NA
HAJI NASSOR, PEMBA
MADIWANI
na wananchi wa wadi sita za mkoa wa kaskazini Pemba, wamesema kazi iliofanya na
Mtandao wa Asasi za Kiraia Pemba, PACSO, ndio imaewaamsha na kutambua umuhimu
wa kufuatilia kwa karibu, matumizi ya fedha za umma kwenye miradi mbali mbali
ikiwemo ya barabara.
Walisema hawakuwa wakifikiria kuwa
wanawajibu na haki ya kujua gharama za ujenzi wa miundombinu hiyo, hata
inayopita kwenye maeneo yao, wakidhani kuwa kazi hiyo inawapasa watendaji wa
taasisi za fedha pekee.
Wakizungumza kwenye kongamano lililofanyika
Kituo cha elimu mbadala na watu wazima Wingwi wilaya ya Micheweni la kujadili
ripoti ya awali ya kufuatilia matumizi ya fedha za umma, walisema utafiti huo
umewapa taaluma.
Walisema wakati wanapitiwa kuhojiwa na
watu waliondaliwa na PACSO, juu ya ikiwa wanafahamu lolote gharama ya ujenzi wa
barabara na ubora wake, hawakuwa wakijua kuwa wana haki hiyo.
Farida Ali Saleh wa Wete, alisema wapo
wananchi baadhi yao, walioshindwa kutaja gharama za ujenzi wa barabara zao za
ndani, kwa vile walishazoea kuwa hayo hayawahusu.
“Utafiti uliofanya na PACSO, sasa
wengi umetuzindua kuwa, tuna haki ya kuangalia matumizi ya fedha za umma na
hata ujenzi wa barabara, hongera mtandao’’,alifafanua.
Nae Khamis Rashid, alisema wananchi
walikuwa wamekosa uwelewa wa umuhimu wa kuzingalia na kuzifuatilia fedha zinazofikishwa
kwenye maeneo yao kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Diwani wa wadi ya Jadida Wete Mwanaali
Ali Salum, alisema, hata wananchi kabla ya kupita utafiti huo, hawakuwa
wakifikiria kuwa, kuna umuhimu wakushirikishwa kwenye miradi ya barabara hasa
za ndani.
“Utafiti huu wa mradi wa kufuatilia
rasilimali za umma (fedha), naamini sasa umewapa mwanga wananchi, kwamba na wao
ni sehemu ya kuifanikisha miradi ya ujenzi wa barabara na hata kuangalia kipaumbele
chao”,alisema.
Akifungua kongamano hilo, Mratibu wa
mradi huo Omar Ali Omar, alisema mradi huo wa miezi mitatu ambao umegharimu
shilingi milioni 68, ulikuwa na lengo la kuangalia uwelewa wa wananchi juu ya
rasilimali za umma.
Alieleza kuwa kwenye utekelezaji wa
mradi huo, wananchi 36 kutoka wadi za Chimba, Kiuyu Maziwang’ombe, Micheweni,
Mtambwe, Konde na Kiuyu Minungwini walipewa mafunzo juu ya ufuatiliaji wa fedha
hizo.
“Baada ya mafunzo hayo, tuliwapa
madodoso ya aina mbili, moja kwa ajili ya jamii na la pili kwa taasisi za fedha
kama Halmashauri, baraza la mji na hata wizara inayosimamia majenzi na
kilimo’’,alifafanua.
Hata hivyo Mratibu huyo alisema ripoti
kamili ya utafiti huo, inatarajiwa kutolewa wakati wowote, ingawa mradi huo wa
miezi mitatu, unatarajiwa kukamilika mwezi huu.
Mtandao wa Asasi za kiraia Pemba PACSO
ambao umeanzishwa mwaka 2005, tayari umeshatekeleza miradi saba iliofadhiliwa
na taasisi ya ‘the foundation for civil society’ ya Tanzania bara ukiwemo wa
utoaji wa elimu ya katiba pendekezwa.
No comments:
Post a Comment