Habari za Punde

Walimu watakiwa kuacha kuingiza itikadi zao za kisiasa wanaposomesha somo la uraia

Na Haji Nassor, Pemba  
WAALIMU wa skuli kisiwani Pemba, wanaosomesha somo la uraia, wametakiwa kutoingiza itakadi zao za kisiasa madarasani, kwani kufanya hivyo kutawagawa wanafunzi wao makundi ya itakadi, tofauti jambo ambalo sio sahihi.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Mwanasheria wa kujitegemea kisiwani humo, Mohamed Hassan Ali, alipokuwa akitoa soma la uraia kwa waalimu hao wa wilaya ya Wete, kwenye mkutano ulioandaliwa na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar na kufanyika skuli Chasasa sekondari wilayani humo.
Alisema somo la uraia ni zuri kwa wanafunzi, maana huwapa uweledi wa kujua mambo kadhaa, na kuwa raia wema, endapo waalimu wanaosomesha wataweka kando itikadi zao, wanapokuwa madarasani.
Alisema sio busara hata kidogo kwa waalimu hasa wa somo hilo, kushindwa kujizuia na matamanio yao ya vyama vyao, na kuingiza kwenye masomo wanapokuwa madarasani.
Mwanasheria huyo alieleza kuwa, zipo athari kadhaa pindi waalimu wakieleza hisia zao za kisiasa kwa wanafunzi, ikiwa ni pamoja na wanafunzi kupoteza imani na waalimu wao, sambamba na kutolipokea vyema somo hilo.
“Waalimu kama manavyama vyenu mnavishabikia, basi hilo libakie moyoni tu, lakini sio mnaposomesha mkawadhihirishia wanafunzi, athari yake ni kubwa maana wapo wengine mnaweza kutofautiana’’,alifafanua.

Katika hatua nyengine mwanasheria huyo wa kujitegemea Kisiwani Pemba, alisema suala la uzalendo ndio pekee ambalo kama wananchi watalishiba vyema, nchi inaweza kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo katika Nyanja mbali mbali.
Alifafanua kuwa, uzalendo ndio unaompa mwananchi kulinda rasilimali zake, mipaka, kutoa taarifa za wageni pamoja kutii sheria bila ya shuruti.
Mapema akifungua mafunzo hayo Afisa Mdhamini wizara ya elimu Pemba Salim Kitwana Sururu, aliwataka waalimu hao kuheshimu kazi zao na kujitenda mbali na mkumbo wa kisiasa.
Baadhi ya waalimu hao wakichangia mada kadhaa, walisema bado ipo haja kwa vyombo husika, kuendelea kutoa elimu ya uraia kwa jamii, ili suala la uzalendo lifahamike.

Mada kadhaa zilijadiliwa kwenye mafunzo hayo ya siku mbili, ikiwa ni pamoja na utaratibu wa makosa ya jinai, sheria ya mzanzibar mkaazi, ambapo mafunzo hayo ni mfululizo wa Kituo cha Sheria kuwajengea uwezo waalimu wa skuli za Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.