Na Mwandishi Wetu Pemba.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amemuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungao
Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuwathibitishia wananchi na wanaCCM kuondoa shaka
na hofu kwani Serikali yao ipo na itaendelea kuwalinda siku ya uchaguzi Mkuu wa
mwaka huu.
Dk. Shein ambaye ni Mgombea nafasi ya
Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM aliyasema hayo katika hotuba yake aliyoitoa
kwenye mkutano wa kufunga Kampeni ya chama hicho uliofanyika huko katika
viwanja vya Gombani ya Kale, Chake Chake, Pemba uliohudhuriwa na maelfu ya
wananchi na wanaCCM.
Dk. Shein alitoa shukurani kwa wanaCCM na
wananchi kwa kuhudhuria kwa wingi katika mikutano yote tokea tarehe 13 mwezi
huu zilipozinduliwa Kampeni za chama hicho.
Alisema kuwa katika mikutano hiyo ahadi
kwa kila Jimbo, Wilaya hadi Wadi zilitolewa kwa mujibu wa utekelezaji wa Ilani
ya CCM pamoja na kuelezea mambo makubwa kwa Zanzibar.
Alisema kuwa katika miaka mitano ijayo
baada ya kuchaguliwa yeye na chama chake atayatekeleza yale yote yalioahidiwa
na chama chake.
Dk. Shein aliahidi kutokana na Ilani ya
chama hicho kuendeleza kusimamia amani,
utulivu na umoja kwani ndio njia pekee ya kuleta maendeleo.
"Anaezania ni zihaka na anataka
kufanya fujo ajaribu aone",alisema Dk. Shein.
Akilizungumzia suala la karafuu, Dk.
Shein alisema kuwa Ilaini ya CCM kama iluvyoelekeza mwaka 2010, Serikali ya SMZ
italiendeleza zao la karafuu na halitobinafsishwa na kuwataka wananchi wa Pemba
wasikubali kurejeshwa nyuma kwani wanapata asilimia 80 ya soko la dunia la
karafuu zao wanazoziuza na Serikali italiendeleza zao hilo.
Alirejea ahadi yake ya kuwa endapo bei ya
zao hilo itaendelea kuwa hivyo hivyo katika soko la dunia bei ya karafuu
ataiongeza hadi kufikia kilo elfu 20,
badala ya elfu 14 ya bei ya sasa.
Alisema kuwa alitangaza kuwa siku ya
tarehe 12 Januari mwaka huu, kuwa atafuta michango yote ya elimu ya msingi
kuanzia Julai mwaka huu na katika Kampeni hizi alisema kuwa mitihani ya kidatu
cha nne na Sita nazo ameamua wazee wasichangie atakapoingia madarakani.
Pia, arijea kauli yake kuwa mwaka wake wa
mwanzo ataondoa michango ya Sekondari na kueleza kuwa mwaka wa Pili katika uongozi wake atatangaza
huduma za afya bure na kusema kuwa afya na elimu itakuwa bure kama alivyoasisi
Mzee Karume kwani uwezo upo.
Dk. Shein baada ya kusema hayo
alishangazwa na vyama vya upinzani kuhemkwa na kuiga kwa kila analoliahidi.
Alisema kuwa lengo la Serikali ni
kuimarisha zaidi huduma za maji safi na salama ambazo kwa sasa ni alisilimia
87.7, kwa mijini na alisimia 70 vijiji, na kueleza lengo ni kufikia asilimia 97
mijini na 80 kwa vijiji na hilo
linawezekana.
Aidha, Dk. Shein alieleza jinsi
alivyojiandaa na suala la ajira kwa vijana sambamba na mikakati ya ujenzi wa
vyuo vya amali kikiwemo kitakachojengwa huko Mtambwe kwa Pemba na Makunduchi
kwa Unguja.
Pamoja na hayo, alisema kuwa Unguja na
Pemba ni visiwa vilivyozungukwa na bahari na asilimia ya watu wake wengi ni
wavuvi na kusema kuwa Serikali atakayoiongoza itaimarisha uvuvi wa bahari kuu
kwa mashirikiano ya Serikali mbili kwa
nguvu zote ili kuitumia bahari kuu kwa kuweka miradi ikiwa ni pamoja na
kuwakaribisha wawekezaji ili itoe tija ambapo Makao Makuu yake hivi sasa yapo
Fumba Zanzibar.
Dk. Shein, aliwataka wana CCM na wananchi
kuwachagua viongozi wa CCM, Pia, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa shukurani
kwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa mashirikiano makubwa aliyompa tokea wakiwa
wote Mawaziri sambamba na kuusimamia Muungano katika kipindi chake chote cha
urais.
Dk. Shein alisema kuwa Dk. Kikwete ametoa
mchango mkubwa sana katika kuendeleza suala la mafuta na gesi kwa upande wa
Zanzibar na kuwataka wananchi na WanaCCM kwenda kupiga kura kwa lengo la
kuyalinda Mapinduzi pamoja na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisema kuwa yuko tayari kuiongoza
Zanzibar na afya yake inamruhusu na kusisitiza kuwa mafanikio yote tokea
1964 yamefanywa kwa pamoja na kuwaeleza
kuwa bila ya CCM yote hayo yasingelipatikana huku akiwaeleza wananchi kuwa viongozi wa upinzani hawana vipaji vya
kuongoza.
Nae Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete alisema kuwa
CCM itaendelea kuongoza Jamhuri ya Tanzania na pamoja na Zanzibar na kuwaombea
kura wagombea wote wa CCM.
Aliwataka wananchi na wanaCCM kukichagua
chama hicho kwani kimeongoza vizuri kwani nchi iko salama na imetulia na watu
wanafanya shughuli zao bila ya bughuza na kueleza kuwa kama ingeongozwa vibaya
hatua hiyo isingelifikia.
Alisema kuwa kuna kila sababu ya kumchagua
Dk. Shein kuwa Rais wa Zanzibar kwani Zanzibar iko salama na ameiongoza kwa
umakini sana na kwa upande wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Dk. Shein amekuwa
makini katika serikali hiyo na kama si umakini wake hata miaka mitano
isingelimaliza.
Alisema kuwa ameongoza kwa umakini
Serikali hiyo na kusisitiza kuwa maendeleo yapo yanatyoonekana katika kila
nyanja kwenye sekta zote na hata kwenye vipato vya watu.
Rais Kikwete alisisitiza kuwa hakuna
mbadala wa Dk. Shein, na Maalim Seif si mbadala wa Dk. Shein kwani Maalim Seif
angezoza Serikali hiyo hata siku tatu zisingefika kwani si mstahamilivu.
Alisema kuwa kiongozi huyo wa upinzania
katika lugha zake anazozungumza haunganishi watu badala yake anawachonganisha
na kusisitiza kuwa Dk. Shein ndio anaeweza kufanya kazi ya urais wa Zanzibar.
Rais Kikwete aliwataka wananchi na
wanaCCM wamchague Dk. Shein pamoja na Wawakilishi, Wabunge na Madiwani wengi wa
CCM ili aweze kuongoza vizuri, na wengine waendelee kuwa washiriki.
Alisema kuwa kwa upande wa mgombe nafasi
ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, John Pombe
Magufuli, hilo ndio chaguo la wengi na
kueleza kuwa wapinzani wake hivi sasa wamekalia kuti kavu na kuwataka wananchi
wakitaka mambo mazuri kwa kuitaka Zanzibar na Tanzania kwa jumla ziendelee
kustawi na kuwa na maendeleo wawachague Dk. Shein na Magufuli.
Alieleza kuwa CCM katika kumteua John
Magufuli haikufanya kosa kwani ni
muadilifu kwani angekuwa na tatizo lolote la uadilifu asingelipata nafasi hiyo.
Alisema kuwa Dk. Magufuli ni hodari,
muaminifu, muadilifu na wanaomsema vibaya ni wale waliojaa hofu katika maisha
yao ya ujanja ujanja.
Alisema kuwa katika Wizara zote
alizofanya kazi Magufuli,amethibitisha ukomavu wake pamoja na ujasiri na
mvumilivu wake sambamba na hayo ni muumini wa
Muungano wa Tanzania na mpenda maendeleo kwani katika hotuba zake
anaonesha jinsi anavyokereketwa na maendeleo na iwapo atapewa nafasi hiyo
mafanikio makubwa yatapatikana Tanzania.
Dk. Kikwete alisema kuwa Magufuli
anaamini umoja na tokea ameanza Kampeni zake hajajinadi juu ya dini yake wala
ukabila wake na kusema kuwa Tanzania inataka kiongozi anaesema mamenao yake
akayaamini yeye mwenyewe.
Alisisitiza kuwa uchaguzi utakuwa wa
amani, na kueleza kuwa anaetayaarisha matayarisho ya Uchaguzi ni Tume ya
Uchaguzi, na Serikali kazi yake ni kuwapa fedha kwa ajili ya shughuli zao
lakini kuhakikisha kuna amani na utulivu siku ya kupiga kura ni jukumu la
Serikali na yeye ndio amiri Jeshi Mkuu.
"Tutahakikisha kuwa uchaguzi utakuwa
wa amani na utulivu na anayetaka kufanya majaribio ya utayari wetu na ajaribu,
natakata Watanzania wapate fursa ya kuwachagua viongozi wanaotaka",alisema
Dk. Kikwete.
"Tarehe 25 jitokezeni hakutatokea
lolote...kuungana kwa vyama vinne ndio kuonesha dalili za
kushindwa"alisema Rais Kikwete.
Aliwataka wanaCCM na wananchi kujitokeza
kwenda kupiga kura na hakutatokea lolote na atakae jaribu ataona na kutumia
fursa hiyo kuwaombea kura kutaka kupewa kura Dk. Shein, Dk. Magufuli, Samia,
Wabunge, Wawakilishi na Madiwani.
Nae Mgombe Mwenza wa Urais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, akitoa salamu za ndugu zao wa Tanzania Bara alisema kuwa
wao wanasema kuwa CCM mbele kwa mbele na kusema kuwa Pemba ya 2010 si ya leo.
Alisema kuwa CCM mwaka huu wameamua
kutimiza nembo ya Serikali ya Adama na Hawa na kusema kuwa Adama na Hawa ni
Magufuli na Samia na wako yatayari kukabidhiwa Tanzania na mali asili zake kwa
lengo la kuitumikia.
Aliwakataka akina mama bila ya kujali
vyama vyao wapige kura CCM kwa sababu CCM imeamua mwaka huu kumpa heshima kubwa
mwanamke kuwa Mgombea Mwenza.
Aliwataka akina mama kukamatana na
kuuonesha ulimwengu kuwa wanawake wakipewa nafasi wanaweza kuiongoza Tanzania.
Aliishukuru amwamu ya nne ya Urais wa Dk.
Kikwete kwa kujenga miundombinu kwa kutoa fursa kwa ajira na kusema kuwa
Tanzania nzima imeunganishwa kwa barabara za lami na kueleza kuwa zikitoa
huduma na kuwawezesha wananchi kusafirisha bidhaa zao, sambamba na kuinuka kwa soko la ajira.
Alisema kuwa Ilani ya CCM imeonesha jinsi
vijana wa wanawake walivyopewa kipaumbele ili kuweza kupata fursa na kueleza
kwa upande wa walemavu nao watapewa nafasi bila ya ubaguzi.
Kwa upande wa wazee alisema kuwa, wazee
wote ambao walikuwa wakulima na hawapati mafao watapewa sawa na wale waliokuwa
wakifanya kazi Serikalini ambapo tayari kwa upande wa Zanzibar mchakato huo
umeanza.
Alisema mkuwa CCM ina mpango kazi kwa
yale yote ambayo yatafanywa katika awamu na kuonesha kuwa rasilimali fedha za
kuendeleza ahadi hizo zitapatikana.
Alisema kuwa CCM ina mfumo na muuundo
unaoelekewaka na kusisitiza kuwa mchakato ulioendeshwa katika chama hicho hadi
kupatikanwa kwa wagombea na tofauti na jinsi walivyopatikana wagombea katika
vyama vyengine vya siasa ambao ni wasanii na kusisitiza kuwa wapewe kura CCM
wenye uzoefu wa kuongoza.
Samia alisema kuwa katika kuendesha
Serikali hawezi kupewa mtu ambae sifa zake hazina uwezo, alisema kuwa CCM ina
lengo la kulinda na kudumisha Mapinduzi na Muuungano wa Jamhuri ya Tanzania.
Mgombea huyo Mwenza wa CCM alisema kuwa
ili walinde usalama wa Tanzania pamoja na kulinda Muungano na kwa umoja watu
waweze kuishi kwa kusikilizana na kupendana. "Watanzania hawako tayari
kuwapa kura wasanii"alisema Samia.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Idd akitoa salamu kwa wananchi aliwataka wajiandae kwa ushindi
wakiwemo akina mama kwa kupaka hina na kutia wanja kusubiri ushindi wa CCM.
Alisema kuwa chama cha CUF katika
uchaguzi wa mwaka huu kitashindwa na Katibu Mkuu wake utakuwa ndio mwaka wake
wa mwisho wa siasa kama alivyoeleza mwenyewe aliposema kuwa hata Ukatibu Mkuu
wa chama hicho anauwacha.
Alisema kuwa viongozi wa CUF wamekuwa
wakiwadanganya sana wananchi na kuendedelea kueleza kuwa wafuasi wa chama hicho
wamejiandaa kuleta vurugu na wamejiandaa kuleta mamluki kutoka nchi jirani kwa
lengo la kuja kufanya vurugu kisiwani humo.
Kwa upande wa Unguja alisema kuwa tayari
Serikali imeshapata taarifa kuwa kuna watu wamejificha kwenye nyumba ya
kiongozi mmoja wa chama hicho huko Mombasa Unguja kwa lengo la kuja kufanya
fujo siku ya uchaguzi na kusema kuwa hawatahi kufanya kwani taarifa zipo na
watashughulikiwa na vyombo husika.
Aliwataka wanaCCM na wananchi kutoogopa
kwenda kupiga kura kwani ulinzi utawekwa kila mahala ili kuhakikisha kila mtu
mwenye haki ya kupiga kura anapiga kura kwa kupata haki yake hiyo ya msingi.
Balozi Seif alisema kuwa matusi
anayotukanwa na viongozi wa CUF jibu lake ni siku ya tarehe 25 siku ya kupiga
kura. Aidha, Balozi Seif alisema kuwa wenye familia ya Marehemu Mzee Karume
hawataki kubandikwa picha zilizowekwa na CUF zinazomuonesha Maalim Seif na
Marehemu Mzee Abeid Karume zikimuonesha Maalim Seif akisema kuwa atavaa viatu
vya muasisi huyo.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar
Vuai Ali Vuai alitoa shukurani kwa washiriki na jamii yote waliotoa misaada yao
mbali mbali katika Kampeni hiyo kwa chama hicho kutokana na mashirikiano makubwa
waliyoyatoa wananchi, wanaCCM, wasanii, waandishi wa habari na wengineo.
Vuai alisema kuwa Dk. Shein hana ubaguzi,
hana choyo na muumini wa CCM ameweza kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar, huku
akimpongeza Dk. Jakaya Marisho Kikwete alimpongeza kwa kusimamia vyema
kuondokana na migogoro ya Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu huyo, aliwataka wanaCCM
kutochokozeka kwani wafuasi wa chama cha CUF wameamua kwa makusudi kufanya
vurugu kwani wameshajua kuwa watashindwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini
Pemba, Mberwa Hamad aliwaeleza wanaCCM kuwa ushindi kwa chama hicho hauepukiki
katika uchaguzi wa mwaka huu hivyo aliwaondoa hofu na kuwataka kwenda
kuwachagua viongozi wa CCM siku ya Jumaapili ya tarehe 25, Oktoba mwaka huu.
No comments:
Post a Comment