Habari za Punde

Zlsc Pemba: Kuwadhalilisha walemavu ni kuvunja sheria

Na Salmin Juma ,Pemba

Jamii nchini imetakiwa kuacha kuwadhalilisha watu wenye ulemavu hasa wa akili ambapo imeelezwa kua, kushafanya hivyo ni kinyume cha sheria na kunaweza kupelekea mtu kuingia hatini.

Vitendo vya udhalilishaji kwa watu wanaoishi na ulemavu vinaoneka kutuwama katika jamii ikiwa ni pamoja na kuwapa ujauzito, kuwalawiti,kuwanyima fursa za elimu na mengineyo.


Hayo yamebainishwa leo na mratibu wa kituo cha huduma za sheria Zanzibar Legal Service Centre (ZLSC) afisi ya Pemba Bi Fatma Khamis Hemed alipokua akiwasilisha mada ya SHERIA YA WATU WENYE ULEMAVU katika mafunzo maalum yaliyoandaliwa na kituo hicho kwaajili ya kuelewa haki za binaadamu kwa wazazi na walezi wanaoishi na watu wenye ulemavu huko chakechake Pemba.

Amesema mtu mwenye ulemavu ni binaadamu wa kawaida na anastahiki kuheshimiwa na kutunzwa ili kua katika mazingira mazuri kama ilivyo kwa watu wengine.
Akionyesha hali ilivyozidi kua mbaya katika jamii Bi Fatma amesema imeshawahi kutokea katika maeneo ya Wawi mkoa wa kasini Pemba mtoto mwenye ulemavu kulawitiwa na kesi yake ilimalizwa kienyeji.

Bi Fatma amewataka wazazi, walezi na wale wote wanaoishi na watu wenye ulemavu kuzingatia haki zao za msingi zilizoainishwa kisheria ambapo amesema sheria nambari 09/2006 imetoa haki kwa watu hao ya kushiriki katika kupiga kura, haki ya kupatiwa elimu,haki ya kushiriki katika michezo na burudani,haki ya kufanya kazi,haki ya kupatia huduma bora ya afya na nyenginezo.

"wakiwezeshwa wanaweza tena wanaweza kufanya vitu vizuri na vikapendeza sana,hivyo si vyema kuwadhihaki na kuwaona kua si lolote" alisema Bi Fatma.

Aidha amesema, sehemu ya nne ya sheria hiyo inafahamisha kua, kumkejeli mtu mwenye ulemavu kwa ishara au maneno na ikibainika kua ni kweli mkosaji atatakiwa kulipa faini ya shilingi milioni tano (Tsh 5,000,000) au kifungo cha miaka isiyopungua mitano au vyote kwa pamoja.

Pia amesema kwa wazazi, atakaebainika kumficha mtoto mwenye ulemavu au kumbagua na ikibainika ni kweli atalazimika kutoa faini ya shilingi elfu hamsini(Tsh 50,000 ) au jela miezi isiyopungua mitano au vyote kwa pamoja.

Hivyo amewataka wazazi, walezi na wananchi kwa ujumla kuzingatia haki za msingi za watu wenye ulemavu ambapo amesema kua hata mwanaadamu wa kawaida anaejiona mzima muda wowote anaweza kua mlemavu, hivyo haipaswi kuwadhihaki na kuwadhalilisha kutokana na hali zao.

Kwa upande mwengine amesema sheria hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo katika majengo mbalimbali ya serikali na yakibinafsi, hakuna miundombinu rafiki ya kuwawezesha watu hao kufikia huduma kwa wepesi kama ilivyoelezwa katika sheria hiyo.

Mafunzo hayo yanalengo la kutoa taaluma kwa wanaoishi na watu wenye ulemavu pamoja na wananchi kwa ujumla, kuacha vitendo viovu dhidi ya watu wenye ulemavu kwani nao ni binaadamu wa kawaida na wanastakihi kuishi kwa amani na kuheshimiwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.