STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 10 Machi, 2016
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amekutana na Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam Mheshimiwa Truong Tang Sang ambaye yuko nchini kwa ziara rasmi ya kiserikali ya siku nne kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli.
Katika mazungumzo hayo rasmi yaliyofayika jana Ikulu jijini Dar es salaam, Dk. Shein amesema uhusiano mzuri wa kisiasa na kidiplomasia kati ya Tanzania na Vietman unatoa fursa ya kipekee kwa nchi mbili hizo kuimarisha ushirikiano katika maeneo mengine ambayo yataharakisha maendeleo na kujenga ustawi wa wananchi wa pande mbili hizo.
Aliongeza kuwa Zanzibar na Tanzania kwa jumla zina mengi ya kujifunza kutoka Vietnam hivyo alihimiza ushirikiano zaidi kati ya Zanzibar na nchi hiyo katika nyanja mbalimbali ikiwemo kilimo, uvuvi na ufugaji wa samaki, utalii,biashara na uwezeshaji wananchi vijijini.
Dk. Shein na Rais Truong walikubaliana kuwa mapendekezo ya miradi miwili mikubwa katika kilimo na uvuvi kati ya Zanzibar na Vietnam ambayo ni matokeo ya ziara ya Dk. Shein aliyoifanya nchini Vietnam mwaka 2012 utekelezaji wake ushirikishe pia sekta binafsi za nchi hizo.
Alieleza kuwa mapendekezo ya miradi hiyo ni hatua moja muhimu kuelekea ushirikiano wa muda mrefu wa kiuchumi na maendeleo kati ya Zanzibar na nchi hiyo.
Alifafanua kuwa azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuhakikisha usalama wa chakula na kwa kuwa chakula kikuu cha wananchi wa Zanzibar ni mchele, mkakati wa serikali ni kuimarisha kilimo cha mpunga hivyo ingependa kutumia uzoefu na maarifa kutoka Vietnam kufanikisha azma hiyo.
Dk. Shein alimweleza Rais Truong kuwa Zanzibar ina fursa nyingi za uwekezaji na kwamba milango iko wazi kwa wawekezaji kutoka Vietnam kuwekeza katika sekta mbali mbali zikiwemo kilimo, uvuvi wa bahari kuu pamoja na utalii.
Katika mazungumzo hayo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alimueleza Rais Truong kuwa amefurahishwa na ziara yake nchini Tanzania ambapo imewawezesha kukutana kwa mara ya pili baada ya ziara yake aliyoifanya nchini Vietnam mwaka 2012.
Dk. Shein alibainisha kuwa Vietnam na Tanzania ni marafiki kwa kweli na daima serikali na wananchi wa nchi hizo wameonesha kwa vitendo utayari wao wa kuzidi kuimarisha uhusiano na ushirikiano wao.
Kwa upande wake Rais wa Vietnam Mheshimiwa Truong alieleza kuwa ziara yake nchini Tanzania imekuwa ya mafanikio makubwa na anaamini kuwa imefungua ukurasa mpya katika kuimarisha uhusiano wa nchi yake na Tanzania.
Alibanisha kuwa mazungumzo yake na Rais Magufuli pamoja na makubaliano yaliyofikiwa yataongeza kasi ya ushirikiano katika maeneo mbali mbali ya ushirikiano ikiwemo biashara.
Rais Truong alisema kuwa iko haja ya kukuza kiwango cha biashara kati ya nchi yake na Tanzania na kuongeza kuwa anatambua fursa nyingi za uwekezaji zilizopo Zanzibar na Tanzania kwa jumla na kwamba mafanikio ya baadhi ya wawekezaji waliowekeza nchini yataongeza hamasa ya wawekezaji kutoka Vietnam kuwekeza Tanzania.
Nchi yake alisema iko tayari kushirikiana na Zanzibar katika sekta za kilimo, Utalii, uvuvi na katika maeneo mengine na kusisitiza Vietnam ingependa kuona ushirikiano madhubuti zaidi na Zanzibar.
Rais Troung alipendekeza kuwepo uhusiano kati ya miji ya Zanzibar na Vietnam pendekezo ambalo lilikubaliwa na Dk. Shein.
Katika mazungumzo hayo Dk. Shein alifuatana na Mawaziri na Makatibu wa wakuu wa Wizara za Kilimo, Afya, Biashara, Uvuvi na Mifugo pamoja na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora Mheshimiwa Dk. Mwinyihaji Makame.
No comments:
Post a Comment