Habari za Punde

Aina mpya ya mikoba wanayofunzwa wanawake, wapata tamaa ya soko


Wakiri TAMWA kupitia WEZA II, imewapa mwarubanini wa maisha yao
NA HAJI NASSOR, PEMBA

“Hee…kumbe hata ukili wafanywa kipochi na mkoba wa lap top, sisi kwenye ushirika wetu hili ni jambo jipya sana…..tuliozea ile mikoba ya zamani tu’’,ndio kauli ya Tamima Salum Ali wa Kengaja.

Mama huyu anatokea kwenye ushirika wa ‘Hatima njema’ unoajishughulisha na ususi wa mikoba inayotumia rasilimali ya ukindu, amewawakilisha wenzake kwenye mafunzo ya mikoba ya kisasa.

Tamina anamini sasa, kwa aina mpya na ya kisasa ya mikoba wanayofunzwa na TAMWA kupitia WEZA II, sasa mwanga wa maisha yao kupitia ushirika wao yanakaribia.

“Kwa muda mrefu sisi tuliganda kwenye kutengeza aina moja pekee, ambayo ina umbo la bao, lakini sasa jinsi ukili ulivyosarifiwa hatuna shaka maisha kupitia ushirika wetu yataimarika’’,anasema.

Akiwa kwenye mafunzo yaliofanyika Kiuyu kwa muda wa siku tatu, kwa makundi tofauti anasema kumbe, Tamima kama TAMWA kupitia WEZA II, wengepata mradi mapema na kuwapa mafunzo hayo, leo wengekuwa kwenye hadhi nyengine.

Tamima anaamini sana mafunzo ya kutengeza mikoba ya kisasa, hana wasiwasi wa soko kama ilivyokuwa kwa mikoba waliokuwa wakitengeza wao, bila ya kupata utaalamu.

Anasema wala hakuwa peke yake, maana wapo wanaushirika 50 kisiwani Pemba kutoka shehia 25 waliopewa mafunzo hayo, kwa siku tatu tatu kila wanaushirika 25.

Lengo la mfunzo hayo kwa mujibu wa Mratib wa mradi huo wa WEZA II, ni kuona wanawake wanaondokana na umaskini lakini kupitia umoja wao waliojikusanya kwenye vikundi vya ushirika.

Ndio maana kwa ari na moyo wa TAMWA kupitia WEZA II, ilikaa meza moja na wafadhili wao Milele Foundetion na kupatiwa mradi huo wa miaka mitatu.

WEZA ni mradi wa kuwawezesha wanawake kicuhumi ambao kwa mara ya kwanaza uliingia kisiwani Pemba mwaka 2008, ukiratibiwa na Chama cha Waandishi wa habarai wanawake Tanzania TAMWA ofisi ya Zanzibar.

WEZA, kwa wakati huo iliwaibua wanawake wa mkoa wa kaskazini Pemba pekee, kati ya mikoa miwili ya Pemba, ambapo ilianzisha vikundi vya ukulima wa mboga mboga, ususi wa mikoba, mikeka kisha ukamaliza muda na mwaka jana kuibuka WEZA II, pia ukiwa chini ya TAMWA.

Sio tu kutoa mafunzo pekee, bali hata baadae vipo vikundi vya ushirika ambavyo vitabahatika kununuliwa cherehani maalumu, ili kuiremba na kuipendezesha vyema mikoba hiyo ya kisasa wanayofundishwa.

“Wapo wanawake kwenye vikundi vya ususi wa mikoba, watapatiwa wameshapatiwa mafunzo, lakini hata wale wanajishughulisha na upandaji w amboga mboga, nao TAMWA imewaona’’,anasema.

Maulid Saleh Hamad, nae kupitia kikundi chao cha ushirika kinachoitwa ;Nguvu Yetu Umoja Wetu’ Kiuyu wilaya ya Wete, yeye anasema wala ndani ya ushirika wao, hawakua na habari kwamba ukili unasarifiwa.

“Sisi ilikuwa tukisuka mikoba na kisha inakaa bila ya kupata soko, maana hatukuwa na aina mpya ya kumvutia mteja, lakini sasa TAMWA imeshatuma njia ya kujikomboa’’,anasema Maulid.

Yeye kwa upande wake anasema anachongoja ni kumalizika kwa mafunzo hayo ili nae awaelekeze wenzake tisa (9) ambao hawakupata bahati ya kuhudhuria mafunzo hayo adhimu na admimu.

Hata mwanaushirika kutoka “Tupande’ kilichopo Kiungoni Kimango Mfaunda Faki Hamad anasema tangu walipoanzisha ushirika mwaka 2012, hawajahi kupata mafunzo ambayo yanatoa mwanga wa maisha kama hayo.

Anaona sasa, kupitia mafunzo hasa kwenye ushirika wao, ni kukaza kamba ili kushona mikoba ya kileo, ambayo imekuwa ikipendwa sana na watu mbali mbali wakiwemo watalii.

Yeye anasema “hana shaka juu ya soko, maana hata hiyo ya zamani walikuwa wakiitengeza kutokana na umahiri na ushupavu walionao, kuwa itanunuliwa’’,anaeleza.

Mbinu wanayoitumia ili kusaka soko, sio kubwete nyumbani bali wamekuwa wakigawanana majukumu, ili kuhakikisha mwisho wa siku wanafikia malengo yao.

Ndio maana mkufunzi na mjasiriamali wa mafunzo hayo alieaminiwa na TAMWA, Nassra Salum Mohamed wa Kiuyu, anasema suala la soko kwa wanaushirika sio kukaa nyumbani na kulilia bali inawapasa kuchakarika.

Kwa uzoefu wake, anasema lazima kwa siku za awali wanaushirika wajitutumue kutoka wanakoishi na kwenda hata maofisini au sehemu wanazofikia watalii au mkusnyiko wa watu.

Maana anasema hadi mkoba huo wa kisasa kukamilika kwa zana zake, zote wastani katia ya shilingi 15,000 hadi shilingi 17,000 hutumika, ingawa kwa bei ya kawaida mkoba huo kisha huuzwa kati ya shilingi 22,000 hadi shilingi 25,000.

Ingawa katika kuukamilisha mkoba huo wa kisasa, lazima uwe na ukindu na kisha kuupakasa, kisha kupikwa kwa rangi moja au mbili, na kuushokana kama kawaida kwa kutumia utembo au nyuzi za kipolo.

Baadae hulazimika kuwa na kipolo ambacho huunganishwa na ukili huo, ambao huzibwa kwa kitambaa, kabla ya kuweka zipu ndogo na kubwa, kutokana na aina ya mkoba unaohitajika.

Hili lilimshangaaza na kumpa matumaini makubwa, Khadija Ramadhan Ali anaetokea ushirika wa “Tupendane group’ kwamba mafunzo hayo, anaamini ni mazuri maana sasa ukili wa mikoba watauviringa wapendavyo.

“Mimi mafunzo nayona mazuri sana, na natamani yasimalize, maana sijaonapo kuwa hata kipochi na mkoba wa kumputa waweza kufanya, hapa lazima soko litapatina’’,anasilimulia.

Kwake yeye anasema ndani ya ushirika wao kama waliopoteza muda kuchelewa kupewa mafunzo hayo, ambayo anaona sasa kama mkombozi ndani ya ushirika wao.

Aliwaomba TAMWA kupitia WEZA II, kuharakisha kuwapatia mashine au sherehani za kushonea mikoba hiyo, maana kwa kutimia cherhani za kawaida kazi haiendi vyema.

Asha Makame Alawi nae alijikuta ndani ya mafunzi hayo, ya utengezaji wa mikoba, vipochi na mikoba maalum ya ofisini kwa kutumia ukindu, akiwawakilisha wenzake wa ushirika wa ‘Yarabi tupe’.

Anasema kabla ya ujio wa TAMWA kupitia WEZA II, hawa kuwa wakijua namna ya ushoni wa mikoba hiyo, ambayo anasema kumbe walichelewa sana kupata mafanikio.

“Hii mikoba ni aina mpya, maana ukiwa mbali utafikiri ni ile ya madukani inayotoka Ulaya na Arabuni, lakini kumbe ni ukindu uliosarifiwa’’,anasema.

Hakuwa tofauti na mjasriamali Salha Hilali wa Chakechake kijiji cha Mvungwa, ambae nae kabla ya mafunzo hayo, hakuwa akielewa lolote jinsi ya ususi wa mikoba hiyo.

“Mimi naishukuru sanaTAMWA na wafadhili wake Milele Foundation kwa kutuona kwenye ushirika wetu, maana ilikuwa hii mkoba twaiona kwenye tv, lakini leo nshfundishwa na najua kutengeza sasa’’,anafafanua.

Msimamizi wa Mradi huo wa kisiwani Pemba Jit-hada Abdalla Salim yeye anasema kama wanawake hao 50 watawafunza wenzao, basi elimu hiyo ya utengenezaji wa mikoba ya kisasa itaenea.

“Lengo hasa sio hawa wanawake walio kwenye vikundi vya ushirika pekee, bali kila mwanamke wa kisiwa cha Pemba, apate mafunzo haya kupitia walioshiriki’’,anafafanua.

Ndio maana amekuwa wakiwataka mara kwa mara kuhakikisha wanafuatilia kwa kina mafunzo hayo, ili wawe na uhakika wa kuwapa taaluma hiyo wenzao mbali mbali.

Lakini hata Magrate Antony nae kutoka Kikwajuni Unguja ambae alikuwa mmoja kati ya wakufunzi ndani ya mafunzo, hayo alisema kama wakielewa vyema wanawake jinsi ya ususi wa mikoba hiyo, wala hawatolalamikia soko.

“Mikoba ya kisasa ya ukindu ambayo huwa na zipu na mfunikio kama ile kutoka nje, hupendwa na wazawa na hata watalii, sasa lazima wanawake hawa wajipange ili wavune matunda’’,anafafanua.

TAMWA ilishawahi kuwapa mafunzo ya ususi wa mikoba, kilimo cha mboga mboga na jinsi ya kusaka masoko, kupitia WEZA I ingawa kwa sasa imekuja na aina mpya ya utengenezaji mikoba.

Kwa wakati huo, wanawake waliyatambua masoko ya kuuzia bidhaa za mboga mboga na mikoba, na sasa TAMWA kupitia WEZA II imetia nanga tena kisiwani Pemba ili kuendeleza pale palipoaachwa na WEZA I.

Baadhi ya wanaume waliozungumza na ukurasa huu, wanasema sasa wanawake ndio wanaojenga familia kutokana na kuingia kwenye vikundi vya ushirika na kujipatia kipato.

Ali Juma Ali ambae mke wake yumo kwenye ushirika wa ‘Umoja Wete Nguvu Yetu’ cha Kiuyu anasema yeye sasa anakula matunda yanayotokana na jitihada za mke wake kujiingiza kwenye ushirika.

“Lazima wanaume sasa tuamke, maana wanawake wamekubali kujikusanya na kuweka anasa na mambo mengine pembeni maana wameshajua umuhimu wa wao kuzisaidia familia’’,alieleza.

Kombo Hija Makame wa Mchanga mdogo anawashauri wanawake wenyewe kusimama kidete ili kuhakikisha wanawekewa banki maalum, ili wapatiwe mikopo yenye masharti nafuu.

Hassan Chumu Hassan wa Kwale yeye anasema, uhuru walionao wanawake kwa waume zao, lazima wautumie vyema ili iwe chanzo cha kufika watakako.

Wizara inayosimamia wanawake na watoto, imekuwa na mpango maalumu wa kuwawezsha wananchi kiuchumi ambapo inalenga kuinua hali za wananchi kiuchumi.

Lengo hasa ni kuwapatia wananchi hao wakiwemo wanawake, mikopo na kuwajengea uwezo wa kiujasiriamali na kuwangunanisha katika vyma vya ushirika.

Kwa 2015/2016 pekee mikopo 337 kwa Unguja na Pemba ilitolewa kupitia Mfuko wa Uwezeshaji wananchi kiuchumi, ambapo yakiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 523 iliwanufaisha wananchi 1,907 wakiwemo wanawake 1,136 ndani ya shehia 161 za Zanzibar.

Mwanaharakati wa masuala ya wanawake Pemba, Stara Khamis Salim anasema lazima taasisi zinazotoa mikopo zilegeze masharti hasa kwa wanawake, ili wakidhi vigezo na kuiomba.

Kwani anasema “wanawake wamekuwa wakipewa mafunzo mbali mbali mfano kupitia wizara husika na asasi za kiraia kama TAMWA, lakini hushindwa kuchukua mikopo”,alieleza.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mwanajuma Majid Abdalla, akizungumza na wanawake kwenye siku ya wanawake duniani ambapo kwa Pemba, ilifanyika Chakechake, alisema lazima wanawake weke chonjo siasa wafanye kazi.

“Vikundi vya ushirika endeleeni kujikusanya pamoja, ili muwe na sauti moja na hata iwe rahisi kuomba mikopo ambayo ipo na haina masharti magumu’’,anasema.

Naibu Katibu Mkuu wizara ya wanawake na watoto Zanzibar Mauwa Makame Rajaba, anawashauri wanawake kutoshindwa kutekeleza shughuli zao kwa ukosefu wa mitaji, maana sasa serikali imeshajipanga.

“Kama kuna wanawake wanahitajia mashine kwa ajili ya kuendeleza shuguli zao, waandike barua wizarani na kima cha fedha cha kununulia mashine husika, ili wapatie fedha za mkopo zenye masharti wanayoyaweza’’,anafafanua.

Akizungumza kwenye kipindi cha meza huur Evamarie Semakafu kutoka asasi ya Ulingo Tanzania bara, anasema wanawake kama hawakusimama wenyewe katika kujikomboa kiuchumi, inaweza kuwa ndoto.

Mwanaharakati wa masuala ya wanawake Pemba, Jitihada Abdalla Salum, anasema mafunzo yanayotolewa na TAMWA kupitia WEZA II, kama wanawake hao wakiyafahamu vyema, yanaweza kuwa mkombozi.

Shemsa Hakim Khamis dereva wa gari ya kuchukulia wageni (TAX) uwanja wa ndege wa Pemba, anasema huu sio wakati wa wanawake kujibakiza nyumbani wakidhani wanaweza kumalizia shida zao kila kitu.

“Wanawake hasa walioolewa, wakiwa na dhana kuwa hata mchango wa harusi umsubiri muume, ujue bado umelala usingizi mzito, hii ni karne ya mwanamke kujitegemea’’,ameshauri.


Sheikh  Massoud Hamad Ali wa Chakechake Pemba, anasema dini ya kiislamu wala haijamkataza mwanamke kufanya kazi, cha kuzingatia ni yenye heshima kama ujasiriamali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.