Habari za Punde

Dk Shein: Tutahakikisha matangazo ya ZBC TV yanakuwa bora ifikapo mwishoni wa mwaka

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                        21 Septemba, 2016
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewahakikishia watumishi wa Shirika la Utangaza Zanzibar (ZBC) kuwa Serikali itafanya kila linalowezekana kuona kuwa matangazo ya televisheni ya Shirika hilo yanaimarika ifikapo tarehe 31 Disemba, 2016.

Akizungumza na watumishi katika vitengo mbalimbali vya shirika la utangazaji ZBC Televisheni leo wakati alipofanya ziara ya ghafla, Dk. Shein aliutaka uongozi wa shirika na Wizara husika kuchukua hatua za haraka kushughulikia matatizo madogo madogo yanayowakabili watumishi wa kituo hicho wakiwemo watangazaji wake.

“Tuna orodha ndefu ya mahitaji yenu na sisi tunaifanyia kazi kwa kukamilisha mambo ya msingi katika hatua za awali ili lengo la kuleta mabadiliko ya awamu ya kwanza ilifikapo Disemba 31 mwaka huu litimie” Dk. Shein aliwaambia watumishi hao.

Alifafanua katika awamu hiyo lengo ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwisho wa mwezi Disemba mwaka huu matangazo ya ZBC televisheni yanakuwa katika mfumo wa digitali uliokamilika.

Katika ziara hiyo ambayo uongozi wa shirika hawakuitarajia, Dk. Shein alitembelea vitengo vyote vilivyopo katika jumba la utangazaji la shirika hilo maarufu ‘Karume House’ lililopo Mnazi Mmoja na kuangalia hali halisi ya utendaji kazi, vifaa na jengo la kituo hicho.

Katika ziara hiyo mbali ya uongozi wa shirika, Dk. Shein alisitikiliza maelezo kutoka kwa wakuu wa vitengo na watumishi wa shirika hilo kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili huku akionesha kuguswa na hali ya mambo yalivyo katika kituo hicho ambacho ni moja ya vituo vikongwe vya televisheni barani Afrika.

Alikubaliana na hoja mbali mbali mbali zilizoelezwa na watumishi hao na kueleza mipango ya serikali ya namna ya kuliimarisha upya shirika hilo ili liweze kutoa matangazo yanayolingana hadhi yake na yanakidhi mahitaji ya wakati uliopo.

Alifafanua kuwa ongeza kuwa shirika hilo linakabiliwa na changamoto nyingi na serikali imedhamiria kuzitafutia ufumbuzi hatua kwa hatua lakini lengo letu lake la kwanza ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwisho wa mwezi Disemba mwaka huu matangazo ya ZBC televisheni yanakuwa katika mfumo wa digitali uliokamilika

Miongoni mwa changamoto ambazo watumishi wa shirika hilo walimueleza Mheshimiwa Rais ni kukosa mafunzo, uchakavu na upungufu wa vitendea kazi, usafiri, watumishi wengi wenye taaluma kustaafu na mahitaji mengine madogo madogo hasa kwa watangazaji wa shirika hilo.

Kwa hivyo mheshimiwa Rais aliwataka watumishi hao kufanyakazi kwa bidii na kuahidi kuwa baadhi ya changamoto hizo zitatafutiwa ufumbuzi katika kipindi kifupi kijacho.

Katika ziara hiyo Dk. Shein aliutaka uongozi wa shirika kuimarisha studio ya shirika hilo kwa kuzingatia historia ya chumba cha studio hiyo ambayo kabla ya kuazishwa televisheni Zanzibar ulikuwa ukumbi wa Manispaa(municipal hall).

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa ZBC Bi Aiman Duwe alieleza kuwa pamoja na changamoto zilizopo bado watumishi wa shirika hilo wamekuwa wakijitahidi kufanya kazi kwa ueledi ili kukidhi matarajio ya watazamaji wao.

Katika ziara hiyo walikuweko viongozi mbali mbali wakiwemo Katibu Mkuu Kiongozi Dk… Abdulhamid Yahya Mzee na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo Omar Hassan Omar.


Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.