STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 4.10.2016
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa
miezi miwili kwa Taasisi zote zinazohusika na ujenzi wa ofisi ya Zimamoto
zinazojengwa katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume,
Zanzibar ziwe zimeshakamilisha ujenzi huo.
Dk. Shein alitoa agizo
hilo mara baada ya kutembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya
Zimamoto huko katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, ambapo
ujenzi huo unaonekana kusuasua kwa muda mrefu.
Kutokana na kusuasua kwa
ujenzi huo ndipo kulikompelekea Dk. Shein kutoa agizo hilo kwa Taasisi zote
husika kukamilisha ujenzi huo ndani ya kipindi hicho hasa ikizingatiwa kuwa wahusika
walipewa agizo hilo mwezi Mei mwaka jana wakati Mheshimiwa Rais alipofanya
ziara kutembelea uwanja huo.
Dk. Shein alisema kuwa
tokea kipindi hicho hadi leo bado ujenzi
huo haujaanza na kusisitiza ni lazima ukakamilike katika kipindi hicho hasa
ikizingatiwa kuwa tayari serikali imeshatoa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni
3.5 kwa ajili ya ununuzi wa gari za zimamoto pamoja na dola milioni 1.5 ambazo
zimetolewa na Benki ya dunia kwa ajili ya nununuzi wa gari hizo.
Dk. Shein alisisitiza kuwa
tarehe kama ya leo mwezi wa Disemba mwaka huu atarudi tena kwa ajili ya
kuangalia jengo hilo likiwa limekamilika kwani anatambua kuwa Serikali ina
fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi huo ila kuna changamoto ndani ya taasisi
hizo zinazokwaza utekelezaji wa agizo lake.
“Tusifanye kazi kwa
utamaduni tuliozoea, nimekupeni muda mrefu miezi miwili, malizeni mkimaliza
nitakuja, hamkunialika nitakuja mkinialika nitakuja…pesa zipo lakini
hamjaziomba”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alieleza
kuwa kukamilika kwa ujenzi huo kutakuwa na tija kubwa Serikali hasa
ikizingatiwa kuwa ujenzi wa jengo jipya la abiria katika uwanja huo
linatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
Nae Waziri wa Ncho Ofisi
ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar
Khair alimueleza Dk. Shein haja ya kuwepo kwa mashirikiano kati ya taasisi zote
zinazosimamia ujenzi huo hasa kwa upande wa Wizara ya Mawasiliano, Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Zanzibar na Idara ya Zimamoto ili kufanikisha jukumu hilo.
Mapema Kamishna wa Idara
ya Zimamoto Zanzibar Ali Abdalla Malimosi alimueleza Dk. Shein changamoto mbali
mbali zinazoikabili kikosi hicho katika eneo hilo la uwanja wa ndege wa
Kimataifa wa Abeid Amani Karume.
Wakati
huo huo,
Dk. Shein alifika Mbweni kukagua eneo la mradi wa ujenzi wa nyumba za kisasa zinazojengwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii
Zanzibar (ZSSF) na kupongeza juhudi zinazochukuliwa na Mfuko huo katika
kuimarishaji miradi mbali mbali ya maendeleo yenye tija.
Dk. Shein alisema kuwa
ndani ya miaka sita ya uongozi wake, Mfuko huo umeweza kufanya vizuri kwa kuanzisha
miradi kadhaa ukiwemo ujenzi wa viwanja vya kufurahishia watoto Kariakoo
Ungujua na Tibirinzi Pemba, ujenzi wa
mnara wa kumbukumbu ya miaka 50 ya Mapinduzi, pamoja na ujenzi wa jumba la
treni unaotarajiwa kuanza mwezi ujao.
Katika maelezo yake Dk.
Shein alisema kuwa ujenzi huo wa nyumba za kisasa una faida kubwa ambao
unatarajiwa kuwa na nyumba 252 zikiwemo za vyumba vitatu, viwili na vinne.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji
wa Mfuko huo Abdulwakil Haji Hafidh alimueleza Dk. Shein kuwa ujenzi huo wa
majengo 18 ya ghorofa unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2018 na
unatarajiwa kugharimu Tsh. bilioni 43.
Mkurugenzi huyo alieleza
kuwa mradi
huo utakuwa na Mabloki 18 ya Majengo ya Ghorofa Saba zenye Fleti 252 ambao utajengwa
kwa awamu tatu tofauti ambapo tayari wameshaanza kujenga Mabloki Matano yenye
Nyumba 70.
Alieleza pia kuwa tayari
kwa hatua za awali shirika limeshatumia shilingi bilioni 8 ambapo tayari ujenzi
huo ukiwa unaendelea nyumba 55 zimeshapata wanunuzi kutoka sehemu mbali mbali
na hivi sasa wanafunga mikataba nao.
Mkurugenzi Mtendaji huyo alieleza
kuwa mradi wa nyumba za Mbweni mwanzoni ulipangwa kwa ajili ya wananchi wenye vipato
vya kati na chini ambazo zitauzwa kati ya shilingi milioni 168 hadi 249 lakini imebainika
kuwa watu wengi hawatazimudu hivyo Mfuko umeamua kujenga za kipato cha chini huko
eneo la Tunguu.
Alibainisha kuwa awamu ya
kwanza ya mradi huo unaojumuisha ujenzi wa magorofa matano itakamilika mezi
Aprili mwakani na kufuatiwa na ujenzi wa magorofa mengine 8 katika awamu ya
pili na awamu ya tatu ni ya ujenzi wa magorofa yatakayo baki.
Alieleza kuwa
tayari wameshaanza kutafuta wanunuzi na wameshatembelea sehemu mbali mbali za
ndani na nje kwa ajili ya kujitangaza
huku akimueleza kuwa nyumba hizo zitakuwa na maeneo ya huduma muhimu yakiwemo maduka pamoja na ukumbi
mkubwa wa kisasa ambao utajengwa katika eneo hilo.
Mkurugenzi huyo alisema
kuwa juhudi za makusudi zimefanywa katika kuhakikisha ujenzi wa nyumba hizo
unakuwa imara zaidi chini ya Kampuni ya ujenzi ‘Dezo Civil Construction Limited
yenye makao makuu yake Jijini Dar-es Salaam.
“Ujenzi wetu tumeupanga kuutekeleza kwa awamu tatu
ambapo awamu ya kwanza tutajenga Bloki Tano, ile ya Pili pia tutajenga Bloki
Tano na ya mwisho tutamalizia kwa Bloki Nane “, alisema Mkurugenzi huyo wa
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar.
Akitoa maelezo
wakati akimtembeza kwenye ujenzi wa nyumba hizo Meneja Mipango,Uwekezaji na Utafiti wa Mfuko wa
Hifadhi ya Jamii Zanzibar Khalifa Muumin Hilal alimuhakikishia Dk. Shein umadhubuti mkubwa wa nyumba hizo.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment