Habari za Punde

WAZIRI MKUU ASHIRIKI KAMPENI YA KITAIFA YA MAZOEZI YA WIZARA YA AFYA. · Aungana na wakazi Dar kufanya mazoezi

 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kuongoza matembezi ya kuhamasisha ufanyaji wa mazoezi ili kujikinga na magonjwa yasiyo ambukiza Mei 04, 2024. Matembezi hayo ya Kilomita 10 yalianzia Coco Beach jijini Dar Es Salaam hadi Mzunguko wa Hospitali ya Agha Khan na kurudi Coco Beach. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameshiriki mazoezi ya pamoja ya kampeni ya kitaifa inayoratibiwa na Wizara ya Afya ya kuhamasisha ufanyaji wa mazoezi kwa watanzania ili kujiepusha na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Mheshimiwa Majaliwa amesema hatua hiyo pia ni kuunga mkono wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kufanya mazoezi ili kujikinga na magonjwa hayo.

Ameyasema hayo leo (Jumamosi Mei 4, 2024) aliposhiriki katika kampeni ya ufanyaji mazoezi pamoja na matembezi ya kilomita 10 yaliyoanzia katika fukwe za Coco kupitia daraja la Tanzanite hadi Ocean Road jijini Dar es Salaam.

"Mnakumbuka programu hii iliyoanzishwa na Rais wetu Dkt. samia Suluhu Hassan na yeye mwenyewe kushiriki na kuwahamasisha watanzania kushiriki mazoezi mbalimbali, katika kipindi cha miaka mitatu ya Dkt. Samia moja ya mambo ya kujivunia ni mafanikio katika sekta ya michezo."

Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Viongozi wa  Manispaa ya Kinondoni kufanya maboresho zaidi katika eneo la fukwe za Coco ili liwe safi na livutie watu wa rika mbalimbali.

"Nawapongeza jeshi la polisi kwa kazi nzuri ulinzi katika eneo hili, Nitoe wito kwenu kuendelea kuimarisha ulinzi ili eneo hili liwe salama kwa watu wa rika na jinsia zote."

Awali, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amemshukuru Waziri Mkuu kwa kukubali kushiriki katika mazoezi hayo huku akitoa taarifa ya ongezeko la magonjwa 10 yasiyo ya kuambukiza jambo lililofanya Wizara hiyo kuleta ombi la kuanzisha utaratibu wa mazoezi kila jumamosi.

"Mwaka 2022 kati ya magonjwa 10 yanayowasumbua watanzania moja lililojitokeza ni shinikizo la juu la damu bajeti ya mwaka 2022/2023 likaongezeka na kisukari katika magonjwa 10 yanayowasumbua watanzania. Wajibu wa Wizara ya Afya ni kuwakinga Watanzania wasipate magonjwa."

Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amesema kama Mkoa watajipanga kuhakikisha utaratibu huo wa mazoezi utakuwa endelevu kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na wadau mbalimbali wa michezo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.