiyo iliyotokea katika kijiji cha Mto wa Pwani Mkokotoni watu watatu walifariki dunia na wengine kujeruhiwa ambapo wawili kati yao bado wamelazwa katika hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja mjini Unguja.
Dk. Shein alishiriki mazishi ya Bi Mwanaidi Zamir Haji na Bi Munira Abdalla wote wakaazi wa Mkele Wilaya ya Mjini. Mazishi yao yaliyofanyika kwenye makaburi ya Mwanakwerekwe kwa nyakati tofauti.
Mwana CCM mwingine aliyefariki ni Bibi Mwanahawa Haji Machano mkaazi wa Shaurimoyo mjini Unguja na mazishi yake yamefanyika kijijini kwao Mkwajuni.
Dk. Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar aliwatembelea na kuwafariji majeruhi waliolazwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja kutokana na ajali hiyo pamoja na wagonjwa wengine waliolaza katika wodi za akimamama walikolazwa majeruhi hao.   
Majeruhi hao ni Bi Salhia Sheha Khamis wa Kwamtipura, Bi Sawade Haji Khamis mkaazi wa Shaurimoyo na Bi Mauwa Haji Khamis ambaye amelazwa kutokana na mshituko alioupata baada ya  taarifa za ajali hiyo.
Mazishi hayo yalihudhuria na viongozi na mamnia ya wananchi akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali vuai.

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

                                               

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.