STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 13.10.2015
WANANCHI na WanaCCM wa Mkoa wa Kusini Unguja wamepongeza juhudi
zilizochukuliwa na Dk. Shein katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ikiwa
ni pamoja na kuwasogezea huduma za maji kwa asilimia 80 katika Jimbo la Chwaka
huku wakimuhakikishia kiongozi huyo kuendelea kumuunga mkono.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika
mkutano wa Kampeni ya uchaguzi wa CCM uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi na
wanaCCM uliofanyika uwanja wa mpira
Chwaka, Jimbo la Chwaka, Wilaya ya Kati Unguja, Mkoa wa Kusini Unguja, viongozi
wa CCM waliohudhuria mkutano huo kwa nyakati tofauti walisema kuna CCM ndio
chama pekee kinachojali maslahi wa wananchi.
Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Kati Hassan
Mrisho Vuai alimpongeza Dk. Shein kwa kutekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya
CCM, walieleza kuwa Dk. Shein ameweza akutekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi
sambamba na kuongoza vyema Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Alieleza kuwa sekta mbali mbali za
maendeleo zimeimarika ikiwemo sekta ya maji ambayo imeimarika kwa asilimi 80
ambapo tatizo la maji katika Jimbo la Chwaka limepungua kwa kiasi kikubwa.
Aidha, kiongozi huyo alieleza kuwa CCM ndicho
chama kilicholeta ukombozi, misingi ya kutela umoja, amani na maendeleo kwa Watanzania
na hawana sababu ya kuacha kukiunga mkono chama hicho kwani wazee wao wamewaachia
chama hicho na wataendelea kukiunga mkono daima.
Alieleza kuwa upinzani si ubabe, na
kuwataka wafuasi wa chama cha CUF wanapokwenda katika Mikoa yao waweke heshima
na kusema haifai kuanza kutoa matusi hasa pale wanapowaona wanachama wa CCM, na
kusema kuwa wao wanafuata sheria na taratibu za Tume na kuwaomba wanapokwenda katika
maeneo yao wajue kuwa kuna watu na
heshima zao na kusisitiza kuwa 'kuku hafundishwi kutaga.
Aidha, viongozi wa CCM Mkoa huo wa Kusini
Unguja walimpongeza na kumueleza kuwa Kusini watatoa kura za ndio siku ya
tarehe 25 kwa viongozi wote wa CCM.
Viongozi wa chama wa Mkoa huo walieleza
kuwa wanachama wa CCM hawataki shari wala ugomvi licha ya dalili mbali mbali za
shairi na ugomvi zinazooneshwa na wafusi wa vyama vya upinzani dhidi yao
kikiwemo chama vha CUF.
Nae Modelin Kastiko alieleza mafanikio
yaliopatikana katika Jimbo la Chwaka na kueleza bahati kubwa waliyoipata
wanachakwa kwa kujengewa Chuo cha Maendeleo ya Fedha katika kijiji hicho.
Nae Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM ambaye
pia, ni Waziri Kiongiozi mstaafu Shamsi Vuai Nahodha, aliwaeleza wanaCCM kuwa
wana kazi kubwa ya kulinda Mapinduzi na kuulinda Muungano kwani anaamini kuwa
maadui wa Mapinduzi na Muungano bado wapo.
Alisema kuwa mwaka 1995 kuna kiongozi
mmoja wa CUF wakati wakihitimisha Kampeni za chama hicho alisema kuwa siku hiyo
ndio mwisho wa Serikali inayoongozwa na mtu mweusi, na kusema kuwa wakipata
Serikali watayaondosha Mapinduzi kwani hayana maana na yamepitwa na wakati.
Hivyo aliwaeleza wananchi wanaoyataka
Mapinduzi na wanaoujali na kuupenda Muungano ni lazima wamchague Dk. Shein, kwani ana historia ya
kuupenda Muungano wa Serikali mbili, kuyapenda Mapinduzi, na anawahemshimu
waaasisi wa Mungano na Mapinduzi hivyo kuna kila sababu ya kumchague Dk. Shein.
Alisisitiza kuwa hakuna kazi ngumu ya
kuongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama ilivyo hivi sasa kwani kuna viongozi
wanaowadanganya wananchi na kusema uongozo huku akisema kuwa kazi ya kuongoza
Serikali hiyo ni lazima apatikane mtu mwenye sifa kama Dk. Shein.
Kutokana na hilo aliwaomba wananchi na
wanaCCM kumchagua Dk. Shein na kusema kuwa iwapo wakimchagua watakuwa wanaunga
mkono Sera za uhakika na zinazotekelezeka.
Alisema kuwa kama anatafutwa rais wa
kuleta maendeleo basi Dk. Shein anatosha.
Waziri wa Maji, Ardhi na Nishati ambaye pia, ni Mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya Taifa, Ramadhan Abdalla Shaaban nae aliendelea kulielezea suala la
mafuta na kuwasisitiza wananchi kutodanganyika juu ya suala hilo kuwatokana na
maelezo ya viongozi wa kambi ya upinzani.
Waziri Shaaban alisema kuwa mgombea urais
kupitia chama cha CUF Maalim Seif Sharif
Hamad hivi karibuni alieleza kuwa Katiba inayopendekezwa haikutoa fursa ya
kuchimba mafuta, na kutumia fursa hiyo kuisoma Katiba inayopendekezwa na mambo
yanayohusu mambo ya Muungano ambapo suala la mafuta halipo.
Alieleza kuwa Kifungu cha 26 cha Katiba
hiyo inayopendekezwa kimeelezea vizuri suala hilo na kusisitiza kuwa Sheria
zote za mafuta zitatungwa na Baraza la Wawakilishi kwa mujibu wa Katiba
inayopendekezwa huku akieleza kuwa suala la mafuta linashughulikiwa na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema kuwa hakuna haja ya kupewa kura
za ndio viongozi ambao wamekuwa wakiwadanganya wananchi na kuwataka wananchi
wasidanganyike huku akisisitiza kuwa mafuta ya Zanzibar yatachimbwa na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar na hivi sasa mchakato unaendelea.
Nae Waziri wa Kilimo na Maliasili Dk.
Sira Ubwa Mwamboya alisikitishwa na baadhi ya madaktari ambao wamekuwa
wakifanya mradi wa kuwatolesha fedha wananchi wakati tayari Dk. Shein
ameshatangazia kuwa matibabu kwa wazazi hivi sasa yanatolewa bure.
Alisema kuwa miongoni mwa Madaktari hao
ni Dk. Mwana ambae hivi sasa amekuwa akisimama kwenye majukwaa ya mikutano ya
siasa kupitia chama cha CUF na kusema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
haikufanya kitu kwenye Wizara hiyo wakati yeye mwenyewe alikuwa akifanya kazi
hospitalini hapo na kufanya biashara za vifaa vya uzazi hospitalini hapo
sambamba na kuwatolesha fedha wazazi wanaofika hospitalini hapo kujifungua
kinyume na sheria za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Nae Balozi Ali Karume, alisema kuwa
anaamini kuwa Dk. Shein atamalizia vizuri kazi ambazo ameshaanza kuzifanya,
hivyo ana kila sababu ya kuchaguliwa tena kuiongoza Zanzibar.
Alisema kuwa Dk. Shein ana sifa zote za
kuendelea kuwa Rais wa Zanzibar na kusisitiza kuwa hakuna maendeleo makubwa
kama kuishi katika nchi yenye amani na utulivu kama ilivyo Zanzibar chini ya
uongozi wa Dk. Shein.
Rajab Mkasaba,
Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment