Habari za Punde

Maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika Kufanyika Kesho.

Meneja wa Takwimu za Pato la Taifa Daniel Masolwa (kushoto) 
kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu akizungumza na waandishi wa 
habari (hawapo pichani) wakati akielezea maadhimisho ya Siku ya 
Takwimu Afrika yatakayofanyika Novemba 18 katika ukumbi wa 
Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam, kulia ni Afisa Habari 
wa Idara ya Habari Beatrice Lyimo.Picha na Eliphace Marwa -Maelezo
Na: Veronica Kazimoto,
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango anatarajiwa kuwa mgeni Rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika yatakayofanyika kesho jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa mkabala na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Meneja wa Takwimu za Pato la Taifa Bw. Daniel Masolwa kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu amesema dhumuni la kuadhimisha siku hiyo ni kuongeza uelewa mpana kwa watumiaji wote  wa Takwimu Afrika kuhusu umuhimu wa takwimu katika kupanga mipango ya maendeleo katika sekta zote za kijamii na kiuchumi. 

“Siku hii huadhimishwa ili kutoa fursa ya kutathmini na kufuatilia malengo yaliyofikiwa katika Mipango ya Maendeleo ya ndani na nje ya Nchi”, amesema Masolwa.  

Masolwa ameeleza kuwa kaulimbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni “Kuimarisha Takwimu za Kiuchumi kwa Mtangamano wa Kikanda, Mabadiliko ya Miundo na Maendeleo Endelevu".

Amefafanua kuwa kaulimbiu ya mwaka huu inalenga kuwaelekeza wadau mbalimbali wa takwimu kujikita katika kujadili na kuweka mikakati inayoendana na umuhimu wa kuboresha na kuimarisha takwimu za uchumi na zenye ubora kwa Utangamano wa Kikanda Barani Afrika.  

Maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika hufanyika kila mwaka tarehe 18 Novemba ambapo huandaliwa na kaulimbiu mbalimbali zinazohusiana na umuhimu wa takwimu katika kupanga maendeleo na kutunga sera katika Bara la Afrika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.