Habari za Punde

Wakulima Watakiwa Kutumia Kilimo cha Umwagiliaji ili Kupata Mazao Yatakayokidhi Soko.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imewashauri wakulima kutumia teknolojia ya kilimo cha umwagiliaji maji hasa katika maeneo ya maweni ili kupata mazao yatakayokidhi katika soko la utalii nchini.
Ushauri huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Zanzibar, Juma Ali Juma katika ziara maalum ya kuwatembelea wakulima wa kilimo cha maweni huko Bwejuu Mkoa wa Kusini Unguja.
Wakulima hao wanalima Tungule,  Matikiti maji, bilinganyi, pilipili boga, ndimu, Papai na vitunguu maji.
Amesema endapo wakulima watafanya kilimo hicho kwa kufuata ushauri wa kitaalamu watapata mazao mengi na yanayokubalika katika soko na kujikwamua kiuchumi.
Juma amesema lengo la serikali ni kuhakikisha dhana ya mapinduzi ya kilimo inatekelezwa kwa vitendo kwa kuwapatia elimu ya kitaalamu wakulima wanaolima kilimo mbali mbali kikiwemo cha maweni ili waweze kuzalisha mazao bora na mengi yanayotosheleza soko la ndani ya nchi na kupunguza uagiziaji mazao nje ya Zanzibar.
Naibu Katibu mkuu huyo emefafanua kuwa kilimo hicho kinachostawi katika maeneo ya mawezi ni cha aina za mboga mboga, hivyo wakulima wanatakiwa kuendelea kubuni mbinu za mbali mbali za uzalilishaji mazao hayo kwa wingi ili kwenda sambamba na fursa ya masoko ya ndani.
 Aidha amewasihi vijana nchini kujiajiri wenyewe kupitia kilimo hicho kwa lengo la kupambana na changamoto ya ukosefu wa ajira badala ya kukimbilia mijini wakati fursa za kujiajiri zipo nyingi vijijini.
Kwa upande wake Mkulima wa kilimo hicho kutoka Shehia ya Bwejuu Mohamed Nuru Mohamed, amesema  licha ya kilimo cha maweni kujenga matumaini makubwa ya mafanikio bado wanahitaji msaada wa kitaalamu utakaowasaidia kutumia teknolojia ya umwagiliaji maji kupata mazao mengi zaidi ya wanayopata hivi sasa.
Nae Hassan Ame Hassan, ambaye ni Mkulima wa mazao mbali mbali ya Mboga mboga amekiri kilimo hicho kuwa na manufaa kwani mpaka sasa ana uwezo wa kuhudumia familia yake vizuri yenye watu 17, ambapo kabla ya kuanza kilimo hicho halikua anaishi maisha ya tabu.
Amesema uzuri wa kilimo cha kutumia teknolojia ya umwagiliaji maji ni kuwa hakitegemei msimu wa mvua bali unalima wakati wote kama una miundo mbinu mizuri ya upatikanaji wa maji na mipira imara ya kusambazia maji hayo maarufu kama “Drip”.
Amezitaja changamoto zinazowakabili katika kilimo hicho kuwa ni pamoja na ukosefu wa huduma ya umeme pamoja na miundombinu ya barabara kwa ajili ya kusafirisha mazao yao kuyapeleka katika masoko.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.