Habari za Punde

Umoja wa Mataifa waishukuru Serikali ya Tanzania

 Mwakilishi wa Tanzania  katika Umoja wa Mataifa  Balozi Tuvako  Manongi akizungumza wakati wa uwasilishwaji wa  Ripoti ya  utendaji  kazi wa IRMCT ambapo  alimshukuru kwa namna ya pekee Msajili wa  IRMCT Bw. John Hopkins kwa uongozi wake na  ushirikiano  ambao ameonyesha katika ujenzi wa majengo mapya huko Lakilaki  lakini pia  katika kusimamia  kipindi cha mpito na makabidhiano kutoka  ICTR kwenda  IRMCT.
Rais wa IRMCT, Bw. Theodor Meron akiwasilisha mbele ya  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, hapo  siku ya jumatano, Ripoti ya  utendaji kazi wa  Matawi ya  Mahakama za Kimataifa za  Kesi za Masalia zinachokua nafasi ya  iliyokuwa  Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya  Rwanda ( ICTR) na  Mauaji ya halaiki yaliyotokea  katika iliyokuwa  Yugoslavia ya zamani ( ICTY. Bw. Meron  alitumia pia fursa hiyo  kuishukuru  Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wa hali na  mali  katika  ujenzi wa majengo  yanayochokua nafasi ya  ICTR majengo hayo  yamejengwa katika eneo  la Lakilaki Mkoani Arusha.




Na  Mwandishi Maalum, New York

Umoja wa Mataifa   kwa  mara nyingine tena, umeishukuru Serikali ya  Tanzania kwa kusaidia kwa hali  na mali ujenzi na hatimaye kuelekea  ukamilishwaji  wa Majengo  mapya ambayo yatatumika kwa shughuli za iliyokuwa  Mahakama ya Kimataifa   ya  Mauaji ya Kimbari  ya Rwanda ( ICTR) ambayo ilihitimisha majukumu yake   mwaka jana.

Shukrani hizo zimetolewa siku ya  jumatano  na  Bw.Theodor  Meron,  ambaye ni Rais wa  Mahakama  za  Kimataifa za Kesi za Masalia na Utunzaji wa kumbukumbu na  nyaraka zote muhimu za zilizokuwa   Mahakama za  Kimataifa zilizoshughulikia mauaji ya halaiki  yaliyotokea  Rwanda na   Yugoslavia ya zamani ( IRMCT).
 Bw. Theodor Meron alikuwa akiwasilisha  Ripoti yake ya Nne kuhusu IRMCT mbele ya  Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa . Ripoti ambayo imeanisha maendeleo ya kipindi cha mpito  kutoka ICTR na ICTY kwenda IRMCT kazi ambayo amesema  inakwenda vizuri ingawa kumekuwapo na changamoto  kadhaa.

“Wakati  ninapowasilisha  ripoti  hii, nichukue fursa hii  kutoa shukrani zangu  za dhati kabisa kwa mchango mkubwa na ushirikiano  ambao  tumeupata kutoka  serikali ya  Tanzania, takribani wiki  tatu zijazo majengo hayo yatazinduliwa rasmi baada ya kuwa yamekamilika”. Akasema Bw. Meroe

Baadhi ya  changamoto hizo kwa upande wa iliyokuwa  ICTR  ni  pamoja na  kutokamatwa hadi sasa kwa watuhumiwa  watatu  ambao inaelezwa wapo  mafichoni.
Ni pili ni  mahali pa kuwapeleka watu ambao ama wamekwisha maliza kutumikia vifungo vyao  na kuachiwa huru. Watu hao wamekosa nchi ya  kuwapokea na  hadi sasa bado wanaendelea kuishi  nchini  Tanzania.

Na kwa sababu hiyo, Rais wa  IRMCT ametoa wito kwa  Jumuiya ya Kimataifa kutoa ushirikiano wa kuwachukua watu hao ambao  hawana  mahali pa kwenda na  kwa wale walioko mafichoni nchi ambazo wamejificha watoe ushirikiano  kwa kuwafichua  na kuwakamata ili hatimaye sheria iweze kuchukua mkondo wake

Kwa  upande wake,  Tanzania  kupitia Mwakilishi wake katika Umoja wa Mataifa,  Balozi Tuvako Manongi, amesema  Tanzania  inakaribisha kuhitimishwa kwa ujenzi kwa  ujenzi wa makazo mapya ya iliyokuwa  ICTR katika eneo la Lakilaki ndani ya wakati na kwa bajeti iliyopangwa.
“Kwa namna ya  pekee tunampongeza Msajili wa  Mahakama, Bw. John Hopkins kwa uongozi wake na ushirikiano wake ambao  umewezesha kukamilisha hatua hii muhimu sana”. Akasisiza  Balozi.

Aidha  kukamilika kwa majengo hayo  na  ambayo  yapo katika ardhi ya  Tanzania ni heshima na  fahari kubwa na ya kipekee  kwa Tanzania  na  wananchi wake    kutokana na  jukumu kubwa iliyobeba ya kuwa mwenyeji  wa  Mahakama ya Kimataifa ya mauaji  ya Kimbari ya  Rwanda  kwa niaba ya  Jumuiya ya Kimataifa.

Balozi Manongi pia amepongeza uratibu  uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa kupitia Ofisi ya Mshauri wa  Sheria, Ofisi  ya  Msajili na  the  Hegue ya kuhakikisha kwamba, pamekuwapo na utaratibu mzuri  wa kurithishana kutoka  ICTR kwenda IRMCT. Na kwamba kazi hiyo haikuwa nyepesi.

Akizungumzia kuhusu kazi za IRMCT, Balozi  amesema,  Tanzania  ingependa  kuona  Taasisi za  Kitaifa  zinawezeshwa  ili ziweze kushughulikia  kwa  ukamilifu, haki na usawa  na  kwa  kuzingatia  sheria za  kimataifa kesi zinazopelekwa kwenye  Taasisi hizo za kitaifa.

Aidha akasema uzoefu ambao umepatikana  kutokana na  kazi kubwa   iliyofanywa na  ICTR pamoja na ile ya  ICTY  ni vema ukatumika  kama mfano katika   Mahakama  nyingine za  Kimataifa.

Kwa upande wa mashahidi, Tanzania imesisita  umuhimu wa mashahidi kulindwa na kuhakikishiwa usalama wao dhidi ya  vitisho mara baada ya kutoa ushahidi.

Kuhusu  watu walioachiwa huru baada ya kukamilisha  vifungo  vyao na bado wapo nchini Tanzania. Tanzania imeungana na  wazungumzaji wengine katika mkutano huo wa kutaka pawepo na  majadiliano ya kina ya kuangalia namna  gani ya  kuwasaidia watu hao.

Vile Tanzania imetoa wito kwa  nchi zile ambazo  zinahisiwa  kwamba zinawahifadhi  watuhumiwa  watatu ambao wapo mafichoni na wanatakiwa kufikishwa katika vyombo  vya sheria kutoa ushirikiano ili  hatimaye haki itendeke.

Watuhumiwa ambao wametajwa kuwa walihusika kwa  namna  moja ama nyingine  katika mauaji ya  Kimbari nchini Rwanda na wapo  mafichoni hadi sasa ni Augustin Bizimana, Felicien Kabuga na Proitas Mpiranya.

Kwa  mujibu wa  Ripoti  iliyowasilishwa mbele ya  Baraza Kuu la 
Umoja wa Mataifa, watuhumiwa hao watakapopatikana  kesi zao  zitafanyika katika  Mahakama hiyo  mpya  nchini Tanzania.

Uamuzi kwa kuwa na  matawi   ya   IRMCT  huko  Arusha na the  Hague, Uholanzi unatokana na   maamuzi ya  Baraza la Usalama la  Umoja wa Mataifa  kupitia azimio nambari 1966 la  mwaka  2010.

Kupitia  Azimio hilo  Baraza la  Usalama  liliamua   kwamba, baada ya kumalizika rasmi kwa   ICTR ( 2015) na  ICTY ( 2017) Tanzania ambayo ndiyo ilikuwa mwenyeji wa  ICTR itapewa jukumuu la  kuhifadhi kumbukumbu na nyaraka zote muhimu za iliyokuwa ICTR ikiwa ni pamoja na kumalizia  kesi zitakazokuwa zimebaki. Huku  the Hague ikiwa na dhamana hiyo hiyo kwa kazi zilizokuwa za  iliyokuwa  ICTY.

Mahakama za Kimataifa  za Rwanda na  Yugoslavia ambazo zimefanya kazi kubwa ya kuwafikisha mbele ya sheria watuhumiwa karibu  wote waliohusika na  matukio ya  kutisha ya ukiukwaji wa haki za binadamu ziliazishwa mwaka  1990  na  Umoja wa Mataifa.


















No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.