Habari za Punde

Dk Shein ashiriki maadhimisho ya siku ya mzazoezi kitaifa


 
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                   1.1.2016
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameshiriki kikamilifu katika maadhimisho ya siku ya mazoezi Kitaifa yalioanza katika viwanja vya Tumbaku hadi uwanja wa Amaan na kusisitiza kuwa mazoezi ni tiba mbadala ya maradhi mbali mbali yanayojulikana na yasiyojulikana ambayo yanaisumbua jamii katika maisha yao ya kila siku.

Katika hotuba yake aliyoitoa mara baada ya kupokea maandamano ya  vilabu mbali mbali vya mazoezi vya hapa Unguja, Pemba pamoja na vilabu kutoka Tanzania Bara, huko katika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar, Dk. Shein alieleza kuwa mazoezi ni kinga na yanapunguza uwezekano wa kupata maradhi mbali mbali.

Akiyataja baadhi ya maradhi ambayo yanaweza kuondoshwa kwa kufanya mazoezi Dk. Shein alisema  ni pamoja na maradhi ya saratani, kisukari, ugonjwa wa moyo na shindikizo la damu sambamba na kusaidia kupunguza uzito na unene uliokithiri.

Dk. Shein aliwataka wananchi na wanamichezo wasingojee mpaka wapate maradhi ndipo waanze kufanya mazoezi  na badala yake wajipangie muda wa mazoezi angalau dakika 30 kwa siku kwani kuna faida kubwa katika kukabiliana na maradhi yanayoathiri afya.


“Iwapo hakuna tatizo tujipe mazoea ya kutembea kwa miguu kwa safari zetu za karibu na hata kuepuka kuanda ‘lifti’ kama unapokwenda pana uwezekano wa kufika kwa ngazi ya kawaida kwani yote haya yana faida katika kuimarisha afya zetu”, alisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alieleza kufurahishwa sana na utaratibu wa kufanya mazoezi kupitia vilabu kwani njia hiyo ina faida nyingi zaidi badala ya kufanya mazoezi kwa mtu mmoja mmoja ambapo pia hatua hiyo, inaimarisha umoja na mshikamano.

Dk. Shein, alitumia fursa hiyo kuwapongeza akina mama ambao zamani hawakuwa wakionekana kuwa wengi katika shughuli za michezo na hasa wanapofikia umri wa watu wazima lakini siku hizi kwa sababu ya kupata mwamko na kufahamu umuhimu wa mazoezi wamekuwa wengi kama walivyojitokeza katika maadhimisho hayo.

Kwa upande wa wastaafu, Dk. Shein alieleza kufurahishwa kwake kwa kuwaona baadhi ya wastaafu walioshiriki mazoezi hayo na kueleza kuwa anaamini mazoezi yana mchango mkubwa kwa wastaafu kwa kuimarisha afya na furaha katika maisha yao.

Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini umuhimu wa kuiendeleza sekta ya michezo kwa kuzingatia historia ya Zanzibar ya kuwa na vipaji vya michezo mbali mbali na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya michezo kwa kukamilisha kazi ya uwekaji wa mpira wa kukimbilia katika uwanja wa Gombani na ujenzi wa uwanja wa Mao-tse-tung kwa kushirikiana na Serikali ya China.

Dk. Shein alieleza kuridhishwa kwake na  Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo katika kutekeleza lengo la kurudisha vuguvugu la michezo katika maskuli kwa lengo la kuibua vipaji.

Alisema kuwa katika mradi huo ambao matayarisho yake yameanza tangu mwezi Mei mwaka jana na unatarajiwa kuanza mwezi Februari mwaka huu na unatarajiwa kumaliza mwaka 2017, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itachangia Shilingi milioni 480 na fedha zote zilizobaki zitatolewa na Serikali ya Watu wa China.

Katika mradi wa ujenzi wa mji wa kisasa katika maeneo ya Fumba ambao matayarisho yake yamekwishaanza, pia, utajumuisha ujenzi wa kiwanja cha michezo wenye uwezo wa kuchukua watu 45,000.

Pia, Dk. Shein alisema kuwa  katika eneo la Kijini Matemwe katika Mkoa wa Kaskazini Unguja Kampuni ya ‘Penny Royal’ inayojenga mji wa kisasa katika eneo hilo, vile vile itajenga kiwanja cha Kimataifa cha mchezo wa gofu chenye juma la vishimo 18.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza umuhimu wa kuzingatia nidhamu katika michezo ili kuepuka migogoro hasa katika vilabu vya michezo hapa Zanzibar kwani migogoro hupunguza nidhamu michezoni na huviza maendeleo ya michezo.

Dk. Shein alisema kuwa yeye akiwa ni mwaka michezo anahuzunishwa na kusikitishwa sana na migogoro na mivutano michezoni kwani sio jambo linalotoa taswira nzuri ya maendeleo ya michezo hapa Zanzibar.

“Nawasihi wanamichezo wenzangu tufanye kila linalowezekana kuepuka mizozo isiyo ya lazima michezoni ili kwa pamoja tuweze kufikia azma yetu ya kurudisha hadhi ya Zanzibar katika tasnia ya michezo”,alisema Dk. Shein.

Dk. Shein aliwaeleza wanamichezo hao wa mazoezi ya viungo Zanzibar kuwa ataendelea kushirikiana nao na hata wanapotaka vifaa vya michezo ataendelea kuwatafutia pamoja na misaada mengine kwa kutambua kuwa wanakila sababu ya kudeka kwa Rais wao.

Aidha, Dk. Shein alimuagiza Waziri wa Kilimo na Maliasili Dk. Sira Ubwa Mamboya, kukutana na uongozi wa Chama cha Mchezo wa Mazoezi ya Viungo Zanzibar (ZABESA) kwa lengo la kuwakabidhi eneo la kilimo waliloliomba na kuwataka wachague ni kilimo cha aina gani wanakusudia kulima.

Dk. Shein alitoa pongezi kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kwa kushirikiana na (ZABESA) pamoja na Baraza la Michezo pamoja na wanavilabu wote kwa kufanikisha bonaza hilo linalofanyika kila ifikapo Januari 1 ya kila mwaka.

Dk. Shein pia, alitoa wito kwa wanamichezo wote nchini pamoja na wananchi kujitokeza kwa wingi kuangalia michuano ya Kombe la Mapinduzi ambayo ni maalumu kwa kuadhimisha Mapinduzi matukufu ya Januari 12, mwaka 1964 huku akisisitiza kuwa timu za Zanzibar zihakikishe kombe la Mapinduzi linabaki nyumbani.

Nae Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Zanzibar (BMZ) Sharifa Khamis,  aliwaeleza wanamichezo hao pamoja na wananchi walioshiriki maadhimisho ya siku ya mazoezi kitaifa kuwa  Dk. Shein ndie aliyedhamini maadhimisho hayo na kumpongeza kwa juhudi zake hizo huku akisisitiza kuwa wanamichezo wataendelea kudeka kwa Rais wao huyo kwani anawajali.

Nao wanavilabu haokutoka vikundi zaidi ya 40 kutoka Unguja, Pemba na Tanzania Bara katika risala yao walitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kushirikiana nao katika bonaza hilo sambamba na kuendelea kuwaunga mkono huku wakiwasisitiza wananchi kufanya mazoezi na kuiomba Serikali kuweka siku maalum kwa watendaji wote Serikalini kufanya mazoezi.

Katika bonanza hilo Dk. Shein alikabidhi vyeti kwa vilabu mbali mbali vya Unguja, Pemba na Tanzania Bara, Shirika la Bandari, Kocha wa kike ambaye ni muasisi wa bonaza hilo Bi Nasra Juma Ramadhan.

Viongozi mbali mbali walishiriki katika bonanza hilo la maadhimisho ya siku ya mazoezi na kuungana na Rais kwa matembezi tokea viwanja vya Tumbaku hadi uwanja wa Aman mjini Unguja, akiwemo Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.