Habari za Punde

Wananchi wa Kijiji cha Jambiani Waridhshwa na Uamuzi wa Serikali Kuweka Siku ya Afya Vijijini.

Na Miza Kona Maelezo Zanzibar.
Wananchi wa kijiji cha Jambiani wameeleza kuridhishwa na uamuzi wa Serikali wa kuweka siku maalum ya Afya Vijijini ambapo hupata fursa ya kuonana na kufanyiwa uchunguzi na Madaktari Bingwa wa maradhi tofati na kupatiwa matibabu bila malipo.

Akizungumza katika siku ya Afya ya Kijiji cha Jambiani Sheha wa Shehia ya Jambiani Kibigija Ali Mtumwa Hassani amesema uamuzi huo umewasaidia wananchi kujua afya zao bila ya kutumia gharama ya kuzifuata Hospitali Kuu ya Mnazimmoja.

Amesema baadhi ya wananchi wanashindwa kufuata huduma ya kufanyiwa uchunguzi  mjini kutokana na hali zao kimaisha na hatua ya kuwapelekea wataalamu hao vijijini ni hatua ya kupongezwa.

Sheha wa Shehia ya Jambiani Kikadini Hassan Haji Maringo aliupongeza uamuzi huo ulioanzishwa na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein  na aliwataka wananchi  kuzitumia fursa kama hizo kila zinapotokea.

Baadhi ya wananchi walifanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu wameshauri  wataalamu hao kufika mara kwa  mara vijijini  ili wanapokuwa na matatizo yaweze kujulikana mapema.

Daktari dhamana wa Wilaya ya Kusini Maulid Abdalla Mohd amesema madaktari bingwa wa Kichina wanaofanyakazi Hospitali Kuu ya Mnazimmoja wakishirikiana na wataalamu wazalendo wamefanikiwa kuwafanyia uchunguzi wananchi kutoka vijiji mbali mbali vya Wilaya hiyo.

“Madaktari bingwa wa Kichina wakishirikiana wataalamu wazalendo kutoka Hospitali ya Mnazi Mmoja wamekuja kutoa huduma mbali mbali za Afya kwa wananchi wa vijijini bila ya malipo dawa zipo na huduma nyengine zinapatikana”, alifahamisha Daktari huyo.

Amesema kutokana na kujitokeza wananchi wengi kinyume na walivyofikiria awali wameamua kuandaa siku nyengine kutoa huduma kama hiyo katika kijiji chengine cha Wilaya ya kusini.

Aidha ameeleza kuwa huu ni mpango maalum wa Wizara ya Afya ambao ametoa  Mhe Rais wa kutoa huduma vijijini kila baada ya miezi mitatu kwa lengo la kuboresha huduma za afya vijijini na kujua matatizo yao.

Maradhi yaliyofanyiwa uchunguzi  na kupatiwa matibabu ni Moyo, Sukari, Presha, Masikio, Macho, Matibabu ya Watoto na Kinamama,matatizo ya Ngozi na Kifua pamoja na matatizo ya Mkojo.
MWISHO
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.