STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 03 Juni, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewasili nchini Ujerumani leo kuanza ziara ya kikazi ya siku nane nchini humo.
Katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mjini Frankfurt, Dk. Shein alipokelewa na wenyeji wake pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Balozi Philip Marmo.
Hapo kesho Dk. Shein anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Maonesho ya Kimataifa ya 27 ya Muziki na Utamaduni wa Afrika ambayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka katika mji wa Wurzburg ulioko katika jimbo la Bavaria.
Maonesho hayo ambayo ndio makubwa na ya muda mrefu ya muziki na utamaduni wa Afrika katika bara la Ulaya hufanyika wakati wa majira ya joto na huvutia mamia ya maelfu ya wananchi wa Ujerumani na kutoka nchi nyingine duniani.
Kikundi cha Taarab kutoka Zanzibar ni miongoni mwa vikundi vitakavyoshiriki maonesho hayo ya siku nne ambapo pia mara hii kutakuwa na maonesho ya picha kuhusu Zanzibar yaliyoandaliwa na wapiga picha mashuhuri wa kijerumani Mario Gerth and Joachim Schmeisser.
Siku ya Ijumaa tarehe 5 Juni, 2015 Dk. Shein atakutana na kufanya mazungumzo na Mstahiki Meya wa mji wa Wurzburg na baadae atatembelea Taasisi ya Utibabu ya mji huo(Medical Mission Institute).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ataendelea na ziara yake siku ya Jumapili tarehe 07 Juni, 2015 ambapo atakwenda katika mji wa Frankfurt ambako jioni atakutana na watanzania wanaoishi nchini Ujerumani.
Siku inayofuata atakwenda katika mji wa Postdam ambako atatembelea skuli ya Bruno-H-Burgel ambayo ina ushirikiano na skuli ya Mwanakwerekwe Unguja. Baadae jioni atakutana na mabalozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walioko nchini Ujerumani.
Tarehe 09 Juni, 2015 Dk. Shein atakutana na wanachama wa Chama cha Wafanyabiashara wa Ujerumani ambako atatoa hotuba rasmi.
Katika ziara hiyo Dk. Shein amefuatana na mke wake Mama Mwanamwema Shein,Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Said Ali Mbarouk, Waziri wa Kilimo na Maliasili Dk. Sira Ubwa Mamboya, Naibu waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Dk. Mahadhi Juma Maalim na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.
Wengine ni Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa, Uwekezaji na Uchumi Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa, Katibu Mkuu wizara ya Biashara,Viwanda na Masoko Julian Banzi Raphael na Mkurugenzi wa Idara ya Makumbusho Dk. Amina Ameir Issa.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822
No comments:
Post a Comment