Habari za Punde

Chuo cha Takwimu Mashariki Mwa Afrika Chafanya Mahafali ya Kwanza ya Shahada ya Takwimu Rasmin.


 Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue akiwa kwenye maandamano na wahitimu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika kilichopo maeneo ya Changanyikeni  jijini Dar es Salaam.Kulia kwake ni  Mkuu wa Chuo hicho, Professa Innocent Ngalinda. 
 Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue akihutubia kwenye mahafali ya kwanza ya Shahada ya Takwimu Rasmi ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika kilichopo maeneo ya Changanyikeni  jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika pamoja na wahitimu wa Shahada ya kwanza ya Takwimu Rasmi katika chuo hicho kilichopo maeneo ya Changanyikeni  jijini Dar es Salaam.
(Picha na Emmanuel Ghula)

Na Emmanuel Ghula –NBS Dar es Salaam. 
KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amevitaka vyuo na taasisi za elimu nchini kuhakikisha vinatoa mafunzo bora yanayoendana na mahitaji ya soko la ajira. 

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika mahafali ya kwanza ya Shahada ya Takwimu Rasmi katika Chuo Cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC), Sefue amesema ni vyema vyuo na taasisi za elimu kuhakikisha vinafanya tafiti kujua mahitaji ya wataalamu wanaotakiwa na kutoa mafunzo yanayoendana na soko la ajira. 

“Nchi yetu inahitaji kuwa na watalaamu wa fani mbalimbali hivyo ni wajibu wa vyuo vya elimu ambavyo ndio wazalishaji wa wataalamu hao kuhakikisha vinatoa wataalamu wenye ujuzi wa kutosha unaoendana na mahitaji ya soko la ajira ndani na nje ya nchi,” alisema Sefue. 

Sefue alisema kutokana na umuhimu wa takwimu katika maendeleo, Serikali imekuwa mstari wa mbele kupitia Wizara ya Fedha kuhakikisha inakisaidia chuo hicho kukabiliana na changamoto zinazokikabili ikiwemo uhaba wa fedha za kuendeshea chuo hicho.

Aidha, alisema chuo hicho kuanza kutoa shahada ni hatua kubwa kwasababu chuo hicho ndio tegemeo la Afrika katika kuzalisha watakwimu wanaosaidia katika ukusanyaji wa takwimu bora zinazotumika katika kupanga na kupima utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo.

Aidha, Sefue amekitaka chuo hicho kubuni miradi mbalimbali itakayosaidia kujipatia fedha kwa ajili ya kutatua baadhi ya changamoto zinazojitokeza chuoni hapo. 

Alisema Chuo Cha Takwimu cha EASTC mwaka huu kimefikisha miaka hamsini ya utoaji wa mafunzo ya Takwimu na wataalamu mbalimbali wa takwimu wanaofanya kazi Serikalini wamepitia hapo na hivyo ni wajibu wa Serikali kuhakikisha inakiendeleza ili kiwe kituo bora zaidi kwa utoaji wa watakwimu waliobobea.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho, Professa Innocent Ngalinda amesema chuo hicho kimejipanga vyema kuhakikisha kinaendelea kuzalisha watakwimu bora na wenye weledi katika fani ya takwimu. 

“Hivi sasa tumefikia hatua kubwa sana ya kuanza kutoa wahitimu wa Shahada ya kwanza ya Takwimu Rasmi, tutaendelea kuwa mhimili wa uzalishaji wa wataalamu hawa muhimu katika maendeleo ya nchi yetu na bara la Afrika kwa ujumla,” alisema Professa Ngalinda.

Professa Ngalinda alisema chuo hicho kitaendelea kufanya kazi kwa karibu na nchi wanachama ili kuhakikisha wahitimu wake wanakuwa chachu ya maendeleo kwa kusaidia ukusanyaji wa takwimu bora na kwa wakati ili zitumike katika kupanga na kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo.

Jumla ya wanafunzi 29 wamehitimu na kutunukiwa Shahada ya kwanza ya Takwimu Rasmi katika mahafali hayo ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.