Anaitwa Mama Magreth (Kushoto) ambae ni mwenyeji wa Meatu Mkoani Simu. Miaka kadhaa iliyopita alifika Jijini Mwanza kwa ajili ya kutafuta maisha. Anasema aliuza Makochi aliyokuwa nayo na kusafiri hadi Jijini Mwanza, hii ikiwa ni baada ya mume wake kumtelekeza nyumbani.
Maisha ya Jijini Mwanza yaligeuka ndivyo sivyo kwa Mama Magreth na sasa ni miongoni mwa akina mama ambao ukipita katikati ya Jiji la Mwanza unakutana nao wakiwa wamejipanga barabarani kwa ajili ya kuomba pesa kutoka kwa wasamalia wema ili kujikimu katika maisha yao.
Kwa ufupi ni kwamba, upeo wake wa kutafuta pesa kwa njia nyingine umefikia kikomo na pengine utafufuka upya pale atakapopewa elimu ya nini afanye ili kuondokana na utegemezi mtaani.
Kwake maisha yamekuwa magumu na makazi yake yamekuwa ni nje ya maduka Jijini Mwanza huku akiwa na mtoto mdogo alie na umri chini ya miaka mitatu.
Hana ulemavu wa viungo lakini ni kama ameathirika kisaikolojia baada ya kutengana na mmewe. Hakika wapo wengi Jijini Mwanza na hata nchini kote ambao ni kama Mama Mage wanaohitaji kuamshwa kifikra.Tuwasaidie ili tuwe na jamii isiyo na utegemezi.
Ni mtoto mdogo alie na umri wa Miaka 16, mkazi wa Maduka Tisa Ilemela Mkoani Mwanza (Kushoto). Mwaka 2013 alihitimu darasa la saba lakini alishindwa kujiunga na Kidato cha kwanza kutokana na ugumu wa maisha licha ya kwamba alifaulu kwenda kidato cha kwanza.
"Baba aliachana na mama na kwa kuwa mama anaumwa niliamua kuja hapa (Jijini Mwanza) kwa ajili ya kutafuta pesa ya kutumia nyumbani (anajishughulisha na biashara ya machinga). Kidogo ninachokipata napeleka nyumbani kwa ajili ya matumizi. Lakini kwa sasa hali inazidi kuwa ngumu maana mgambo wa Jiji wanatusumbua sana". Anasema mtoto huyo ambae alidokeza kuwa ana ndoto za kuwa mmoja wa wafanyabiashara wakubwa nchini.
Mmoja wa wakazi wa Jiji la Mwanza (Kulia) anasema wazazi wanapotengana wanasababisha ongezeko kubwa la watoto mitaani na hata wakati mwingine idadi ya akina mama wanaoomba omba mtaani inaongezeka.
Anasema kama migogoro ya kifamilia haitakomeshwa, idadi ya watoto mitaani pamoja na akina mama kutanda barabarani maeneo ya mjini wakiomba pesa kutoka kwa wasamalia wema itazidi kushuhudiwa ikiongezeka kila kukicha.
Imeandaliwa na George Binagi wa Binagi Media Group.
No comments:
Post a Comment