Habari za Punde

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                                                                                                            3.12.2016
---
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kubadilisha mitaala katika Skuli za Sekondari sambamba na kuimarisha vyuo vya amali ili somo la ujasiriamali liweze kuchukua nafasi kubwa katika mitaala na kuhakikisha wanafunzi wanaomaliza elimu ya Sekondari wanafaulu vyema ujasiriamali.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa Kongamano la siku mbili na maonyesho ya Wajasiriamali linalofanyika katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi, Kikwajuni mjini Unguja.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kwa utaratibu huo wanafunzi watapata eimu itakayowasaidia kujiajiri wenyewe na kutumia fursa hiyo kuiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kuhakikisha kuwa inaongeza kasi katika kulishughulikia suala hilo.

Dk. Shein aliwakumbusha vijana kuwa elimu waliyoipata katika Vyuo Vikuu na Taasisi mbali mbali zinazotoa mafunzo ya kazi na ufundi ni mtaji muhimu katika kuendeleza shughuli za ujasiriamali.

Hivyo, aliwataka wasijenge dhana kuwa ujasiriamali ni kufanya biashara ndogo ndogo za bidhaa zinazoonekana katika masoko lakini wajifunze kutokana na uzoefu wa nchi mbali mbali hasa India ambapo vijana wengi waliosoma wamekuwa wakijiajiri wenyewe baada ya kumaliza masomo yao.

Alisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua umuhimu wa kuwaendeleza wajasiriamali katika kuyafikia malengo ya kupambana na umasikini wa kipato na kupunguza tatizo la ajira hasa miongoni mwa wanawake na vijana.

Alisema kuwa kwa lengo la kuongeza ufanisi katika kipindi hiki cha pili cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba  ameamua kuyaweka makundi ya vijana na wanawake katika wizara moja na masuala ya uwezeshaji ili shughuli za uwezeshaji kupitia ujasiriamali ziweze kukuza kipato cha wananchi na kuondoa umasikini.

Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza mafanikio ya Mfuko wa Uwezeshaji ambao katika kipindi cha miaka miwili na miezi minne tangu mfuko huo ulipoanza kazi zake ambapo jumla ya mikopo 998 yenye jumla ya Tsh. Bilioni 1.6 imeshatolewa Unguja na Pemba ambapo tayari marejesho ya asilimia 96 yameshafanyika.

Alisema kuwa jambo la kufurahisha zaidi ni kuwa taarifa zinazonesha kwamba asilimia 67 ya watu waliopewa mikopo ya Mfuko huo ni vijana wenywe umri kati ya miaka 18 hadi 35 huku akiwataka wanasiasa kutowadanganya vijana kuhusiana suala la ajira kwani vijana hivi sasa hawadanganyiki.

Alisema kuwa lengo la viongozi hao wa kisiasa ni kutaka kuwagombanisha vijana na Serikali yao na kuwataka viongozi hao kusema ukweli katika suala zima la ajira.

Dk. Shein aliwahakikishia wananchi na wajasiriamali kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto na Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko imejipanga ili kuona kwamba wajasiriamali wanafikia malengo waliyoyakusudia kwa kuwatafutia masoko.

Dk. Shein aliwaeleza wajasiriamali hao kuwa watu matajiri na maarufu duniani kote ikiwemo Zanzibar ni wajasiriamali hivyo, aliwahimiza kuendelea kukuza vipaji na elimu walizonazo wakiamini kwamba nao wanaweza kufanikiwa kama walivyofanikiwa wao.

Pia, Dk. Shein alisema kuwa Serikali itaendelea kuzitatua changamoto zinazowakabili wakulima na wajasiriamali katika suala zima la kuongeza ubora wa bidhaa na mazao yanayolimwa.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Wizara ya Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto kwa mafanikio yaliopatikana katika kituo cha Kuleta na Kukuza Wajasiriamali kilichopo Mbweni kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo na kusisitiza haja ya kuharakishwa ujenzi wa kituo kama hicho huko Pemba.

Mapema Dk. Shein aliangalia maonyesho ya Wajasiriamali ambapo alipata fursa ya kukagua bidhaa zao mbali mbali wanazozizalisha. Pia katika hafla hiyo alitoa vyeti maalum kwa wachangiaji wa kongamano hilo.

Nae Waziri wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Maudline Castico alisema kuwa kongamano hilo ni la kwanza la aina yake kufanyika hapa nchini na kueleza kuwa mchango wa Sekta binafsi kupitia wajasiriamali wakubwa na wadogo ni muhimu sana ili kufikia lengo la Zanzibar kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kati ifikapo 2020.

Alisema kuwa kongamano hilo linatarajiwa kuhamasisha kuwaelimisha wajasiriamali ili kuendeleza shughuli zao kwa ufanisi zaidi.

Wajasiriamali katika risala yao iliyosomwa na Aziza Saleh, walieleza kuwa wanafahamu kwamba wakati huu wa mabadiliko ya uchumi duniani kote ni wajasiriamali watakaosaidia kuzalisha ajira kupitia ujasiriamali, ili kusaidia Serikali kukuza uchumi wake.

Walieleza kuwa wajasiriamali wabunifu na wavumbuzi wanauwezo wa kuanzisha mambo tofauti kulingana na mahitaji ya soko yaliopo ili kuweza kuchangia pato la Taifa na ukuaji wa uchumi hapa nchini iwapo tu wataelekezwa na kupatiwa utaalamu unaohitajika.

Nao Wawakilishi wa Shirika la kujitolea la Kimataifa (VSO), pamoja na Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) kwa nyakati tofauti waliahidi kuendelea kushirikiana na  Serikali katika kuwasaidia wajasiriamali ili kufikia lengo lililokusudiwa.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.