Na: Hassan Hamad (OMKR)
Chama Cha Wananchi CUF, kimelazimika kufanya mkutano wake wa hadhara katika fukwe za Nungwi, baada ya kiwanja cha Sokoni Nungwi kuonekana kuwa kidogo kutokana na idadi kubwa ya wanachama waliojitokeza kwenye mkutano huo.
Katika mkutano huo wa kampeni Jimbo la Nungwi, mgeni rasmi alikuwa Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama hicho Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad.
Akizungumza katika mkutano huo, Maalim Seif amesema hakuna sababu kwa Chama hicho kukosa ushindi katika uchaguzi mkuu wa tarehe 25 mwezi huu kutokana na kuungwa mkono na wanachama wengi katika maeneo yote ya Zanzibar.
Ameelezea kufurahishwa na jinsi wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja walivyohamasika kukiunga mkono Chama hicho, na kwamba huo ni ushahidi tosha wa kukiweka chama hicho madarakani.
Amesema iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar, atashughulikia migogoro ya ardhi inayojitokeza katika Mkoa huo, baada ya maeneo kadhaa ya wananchi kupewa wawekezaji bila ya utaratibu unaokubalika.
Aidha amerejea kauli yake ya kuwarejesha Zanzibar Masheikh wa Jumuiya ya Uamsho wanaoshikiliwa Tanzania Bara, wiki moja baada ya kuapishwa kuwa Rais na kwamba kesi yao itasikilizwa katika Mahakama ya Zanzibar.
Amemshauri Rais wa Zanzibar kuwadhibiti viongozi wa CCM wenye dhamira ya kuleta vurugu nchini, ili uchaguzi ujao ufanyike katika hali ya amani na usalama.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Zanzibar Bw. Salum Mwalim, amewataka mawakala kuwa makini katika kusimamia kura za wagombea wao.
Amesema vyama vinavyounda Umoja wa UKAWA havitomvumilia wakala atakayefanya uzembe katika usimamizi wa kura, na kwamba atakayebainika atawajibishwa.
Kabla ya Mkutano huo Maalim Seif alitembelea na kufungua barza mbali mbali za Chama hicho ikiwemo barza ya New Singapore katika kijiji cha Bwereu Kitogani, na kuelezea kufarajika kwake kutokana na namna vijana walivyojipanga kukipatia chama hicho ushindi katika uchaguzi ujao.
Wazee wa Nungwi kwa upande wao wamemkabidhi jahazi Maalim Seif, ili aweze kuliongoza hadi kufikia kupatikana kwa mamlaka kamili ya Zanzibar.
No comments:
Post a Comment