Habari za Punde

SUZA yakabidhiwa rasmi taasisi za elimu


 Mheshimiwa Riziki Pembe Juma ambaye ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar (Kushoto) akipokea Hati za  kukabidhiwa Chuo cha Sayansi za Afya kutoka kwa Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo, Waziri wa Afya Zanzibar
 Bwana Iddi Haji Makame, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Utawala na Fedha (Kulia), akikabidhi Hati za Chuo hicho kwa Mheshimiwa Riziki Pembe Juma kwa niaba ya Mheshimiwa Dkt. Khalid Salum Mohamed, Waziri wa Fedha na Mipango.
 Mheshimiwa Riziki Pembe Juma, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar akikabidhi Hati za Taasisi zilizounganishwa na SUZA kwa Mheshimiwa Said Bakari Jecha, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar
Mheshimiwa Rashid Ali Juma (Kulia), Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo akikabidhi Hati za Taasisi ya Maendeleo ya Utalii Zanzibar (ZIToD) kwa Mheshimiwa Riziki Pembe Juma. Katikati ni Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo.



Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar tarehe 16 Januari, 2017 ilikabidhiwa rasmi Chuo cha Utawala wa Fedha Zanzibar (ZIFA), Chuo cha Sayansi za Afya (CHS), na Taasisi ya Maendeleo ya Utalii Zanzibar (ZIToD) ambazo zote kwa pamoja sasa zinakuwa chini ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).

Taasisi zilizounganishwa na  SUZA zitaendesha shughuli zake kama kawaida lakini zikiwa na majina mengine ambapo iliyokuwa ZIFA sasa itakuwa ni Skuli ya Biashara, CHS itakuwa chini ya Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba ambapo ZIToD itakuwa ni Taasisi ya Maendelo ya Utalii.
Makabidhiano hayo yalifanywa na Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo, Waziri wa Afya ambaye aliikabidhi CHS, Mheshimiwa Rashid Ali Juma, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo aliyeikabidhi ZIToD na Mheshimiwa Dkt. Khalid Salum Mohamed, Waziri wa Fedha na Mipango ambaye aliwakilishwa na Bwana Iddi Haji Makame, Kaimu Mkuu wa ZIFA.

Makabidhiano hayo yalifanyika kufuatia Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi mnamo tarehe 16 Oktoba, 2016 kuidhinisha kuunganishwa kwa taasisi hizo kwa kusaini Sheria namba 7 ya mwaka 2016 iliyopitishwa na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na kufuta Sheria zilizoanzisha taasisi hizo. Aidha Sheria hiyo iliyosainiwa na Dkt. Shein kuunganisha taasisi hizi imeifanyia marekebisho Sheria Namba 11 ya mwaka 2009 ambayo nayo iliirekebisha Sheria Namba 8 ya 1999 ambayo ndio ilianzisha Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.