Habari za Punde

Dk Shein aishukuru timu ya madaktari bingwa wa watoto kutoka Misri

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                   20 Agosti, 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameushukuru ujumbe wa madaktari bingwa wa upasuaji wa watoto kutoka Hospitali ya El Shatby iliyo chini ya Chuo Kikuu cha Alexandria nchini Misri kwa mchango wake mkubwa wa kuimarisha huduma za afya kwa watoto Zanzibar.

Ujumbe huo ambao umeongozwa na Mkuu wa Idara ya upasuaji watoto wa hospitali hiyo Profesa Saber Waheeb ulikuwepo nchini kwa wiki moja ambapo waliwafanyia upasuaji watoto 25 waliohitaji matibabu kwa upasuaji.

“Nimevutiwa na kutiwa moyo sana na kazi yenu ya kusaidia watoto wenye mahitaji ya upasuaji na kuwa tunathamini sana mchango wenu” Dk. Shein aliueleza ujumbe Ofisini kwake Ikulu leo.

Dk. Shein aliongeza kuwa katika utumishi wake akiwa mtaalamu wa afya amefanyakazi na wataalamu wengi wa afya kutoka nchini Misri na amekuwa akivutiwa sana na utaalamu na kuridhishwa na huduma wanazozitoa.

“Tunatarajia makubaliano ya ushirikiano kati ya Hospitali yenu na Hospitali yetu ya Mnazi Mmoja yatakuwa na manufaa zaidi kwetu sote na tungependa kuona yanapanuka zaidi katika maeneo mengine” Dk. Shein alisema.

Alifafanua kuwa chini ya ushirikiano huo Chuo Kikuu cha Alexandria kingeangalia uwezekano wa kusaidia kuimarisha skuli ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar-SUZA ambayo imeanzishwa miaka michache iliyopita.

“Mnaweza kukisaidia kwa kuwa na mpango wa kusaidia kufundisha kwa vipindi vifupi vifupi kwa kuanzia na hata kushirikiana katika kufanya tafiti mbalimbali ambazo ni muhimu katika kusaidia kutatua matatizo yanayokabili sekta ya afya” Dk. Shein alifafanua.

Dk. Shein aliueleza ushirikiano huo kati ya Hospitali ya El Shatby na Hospitali ya Mnazi Mmoja ni kieleleza cha uhusiano mzuri uliopo kati ya Misri na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Zanzibar na Misri zimekuwa na uhusiano wa karne nyingi na ndio maana zimekuwa zikishirikiana katika mambo mbalimbali kwa kuwa tuna tamaduni na mila zinazofanana” Dk. Shein alisema.

Kwa upande wake Profesa Waheeb alimueleza Dk. Shein kuwa Timu ya wataalamu kutoka hospitali hiyo iliyo chini ya Chuo Kikuu cha Alexandria imeshafanya ziara tano kama hizo nchini Tanzania.

Alibainisha kwa miaka mitatu mfululizo Timu hiyo imefanya ziara hizo za matibabu mara tano ambapo mbili zimefanyika Tanzania Bara na tatu zimefanyika Zanzibar.

Katika kusaidia kuimarisha hudumu za afya kwa watoto katika Hospitali ya Mnazi Mmoja Profesa Waheeb aliahidi kusaidia mafunzo kwa watumishi wa afya wanaohudumia watoto.

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Issa Haji Ussi Gavu, Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee na viongozi wa Wizara ya Afya wakiongozwa na Naibu Waziri Bi Harusi Said Suleiman.  

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.