Habari za Punde

Ufungaji wa Mafunzo ya Maonesho ya Taaluma ya Sayansi

Na Abdi Shamnah
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema itaendelea kuchukua hatua kuhakikisha maeneo yote ya Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (Karume Institute of Science Technology - KIST) yanalindwa, ili kuiwezesha kufanikisha vyema malengo yake.

Imesema pia inalengo  kuongeza bajeti ya taasisi hiyo ili kuimarisha miundo mbinu mbali mbali iliopo, ikiwemo majengo ya wanafunzi.
Kauli hiyo imetolewa an Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein katika viwanja vya KIST, katika kilele cha maadhimisho ya miaka 50, tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo  1966.
Akizungumza kwa niaba ya Dk. Shein, Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, Salama Aboud Talib alisema tayari Wizara yake kwa kushirikiana an Wizara ya Elimu imelipatia ufumbuzi tatizo la ukosefu wa Hati miliki ya taasisi hiyo, ilioyokosekana kwa kipindi chote hicho.

‘‘Rais aliagiza Wizara yangu tukae pamoja na wizara ya Elimu kulipatia ufuimbuzi tatizo hili, tayari tumeshakaa na tumeshakamilisha taaratibu zote, tuna matarajio itapatikana mapema mwezi ujao’’, alisema.

Aidha alisema hatua ya Rais Shein kutia saini sheria ya mafuta na gesi, namba 6 ya 2009 , ina mnasaba mkubwa na uimarishaji wa Taasisi hiyo kwa kuzingatia mahitaji makubwa ya serikali katika upatikanaji wa wataalamu wa ndani katika usimamizi na uendeshaji wa nishati.

Alitoa rai kwa uongozi wa Taasisi hiyo kujipanga na kufanikisha azma iliyoweka ya kuanzisha kozi ya stashahada kwa ajili ya fani ya mafuta na gesi asilia, sambamba na kozi ya uhandisi wa ndege.

‘‘Hii nayo itakwenda sambamba na juhudi zinazofanywa na Serikali  za kuimarisha huduma za uwanja wake wa Ndege wa Abeid Amani Karume’’, alisema.

Katika hatua nyengine Waziri Salama alitoa wioi kwa wanafunzi kote nchini kujikita na kupenda kusoma masomo ya Sayansi, kwa kigezo kuwa kuna mahitaji makubwa katika fani mbali mbali, ikiwemo ile ya ufundi.

Aliupongeza uongozi wa tyaasisi hiyo kwa kufikia malengo ya kuanzishwa kwake, mara tu baada ya Mapinduzi ya 1964.

Nae, Naibu waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mmanga Mjengo Mjawiri aliushauri uongozi wa KIST kuanzisha masomo ya fani ya Industrial Engineering, kwa kigezo kuwa Taifa linalenga kufanya mapinduzi makubwa kuelekea uanzishaji wa viwanda.

Mapema, akisoma risala ya Wahitimu wastaafu, mwanazuoni Talha Masoud ,alisema pamoja na taasisi hiyo kupata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka 50, bado wahitimu wake wanakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo ukosefu wa ajira, hususan katika taasisi za serikali, huku taasisi binafsi nazo zikielezwa kuajiri wahitimu wachache.

Aliiomba Serikali kuweka kipaumbele kwa makampuni ya ujenzi ya wazalendo katika miradi mbali mbali, ikiwa njia mojawapo ya kutoa fursa za ajira kwa vijana.

Aidha alikososa utaratibu wa kutokuwepo uwiano wa kimaslahi kati ya watendaji wa taasisi hiyo na taasisi nyingine, ikiwemo kada za udaktari na wanasheria.

Aliiomba Serikali iondokane na upendeleo, na kuzichukulia kada hizo kwa mizania iliyo sawa, kwa kigezo kuwa zote ni muhimu katika mustakbali wa maendeleo ya Taifa.

Aliongeza kwa kusema kuwa pale chanagamoto hiyo itakapopatiwa ufumbuzi, ni wazi kuwa wanafunzi wengi watapenda kusoma masomo ya hayo ya ufundi.


Pamoja na kutembelea maonyesho mbali mbali katika sherehe hizo, Waziri Salama alipata fursa ya kukabidhi vyeti kwa wakufunzi na wahitimu waliodumu na utumishi wa kipindi kirefu  ndani ya taasisi hiyo tangu ilipoanzishwa 1966. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.