Habari za Punde

‘SWIOfish’ mradi unaokuja kukuza pato kwenye uvuvi

 MKURUGENZI Idara ya Maendeleo ya Uvuvi Zanzibar Mussa Aboud Jumbe, akielezea hatua wanazopaswa kufanya wajumbe wa Kamati tendaji ya PECA, baada ya kuja kwa mradi mpya wa uhifadhi wa uvuvi SWIOfish, kwenye mkutano uliofanyika ukumbi wa Makonyo Wawi Chake chake Pemba, (Picha na Haji Nassor, Pemba).
WAJUMBE wa Kamati tendaji ya PECA, wakimsikiliza Afisa Mdhamini Wizara ya mifugo na uvuvi Pemba, Mayasa Hamad Ali, wakati akifungua mkutano wa kuwasilisha mradi wa usimamizi wa uvuvi SWIOfish, uliofanyika ukumbi wa mikutano Makonyo Chakechake Pemba, (Picha na Haji Nassor, Pemba).


-Ni baada ya Pweza, dagaa, pono kuhifadhiwa

Na mwandishi maalum, Pemba

KILA mmoja ni shahidi kuwa serikali kupitia wizara inayoshighulia uvuvi, imekuwa kiguu na njia kila uchao, kuhakikisha sekta hiyo inaongeza pato la taifa.

Elewa kuwa, pato la taifa hupanda baada ya wananchi au walengwa nao kunufaika kupitia sekta husika, kwa mfano kwenye kilimo, wastani wa pato la taifa la kila mtu limeongezeka na sasa na kufikia shilingi 1,552,000 sawa na dola za Kimarekani 939 mwaka 2014.

Hapa ni ongezeko kubwa, kutoka pato la shilingi 1,384,000 sawa na dola za Kimarekani 866 kwa mwaka 2013, ambapo taarifa zineleza kuwa sekta ya kilimo ikiwani pamoja na uvuvi, imetajwa kuchangia.


Juhudi za serikali katika kunawirisha sekta ya kilimo chini ya uvuvi, hazikuanza leo, maana kama unakumbu kumbu nzuri, basi tulianzia kwenye mradi wa MACEMP, ambapo leo tena tunao wa SWIOFish.


Washirika wetu wa maendeleo wamekuwa nasi bega kwa bega kila hatua na kila nyanja, na wakati mwengine tumekuwa tukifanikiwa kupata miradi kadhaa, tena kutokana na matumizi sahihi ya fedha.

Leo tena Mashirika mawili makubwa kutoka Marekani yanayotoa ufadhili wa miradi ya maendeleo ya GIF na IDA, yameshabisha hodi nchini kwetu kwa ujio wa ‘Mradi wa usimamizi wa uvuvi kusini Magharibi mwa bahari ya hindi’ au kwa ufupi SWIOFish.

Mradi huu, kwa hatua za awali za utekelezaji, umetia nanga kwenye nchi tatu za Mozambique, Comoro na sisi hapa Tanzania hadi visiwa vyenye samaki wengi vya Zanzibar.
SWIOFish, sasa unakuja kuendeleza mema yalioachwa au kufikiwa na mradi wa MACEMP, ambapo maradi huu sasa unalenga zaidi kukuza pato kwenye sekta ya uvui.

Lengo baada ya kuwanufaisha wavuvu, nao uchumi wa Zanzibar kupitia mradi huo ambao kwanza utatelekezwa kwa miaka sita, utapaa zaidi.

Maana aliekuwa waziri wa fedha wa Zanzibar, Omar Yussuf Mzee, anasema kimuundo, uchumi wetu umeendelea kuchangiwa zaidi na sekta ya huduma ikifuatiwa na kilimo.

Alitoa mfano kuwa, mwaka 2014, sekta ya huduma ilichangia asilimia 44.7, ikionesha kupanda kwa mchango wake kutoka asilimia 41.5 wa mwaka 2013

Hali hii imetokana na kuimarika kwa sekta ndogo za habari na Mawasiliano, fedha, taaluma, ufundi na sayansi, mchango wa sekta ya kilimo kwa mwaka 2014, umepungua na kufikia asilimia 27.9 kutoka asilimia  30.4, mwaka 2013 kutokana na kupungua kwa uzalishaji wa mpunga na mazao mengine ya chakula na kupungua kwa uzalishaji wa mazao ya biashara, hasa karafuu. 

Sasa ujio wa mradi huo uliochini ya Mratibu wake wanadada Ramla Talib Omar kwa hapa Visiwani, unakuja kuwahifadhi samaki aina tatu kuu kwa kuanzia.

Aina moja ambao mradi huu wa SWIOFish unalenga, ni wale samaki wanaoishi kwenye matumbawe, ambayo ni aina fulani ya mawe yenye bustani, ambapo tunasema ni nyumba ya samaki.

Hapo watakaohifadhiwa atakuwemo, kolekole, pono, changu, kundaji, ambapo hili halitofanywa kwa kukurupuka, bali wale waliohifadhi eneo la mkondo wa Pemba PECCA, ndio watakaoifanya kazi hii ya kuibua maeno husika.

“Kwa Pemba nyinyi wajumbe wa PECCA, ndio ambao mtakaa na wavuvi wenu, kisha mtueleze eneo gani mnadhani kuna samaki wengi wa matumbawe, ili mradi huu utie nanga’’, alisema Mratibu wa mradi huo Ramla.

Aina nyengine ambapo mradi huu wa SWIOFish unalenga kuwahifadhi, niwale  samaki aina ya pweza na ngisi, ambapo kila mmoja ni shahidi kwamba wameanza kupungua.

Hili lilielezwa vyema na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi Zanzibar Mussa Aboud Jumbe, kwamba ni maeneo machache sana yenye nyumba za pweza.

“Mnapo kwenda kuibua maeneo yenye kuishi hasa pweza, angalie sana kwenye miamba, maana pweza haishi mchangani, lazima makae vyema na wavuvi’’,alibainisha.

Kwenye mkutano wa siku moja wa kuwasilisha mradi huo, mbele ya wajumbe wa kamati tendaji wa PECCA uliofanyika Chakechake Pemba, wajumbe hao walionekana kufarajika.

Katibu wa PECCA Khamis Sharif, yeye anasema kama mradi huo utatekelezwa vyema kwa mujibu wa maandiko yalivyo, basi manufaa yataonekana.

“Mimi sasa nimeelewa nini mradi wa SWIOFish unakuja kufanya nini kwa wavuvi, kilichobakia ni kuhakikisha unatekelezwa kama ulivyo, ili manufaa yaonekane’’,aliweza wazi.

Lakini pia mradi huo mpya ambao kwa Zanzibar umeshatengewa dola za Marekani milioni 11,520,000 sawa na asilimia 40 ya fedha zilizoingizwa Tanzania, pia unangalia uhifadhi samaki ya jamii ya dagaa (samaki wanaoeleya).

Hapa anaingia dagaa mono, bakari kichwa, dagaa manyama na kaka yao kibua na kama kuna wengine wale wanaoelea, naamini baada ya miaka sita (6) ya hatua ya kwanza ya utekelezaji manufaa yataonekana.

Kama ni mtu wa kumbu kumbu, hata mradi wa MACEMP ambao sasa hatunao tena, ilifanya shughuli za utafiti wa viumbe wa bahari kama vile kamba, kaa, jodari, samaki wa maji ya kuelea, lakini matokeo yake hayajafikia, katika kiwango kilichotarajiwa, sasa SWIOFish ndio muarubani wa hilo.

SWIOFish, kama ulivyonisoma hapo juu, kwa hatua hii ya kwanza utatia nanga nchini Tanzania (hadi Zanzibar), Mozambique and visiwa vya Comoro, ambapo hatua nyengine itaanza baada ya miaka sita.

Pamoja na kazi hiyo, lakini pia SWIOFish unamalengo mengine ya kukuza usimamizi makini wa kuzipa vipaumbele vya shughuli za uvuvi kwa ngazi ya Kanda, Kitaifa na Kijamii 
Tunaposema kikanda kwenye mpangu huu, ni baadhi ya nchi zitajiunga na SWIO moja kwa moja, tangu unapoanza kama Tanzania ambapo nchi nyengine zitajiunga baadae kwa mujibu wa taratibu.

Kwenye ngazi ya kitaifa, mipango ya usimamizi wa shghuli za uvuvi  ambayo imepewa kipaumbele itatekelezwa, ili manufaa ya kweli na endelevu yaonekane. 

Yapo maeneo mengine kama ya kijamii, ambapo hasa lengo lake ni kuongezeka kwa Kamati za usimamizi kwa angalau asilimia mbili (2), hukunao walengwa sasa kuongezeka kwa Idadi ya watakaofaidika moja kwa moja.

Mradi huu wa usimamizi wa uvuvi kusini magharibi ya bahari ya hindi, SWIOFish, sheria ya Uvuvi no 7 ya mwaka 2010 itafanyiwa mapitio, sambamba na uanzishaji wa  na uimarisha wa mfumo wa taarifa za takwimu zitokanazo na, mbinu, leseni, usafirishaji na mapato. 

Lakini kuna maeneo teule katika  mpango huu yatasaidiwa kama vile  ujenzi wa kituo cha utafiti na ofisi  mpya ya eneo la hifadhi mbili mpya za Hifadhi ya ghuba ya Tumbatu ‘TUMCA’ na hifadhi ya Bawe ‘CHABAMCA’.

Kwa Unguja mradi huu utatekelezwa kwenye eneo la hifadhi ya Menei ‘MENAI’ na eneo la hifadhi ya Mnemba MNEMBA, ambapo kwa Tanzania (Zanzibar) wao wataendelea na mpango kwa miaka 15 utakapokamilika hatua kwa hatua.

Mwenyekiti wa wavuvi wa wilaya ya Micheweni Mkubwa Said Ali, anaona mradi huu unaweza kuzaa matunda kutokana kuwa na lengo la uhifadhi wa samaki.

“Mimi nimeshaanza sasa kuhifadhi kwenye bahari ya Makangale, sasa naamini kama mradi huu utaingia kwenye eneo langu basi uvunaji wa samaki utaongezeka’’, alisema.
Sheihan Mohamed Sheihan ambae ni Mwenyekiti wa wavuvi wilaya ya Mkoani, amewataka wavuvi kushirikiana katika hilo ili kuona lengo la mpango huo linafanikiwa.

Kombo Hamada Juma wa Chakechake ambae ni mvuvi anasema kwa hatua za maandishi mradi unaonekena kuja na jambo jipya na hasa ikiwa utatekelezwa ipasavyo.

“Mbona mradi huu wa SWIOFish, una nia nzuri kwa wavuvi na wananchi wote, maana unapogusa kuhifadhi samaki neema kwa kila mmoja’’,alifafanua.

Khamis Haji Mohamed wa Wambaa, yeye aliomba suala la elimu lipewe kipaumbele kwa walengwa, ili kuepusha majaribu ya migogor baina yao na watendaji wa PECCA.

Kila mvuvi sasa baada ya kupata taarifa hizo, yuko macho kuangalia mradi huu mkubwa ambao unatazamiwa kuwakomboa wavuvi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.