Habari za Punde

Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation Imetoa Vitabu 200,000 Vipya Vya Somo la Kiengereza Kwa Skuli za Zanzibar. > Walimu Wamehudhuria Mafunzo ya Kukuza Lugha ya Kiengereza na Kushajihisha Tabia ya Kujisomea.

Kwa siku mbili walimu kutoka sehemu mbalimbali za Zanzibar watakutanishwa na kupewa mafunzo ya kufundisha vitabu vipya vya Kiengereza kwa kutumia lugha ya kiengereza mashuleni.  Mafunzo hayo, yaliyoandaliwa na Asasi ya Milele Zanzibar Foundation, yanaendana na uchapishwaji wa vitabu 200,000 ambavyo vimefadhiliwa na Milele Zanzibar Foundation, kwa mashirikiano na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali chini ya taasisi ya Elimu Zanzibar (ZIE).  Vitabu vijulikanavyo kwa jina la “Let's Learn: English for Zanzibar Primary Schools"  kwa darasa la 1-4 vilichapishwa na Shirika la Oxford University Press na kutathminiwa na kamati maalum ilikusanya wawakilishi kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar pamoja na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar. Vitabu vilizinduliwa Januari katika Sherehe za miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati wa ufunguzi wa skuli ya Mgonjoni na Makamo wa Raisi mstaafu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr. Gharib Bilali na Waziri wa Elimu na mafunzo ya Amali Zanzibar Mheshmiwa Riziki Juma
“Uchapishwaji wa vitabu hivi ni sehemu ya matakwa na hamu kubwa ya Milele Zanzibar Foundation katika kuboresha utoaji wa elimu bora Zanzibar. Umakini na uangalifu mkubwa ulichukuliwa katika kufanikisha uchapishaji wa vitabu vyenye ubora wa juu kutokana na umuhimu mkubwa wa kuwatayarisha wanafunzi ipaswavyo kuweza kusoma, kuandika na kuzungumza kiengereza wakati watapofikia darasa la tano (5). Walimu nao wanatakiwa wawe na uelewa wa kutosha kuwa na vifaa na mbinu bora za kufundisha somo la kiengereza pamoja na kukuza uwezo wao wa kuongea lugha ya kiengereza” alieleza Khadija Shariff, Mkuu wa Miradi, Milele Zanzibar Foundation.  
Vitabu vimefuata mtaala wa elimu ya msingi ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar na kulenga watoto wa kizanzibari kwa kuzingatia mila, utamaduni, historia na mazingira katika kubuni michoro na maudhui ya vitabu vya kiada.
Mfululizo wa kitabu umefuata mtaala mpya wa somo la kiengereza wa Zanzibar ili kuhakikisha kuwa walimu wanauwezo wa kuwaandaa wanafunzi ipasavyo ili kufikia malengo ya kujifunza kama yalivyo ainishwa katika mtaala wa Taifa. Mufululizo huo umejikita katika mbinu za mawasiliano na maudhui ili kujenga uwezo na ujuzi wa kusoma, kuandika, kuongea na kusikiliza na kutumika katika mazingira ya kila siku kupitia michezo, kufanya kazi kwa vikundi na michezo mingineyo. 
Bi Fat-hiya Breik, mwalimu wa Kiengereza na English Resource Teacher wa Teacher Center ya Kiembe samaki, amesema, “Mafunzo ya vitendo yaliomo katika kitabu yanawafanya wanafunzi wawasiliane na washiriki vizuri wakati wa masomo na pia inawasaidia kuwa wajasiri na kujiamini”
Mfululizo huo pia umeambatanishwa na muongozo unaosaidia kutoa maelekezo yanayo muongezea mwalimu umahiri, ufahamu na utendaji. Muongozo umepitiwa ndani ya wiki hii ya mafunzo na kuwatayarisha walimu wa kiengereza wa Zanzibar kuwa na ujuzi unaotakiwa wa kufundisha vitabu na kuonyesha mbinu mbalimbali za kufundisha somo la kiengereza zinazowataka walimu kuwa imara katika kufundisha na kuwashirikisha wanafunzi kwa kutumia nyenzo, na kuboresha uelewa wa walimu na utumiaji wa lugha ya kiengereza.   
“Tunafuraha kubwa si ya kuchapisha vitabu vya wanafunzi tu bali pia vitabu elekezi vya walimu vinavyoonyesha  muongozo hatua kwa hatua katika utekelezaji wa kila somo kwa kutumia njia tofauti ili kufikia lengo lililokusudiwa ” alieleza Fatma Shangazi wa Oxford university Press.  
Mafunzo haya pia ni fursa ya kujadili matatizo ya kawaida na changamoto zinazowakabili walimu wa kiengereza. "Let's Learn: English for Zanzibar Primary Schools” vitaanza kutumika madarasani Febuari 2017.

Kuhusu Milele Zanzibar Foundation: Ikiwa na dira ya kujenga na kuendeleza jamii ilio mahiri na imara Zanzibar, malengo ya Milele Zanzibar Foundation ni kuengeza kasi ya maendeleo katika maeneo ya afya, elimu na fursa za uchumi jamii katika vijiji na maeneo ya mbali kupitia miradi ya maendeleo yenye ukamilifu na endelevu
 
Kuhusu Oxford University Press: Oxford University Press (OUP) ni idara ya chuo cha Oxford inayokuza na kuboresha malengo ya chuo katika utafiti, udhamini wa elimu na elimu kwa ujumla kwa kuchapisha vitabu dunia nzima. OUP ni Chuo Kikubwa duniani chenye kuchapisha na chenye wafuasi wengi kimataifa. Hivi karibuni ilichapisha maelfu ya machapisho kwa mwaka, na ofisi zao zipo takriban nchi hamsini na kuajji karibu watu 6,000 dunia nzima. Imekuwa maarufu kwa mamilioni kupitia miradi za machapisho mbalimbali ikiwemo kazi za kitaalam katika nidhamu zote za kitaaluma, bibilia, muziki, skuli na vyuo, vitabu vya watoto, vitabu kwa ajili ya kufundishia kiengereza kama ni lugha ya kigeni, vitabu vya biashara, kamusi , vitabu rejea na majarida ya kielimu.    

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.