Na Haji Nassor, Pemba
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali
wilaya ya Wete Pemba, imekanusha taarifa zilizosambaa mitandandaoni na baadhi
ya watu kuwa, dakhalia za skuli za Chasasa na Utaani, zimefungwa, kufuatia kuwepo kwa tendo la ulawiti
skulini hapo.
Wizara hiyo imesema, wanafunzi kwenye skuli hizo wapo kama kawaida wanaedelea na masomo yao na wala hakuna wanafunzi waliorejeshwa majumbani, kwa kuwepo dhana ya ulawiti kwenye skuli hizo.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu Afisa elimu na mafunzo ya amali
wilayani humo, Khamis Said Hamad, alisema taarirfa hizo hazina ukweli wowote.
Alisema
hakuna dakhalia yoyote iliofungwa wilayani humo, na taarifa zilizosambaazwa
juzi zinalengo la kupotosha umma jambo ambalo, sio jema.
“Wanafunzi
waliopo dakhalia wanaendelea na kuishi hapo bila ya hofu na wanaendelea vyema
na masomo yao na wala sisi hatujapokea taarifa za kuwepo kwa ulawiti wa kutisha
kama inavyoelezwa’’,alifafanua.
Hata
hivyo Afisa elimu huyo, amewataka wananchi kuacha kushabikia za kuziamini
haraka, taarifa zinazorushwa kwenye mitandao ya kijamii.
Katika
hatua nyengine alikiri kuwa, mwaka juzi alikuwepo mwanafunzi muathirika wa
tendo hilo na alipokelewa kwenye skuli hizo akitokea Mkoani, ingawa baadae
aliondolewa.
“Ni
kweli aliwahi kuja mwanafunzi kusoma hapa alikuwa anafanya au anafanyiwa tendo
la ulawiti, lakini tulipombana aliondolewa na sasa skuli hizo hali iko
shuwari’’, alibainisha.
Baadhi
ya wazazi na walezi wa mji Wete kisiwani Pemba, wameziomba taasisi husika
kufanya utafiti wa kina, juu ya jambo hilo, kutokana kuwepo kwa tuhuma za muda
mrefu.
“Hili
jambo kwenye skuli zetu za Chasasa na Utaani limeshakuwa la muda mrefu sasa,
lazima serikali itafute njia ya kutoa taarifa rasmi, badala ya taarifa za
kudokoa dokoa kama ilivyo sasa’’,alishauri
Khamis Juma.
Nae
Asha Makame Muhunzi, alisema taarifa za kuwepo kwa matendo ya ulawiti ndani ya
wilaya ya Wete, halina shaka, ni vyema sasa hatua zikachukuliwa.
Nae
Afisa huduma za wanafunzi kutoka wizara ya elimu kisiwani Pemba, Said Massoud
Othaman alisema sio wilaya ya Wete tu lakini hakuna dakhalia yoyote iliofungwa
kisiwani Pemba kwa tendo hilo.
Alieleza
kuwa, ijapokuwa kuna taarifa za ulawiti kwenye baadhi ya skuli, lakini taarifa
kuwa skuli za sekondari za Chasasa na Utaani zimefungwa kwa tatizo hilo, sio
kweli.
“Tendo
la ulawiti sasa limeenea kwenye vyuo vya kur-an, skulini, majumbani na maeneo
mengine , hivyo ni jukumu letu wazazi kushirikiana ili kuliondoa’’,alifafanua.
Hata
hivyo alisema wamekuwa wakipokea malalamiko juu ya shutuma za tendo hilo,
ingawa hawajabaini kuwepo kwa udhalilishaji kama inavyoelezwa kwenye skuli hizo.
Afisa
Ustawi wa Jamii wilaya ya Wete Haroub Suleiman Hemed, alisema, kitakwimu
matendo hayo hayako juu wilayani humo, ingawa kimazungumzo hali huwa inatisha.
“Jamii
tushirikiane katika kupambana na udhalilishaji wa aina yote, maana kama kuna
tetesi basi ujuwe jambo lipo au linanyemelea kwenye mazingira
yetu’’,alifafanua.
Mwanafunzi
mmoja ambae hakupenda jina lake lichapishwe alisema kwa sasa hawajamgundua
mwanafunzi mwenzao anaendesha vitendo hivyo, hasa baada ya aliekuwepo
kuondolewa.
Juzi
katika baadhi ya mitando ya kijamii na minong’ono ya watu kwenye mikusanyiko,
kuliwa na taarifa ya skuli za sekondari na Chasasa ambazo zina dakhalia
kufungwa, kutokana ongezeko la tendo la ulawiti kwa wanafunzi.
No comments:
Post a Comment