NA MWANDISHI
WETU, PEMBA
MAMLAKA ya
Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar ZAECA ofisi ya Pemba, inamshikilia
Mdhamini wa Idara ya usajili wa Mali na Biashara kisiwani humo Saleh Mohamed
Abdalla, akiomba rushwa ya shilingi 500,000 kwa walalamikaji wawili.
Tuhuma za kwanza zinazomkabili
Mdhamini huyo wa Idara ya Usajili ni kuomba kiasi cha shilingi 400,000 kwa
mlalamikaji kama bahashishi baada ya kumpatia waraka wa nyumba.
Taarifa za ZAECA zinaeleza kuwa,
Mdhamini huyo alishampa mtu waraka huo wa nyumba, ambapo baadae aliomba fedha
kiasi hicho na kisha kutegeshewa mtego na kunaswa na maofisi wa ZAECA, mjini
Wete.
Aidha imefahamika kuwa, shutuma za
pili zinazomkabili Mdhamini huyo ni kuomba fedha za shilingi 100,000 kwa
mlalamikaji kwa ajili ya kumpatia waraka wa nyumba, ambapo tayari alishapokea
fedha shilingi 40,000 kwa mlalamika huyo.
Akizungumza kwa njia ya simu Kaimu
Mkurugenzi wa ZAECA Suleiman Ame Juma, alisema baada ya mdhamini huyo kunaswa,
alihojiwa na wakati wowote jalada la kesi yake litafikishwa kwa DPP.
“Sisi tukishamkamta mtuhumiwa,
humuhoji na kisha jalada lake, hulipeleka kwa DPP, ili wao walipitie na kama
kuna kesi ya kujibu humpandisha mahakamani’’,alifafanua.
Akizungumza na mwandishi wa habari
hizi, mtuhumiwa huyo alisema alichokiona yeye ni kama mchezo wa kuigiza
aliofanyiwa na mtu anaemjua.
“Mimi nilishampa mtu waraka wa nyumba
tokea mwaka 2011, nimeshasahu, lakini juzi akanipigia simu na kuniletea fedha,
nataka kumuuliza za nini hizi, naona nimeshazungurukwa na watu, wakaniambia niko
chini ya ulinzi’’,alifafanua.
Aidha Mdhamini huyo wa Idara ya
Usajili, alieleza kuwa alishangaa kuona amekuja mtu na kumpa fedha ghafla kisha
kuwekwa chini ya ulinzi, jambo ambalo hadi sasa limemuweka njia panda.
ZAECA wiki mbili zilizopita, ilimshikilia
mtendaji mmoja wa Baraza la mji wa Wete, akipokea shilingi 290,000 kati ya
shilingi milioni 2.5 aliziomba kwa mtu aliedaiwa kumpatia ajira serikali.
No comments:
Post a Comment