Habari za Punde

SMZ Yaahidi Kuendeleza Mipango ya Uchumi Inayochangiwa Kimataifa.

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendelea kuhakikisha mipango yote ya kimaendeleo inayochagizwa na malengo endelevu ya kimataifa inatekelezwa kwa vitendo ili wananchi waweze kunufaika.

Imesema katika malengo ya milennia ya 2015 serikali ilifanikiwa katika baadhi ya sekta zikiwemo sekta za elimu, afya na miundo mbinu hatua zinazotakiwa kuendelea kupewa kipaumbele na wadau wa maendeleo.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar, Juma Reli katika Mkutano wa wadau wa sekta za maendeleo nchini wanaojadili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) visiwani humo. Mkutano huo ulifanyika katika Hoteli ya Zanzibar Ocean View.

Alisema licha ya kuwepo na changamoto mbali mbali za kiutendaji katika utekelezaji wa mipango hiyo ikiwemo suala la wananchi kutokuwa na uelewa mzuri wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya dunia bado mamlaka husika zinaendelea kutoa elimu hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida akitoa neno la ukaribisho katika Mkutano wa wadau wa sekta za maendeleo nchini wanaojadili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) visiwani Zanzibar ambao umeandaliwa na ESRF kwa kushirikiana na Tume ya Mipango Zanzibar chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini.

Reli alieleza kwamba malengo na mipango mbalimbali ya maendeleo ni kuwasaidia wananchi wa Zanzibar waweze kuondokana na tatizo sugu la umaskini, magonjwa na changamoto za kiusalama.

“Katika MDG tumeweza kufanikiwa kwa baadhi ya malengo ikiwemo suala la elimu na afya lakini kuna mengine bado hatukuweza kufanikiwa kuyafikia na kwa sasa tunaendelea na malengo mapya ya SDG’s ambayo tunatakiwa kuyafanyia kazi ili yaende sambamba na mipango ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar." alisema Reli.

Aidha alisema bado wanajadiliana ni kwa namna gani mipango ya kimataifa tutaiingiza katika sera na mipango yetu ya kimaendeleo ili wananchi waweze kunufaika na fursa hizo za kimaendeleo na kiuchumi kwa ufanisi zaidi.

Alisema utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu SDG’s ambayo ni 17 yanatakiwa kupewa kipaumbele kwani yanagusa nyanja mbalimbali za kijamii yakiwemo maisha halisi ya wananchi wanaostahiki kunufaika na fursa na mahitaji muhimu ya kibinadamu.
Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN) Ofisi ya Zanzibar, Anna Senga akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Alvaro Rodriguez katika mkutano wa wadau wa sekta za maendeleo nchini kujadili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) visiwani Zanzibar.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafti, Uchumi na Kijamii nchini ( ESRF), Dkt.Tausi Kida akitoa neno la ukaribisho alisema, ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika SDG’s ni vyema sera na mipango endelevu ya nchi husika iweke vipaumbele vya kukuza uchumi kuanzia ngazi za chini

Kida alieleza kwamba katika utekelezaji wa SDG’s lazima kuwepo na mpango endelevu wa ufuatiliaji kuanzia ngazi za chini hadi taifa kwa lengo la kuhakikisha malengo hayo yanatekelezwa kwa mujibu wa matakwa ya malengo ya kimataifa.

Naye Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN), Ofisi ya Zanzibar, Anna Senga alisema endapo malengo ya dunia yataweza kutekelezwa ipasavyo Zanzibar itaweza kupunguza changamoto mbali mbali zinazokabili sekta za kijamii na kiuchumi.

Alisema UN itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika utekelezaji wa SDG’s kama ilivyokuwa katika utekelezaji wa malengo ya dunia MDG’s yaliyopita ili serikali iweze kufikia ngazi za chini kwa kuinua kipato cha wananchi kiendane na ukuaji wa uchumi wa nchi.
Mgeni rasmi Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar, Juma Reli akitoa nasha wakati akifungua mkutano wa siku moja wa wadau wa sekta za maendeleo nchini wa kujadili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) visiwani Zanzibar ambao umefanyika katika Hoteli ya Zanzibar Ocean View.

Senga aliishauri serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuendelea kuwashirikisha wananchi wa ngazi za chini katika kupanga na kutekeleza maendeleo yao katika maeneo husika ya wananchi.

“Changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya kimataifa ili yaendane na mipango ya maendeleo ya serikali ni upungufu wa ushirikishwaji wa wananchi ama jamii husika na wengine hawafikiwi kabisa katika maeneo yao jambo linalotakiwa kufanyiwa kazi kwa haraka katika kutekeleza kwa vitendo Malengo ya Maendeleo Endelevu ya SDG’s”, alifafanua Senga.

Naye Mshauri wa Masuala ya Uchumi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) Tanzania, Rogers Dhliwayo alisema Malengo ya Maendeleo Endelevu SDG’s yanatakiwa yawekewe vipaumbele mbalimbali vya takwimu na tafti za kiuchumi katika maeneo tofauti ya jamii ili malengo endelevu yaweze kuwafikia walengwa.

Kwa upade wa washiriki wa mkutano huo kwa nyakati tofauti walisema kwamba mipango mbalimbali ya kimaendeleo inayopangwa na serikali inatakiwa kuwekewa vipaumbele kwa wananchi badala ya utekelezaji na tathimini kubakia ngazi za serikali kuu pekee.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida (kushoto) na Mkurugenzi wa Kupunguza Umaskini na Kuinua Uchumi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Anna Mwasha wakinakili mambo muhimu wakati mgeni rasmi (hayupo piichani) akitoa nasaha zake.

Walisema kwamba katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu SDG’s ni lazima kutengeneza mpango mkakati wa mawasiliano wa masuala ya utamaduni, mila na desturi za jamii husika ambapo mipango hiyo inatakiwa kutekelezwa ili iwe rahisi wananchi kufahamu vizuri umuhimu wa mipango hiyo.

Washiriki hao walisema katika utekelezaji wa mipango hiyo ni lazima kuwepo na mikakati ya makusudi ya kuhakikisha changamoto ya umasikini uliokithiri unapungua kulingana na mikakati mbalimbali inayowekwa na vipaumbele vya kimataifa ili viweze kutekelezwa kwa vitendo na nchi husika.

Aidha wameshauri kwamba katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu SDG’s ni lazima kuzingatia suala la serikali za mitaa, kutumia lugha nyepesi katika mawasiliano, kufanya marejeo katika maandiko ya baadhi ya waasisi wa kitaifa akiwemo Mwalimu Nyerere na kufanya utafiti juu ya matumizi sahihi ya Rasilimali.
Pichani juu na chini ni wadau wa sekta za maendeleo visiwani Zanzibar walioshiriki katika mkutano wa kujadili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) visiwani humo ambao umefanyika katika Hoteli ya Zanzibar Ocean View.

Sambamba na hayo wamesema katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) ni lazima kuweka kipaumbele kwa makundi maalum ya watu wenye mahitaji maalum wakiwemo Watu wenye Ulemavu.

Warsha hiyo imeandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF) ambapo imewakutanisha wadau mbalimbali kujadili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) visiwani Zanzibar na kufadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).


Mshauri wa Masuala ya Uchumi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) Tanzania, Rogers Dhliwayo akiwasilisha mada katika mkutano wa wadau wa sekta za maendeleo nchini wa kujadili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) visiwani Zanzibar.

Kutoka kushoto ni Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN) Ofisi ya Zanzibar, Anna Senga, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Celestine Mushy, mgeni rasmi Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar, Juma Reli, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Kupunguza Umaskini na Kuinua Uchumi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Anna Mwasha wakiwa meza kuu.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto ya visiwani Zanzibar, Mauwa Makame Rajab akitoa maoni katika mkutano wa wadau wa sekta za maendeleo nchini wa kujadili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) visiwani Zanzibar uliofanyika katika Hoteli ya Zanzibar Ocean View.
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Celestine Mushy (kushoto) na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar, Juma Reli wakisikiliza maoni ya wadau yaliyokuwa yakiwasishwa kwenye mkutano kuelekea utekelezaji wa SDGs.
Bw. Sefu Mwinyi kutoka Tume ya Mipango Zanzibar akiwasilisha maoni yake katika mkutano huo uliowakutanisha wadau wa sekta za maendeleo visiwani Zanzibar.
Katibu Mkuu Wizara ya ya Elimu na Mafunzo ya Amali visiwani Zanzibar, Khadija Juma (kushoto) akichangia hoja katika mkutano huo. Kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora visiwani Zanzibar, Asha Abdallah Ali.
Mgeni rasmi katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.