Habari za Punde

CCM kina imani kubwa kwa Umoja wa vijana wa chama UVCCM

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                    30 Juni, 2015
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Chama cha Mapinduzi kimejenga imani kubwa kwa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) na kuwa maratajio yake ni kuona umoja huo unaendelea kuwa chimbuko la viongozi wa chama hicho na nchi kwa jumla.

Akizungumza katika hafla ya futari iliyoandaliwa na Umoja huo iliyofanyika katika viwanja vya Ofisi za EACROTAL, Maisara, Dk. Shein aliupongeza uongozi wa UVCCM kwa kuandaa futari hiyo ambayo imeweza kuwakusanya vijana kutoka maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba pamoja na Tanzania Bara.

Aliwataka kuendeleza utaratibu huo wa kuandaa futari kwa kuwa mbali ya kuwa ni jambo linalompendeza Mwenyezi Mungu na lenye fadhila nyingi lakini pia linaimarisha upendo na mshikamano miongoni mwa vijana na jamii.

Aliueleza uongozi wa huo kuwa kuandaa futari ni neema kubwa na kuwa wana bahati hivi sasa wao wanaweza kufanya mambo kama hayo wakati vijana wenzao zamani hawakuweza kupata fursa kama hizo.


Katika salamu zake fupi katika hafla hiyo Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ambaye alikuwa miongoni mwa waalikwa, alieleza matumaini yake kuwa wananchi wa Zanzibar wataendelea kukiunga mkono Chama cha Mapinduzi kutokana na kazi nzuri iliyofanywa katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi chini uongozi wa Dk. Shein.

“Dk. Shein amefanya kazi nzuri kwa kushirikiana na wananchi kutekeleza Ilani ya Uchaguzi hivyo nina imani kubwa wananchi watamchagua tena muda ukifika” Waziri Mkuu alieleza.

Aliwatakia wana CCM na wananchi wa Zanzibar mgungo mwema wa Ramadhani yenye Baraka tele na kuwatakia sikukuu njema ya Eid el Fitri.

Mbali ya Mheshimiwa Waziri Mkuu hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa CCM na Serikali wakiwemo Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai, Mawaziri wa SMZ na SMT pamoja na mavetarani wa umoja huo.

Akitoa salamu zake kwa wageni na waalikwa Mwenyekiti wa UVCCM Sadifa Juma Khamis aliwashukuru watu mbali mbali waliosaidia kufanikisha hafla hiyo pamoja na waalikwa waliohudhuria.

Alieleza kuwa ni faraja kubwa kwa uongozi wa UVCCM kupewa heshima na viongozi kwa kuhudhuria hafla hiyo ambapo wameungana na vijana kutoka Zanzibar na Tanzania bara kwa pamoja. 


Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.