Na Mwandishi Wetu,
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein ameweka jiwe la
msingi katika Maskani mpya ya Ukombozi wa Vijana iliyopo Muyuni na kusema kuwa
Maskani ni sehemu ya kujenga umoja na mshikamano huku akieleza kuwa CCM
itaendelea kuwa namba moja katika kuongoza na kuleta maendeleo hapa nchini.
Dk. Shein ambaye pia, ni Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyasema hayo mara baada ya kuweka jiwe
la msingi katika Maskani hiyo iliyopo Muyuni, Jimbo la Makunduchi Mkoa wa
Kusini Unguja na kusema kuwa CCM haina mbadala.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema
kuwa CCM itabaki kuwa namba moja kwani hakuna chama hata kimoja kinachoweza
kufanana nacho kutokana na kuimarika kwake, historia yake na sambamba na
maendeleo inayoendelea kuwaletea wananchi.
"Chama cha Mapinduzi kitaendelea
kuwa imara na hakuna wa kukichezea hata mmoja kwani chama hichi si chama cha
mchezo" Alisema Dk.Shein.
Aidha,
Dk. Shein alisema kuwa ujenzi wa maskani ni miongoni mwa hatua za
kuimarisha chama hivyo kuna kila sababu za kujenga maskani nzuri na za kisasa
ambazo zitawasaidia wanaCCM kukaa na kujadili mambo yao ya maendeleo ya chama
chao.
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwahakikishia
wanamaskani wa Ukombozi wa Vijana kuwa atawaunga mkono katika ujenzi wa maskani
yao hiyo ili iwe kubwa na ya kisasa na kuwa ya mfano katika Jimbo hilo.
Mapema Wanamaskani hao walieleza kuwa maskani
yao hiyo ilianza na wanachama 27 na hivi sasa wapo wanachama 55 ambao kila
kukicha wanaendelea kujiunga na maskani hiyo ambapo pia walitumia fursa hiyo
kutoa shukurani kwa wale wote waliochangia ujenzi wao huo akiwemo Mwakilishi wa
Jimbo hilo Haroun Ali Suleiman.
No comments:
Post a Comment