Habari za Punde

Zoezi la uandikishaji wapiga kura laendelea vizuri Wilaya ya kati

Na Rahma Khamis-Maelezo 

Zoezi la uandikishaji katika Daftari la Wapiga kura kwa Wilaya ya kati Mkoa wa Kusini Unguja limeendelea vyema ambapo Wananchi katika Mkoa huo wamejitokeza kwa wingi.

Aidha hali ya Amani na Utulivu imetanda katika zoezi hilo jambo ambalo limewanya Maafisa wa Tume ya Uchaguzi kufanya kazi yao kwa wepesi.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Kituo cha uandikishaji Shehia ya Binguni Wilayani huko, Khamis Kombo wakati akitoa maelezo kuhusiana na zoezi hilo lililoanza rasmi leo.

Amesema katika uandikishwaji huo wananchi wengi Wake kwa waume wamejitokeza ili kutimiza haki yao ya msingi ya Kidemokrasia.

Aidha amefahamisha kuwa kundi kubwa la Watu wanaojiandikisha katika Zoezi hilo ni Vijana wapya waliotimza sifa za kuandikishwa.

Kwa upande wake Sheha wa Shehia hiyo Ali Yussuf Mussa amefahamisha kuwa watu wamejitokeza bila wasiwasi ili kutimiza lengo la zoezi hilo.

Amesema changamoto kubwa iliyojitokeza ni baadhi ya Vijana kutojua Shehia zao za kujiandikisha na ambapo waliwaelekeza vyema na kupata haki yao.

Aidha amesema katika Shehia yao hakuna Viashiria vyovyote vya uvunjifu wa Amani kama ilivyodaiwa katika Mkoa wa Mjini magharibi na kwamba watu hufuata taratibu na kuandikishwa kwa wepesi.

“Mpaka sasa tunashkuru katika shehia yetu hali ni shuari licha ya mvua kunyesha kwa wakati ule zoezi hilo lilidorora kidogo kutokana na unyeshaji huo lakini kwa sasa zoezi linaendelea kwa salama na amani bila ya matatizo yoyote .’alisema Sheha wa Binguni

Hata hivyo Sheha huyo ametoa wito kwa Wananchi wote wenye sifa za kuandikishwa ambao hawajajitokeza wajitokeze ili kutimiza haki yao ya kidemokrasia.

Amesema hiyo ni fursa pekee kwa kipindi hiki na kwamba yoyote atakayekosa  itamlazimu kusubiri kwa kipindi cha miaka mitano kupata haki hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.