Habari za Punde

Jee Dirisha la Usajili Bongo Litafungwa kwa Staili Gani?

DIRISHA dogo la usajili linatarajiwa kufungwa leo Alhamis saa 6:00 usikuhuku tayari baadhi ya timu zikiwa zimeshakamilisha usajili wao wakati ndani ya Simba wengine wamejuwa hatima yao ya kuondoka na bado wanaweza kufanya usajili wa mwisho wa kushitukiza.


Kwasasa kipa namba moja ni Mghana, Daniel Agyei aliyetokea timu ya Medeama na kuondoka kwa Vincent Angban raia wa Ivory Coast kunamaanisha kuwa Agyei atasaidiwa na makipa wawili wazawa Manyika Peter Jr na Denis Richard.
Simba imemalizana na nyota watatu ambao wamewapa mikataba, Agyei, James Kotei aliyepewa mkataba wa mwaka mmoja na Pastory Athanas kutoka Stand United wote wamepewa mkataba wa mwaka mmoja kila mmoja.

Mbali na hao pia wapo mbioni kumnasa Juma Luizio kutoka Zesco United ya Zambia kwa mkopo ili kuimarisha safu hiyo ambayo mzunguko wa kwanza haikuwa na makali ya kutosha. Taarifa zinasema straika huyo ameshatua Bongo usiku wa kuamkia leo.

Kocha wa Simba, Joseph Omog alipendekeza wasajiliwe wachezaji katika nafasi ya kipa na mshambuliaji ingawa sasa imeonekana kuboresha pia safu ya kiungo na beki wa kulia ambapo jana ilidaiwa kuwa Wekundu hao walikwenda kumalizana na Mtibwa Sugar kwa ajili ya usajili wa Ally Shomary ingawa dili hilo bado halijakamilika.

Omog alihitaji kipa mwingine baada ya Angban kufanya vibaya mechi mbili za mwisho za mzunguko wa kwanza wa ligi alipofungwa na African Lyon pamoja na Prisons.


Hivi sasa Simba itawatema nyota wake watatu wa kigeni Angban, Fredrick Blagnon na Musa Ndusha anayedaiwa kupelekwa kwa mkopo Uarabuni huku beki Mganda Juuko Murshid ambaye mkataba wake unamalizika mwezi ujao hajajiunga na timu hadi sasa.

Kotei ambaye ana uwezo wa kucheza kama kiungo mshambuliaji na mkabaji atakuwa na kazi ya kugombania namba ili awe kwenye kikosi cha kwanza cha Omog pamoja na nyota wengine kama nahodha Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Mohamed Ibrahim, Said Ndemla na Mwinyi Kazimoto wote wana uwezo mkubwa.

Endapo Simba watafanikiwa kunasa saini ya Shomary basi atasaidiana na Janvier Bokungu pamoja na Hamad Juma ambaye tangu adondoke bafuni hajapata nafasi ya kucheza mara kwa mara. 

Usajili wa Shomary umekuja baada ya Salum Kimenya kugomea ofa ndogo waliyotaka kumpa. Simba walikuwa tayari kumpa Sh 30 milioni huku yeye akitaka Sh 40 milioni.

Simba ambayo ilimaliza mzunguko wa kwanza ikiongoza kwa pointi 35 inajiandaa kucheza ugenini dhidi ya Ndanda FC mechi itakayopigwa Jumapili, Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.