Habari za Punde

Benki ya Kilimo Iongezewe Mtaji wa Kusaidia Wakulima Wadogo.

Na Ismail Ngayonga. Maelezo                                                                               
Sekta ya Kilimo ni muhimili wa Uchumi wa Tanzania, karibu asilimia 80 ya Watanzania wanaishi kwa kutegemea shughuli za Kilimo.

Mchango wa Sekta ya Kilimo umeendelea kuwa muhimu  katika uchumi na maendeleo ya nchi kwa kuwa inatoa ajira kwa asilimia 65.5 ya Watanzania na inachangia zaidi ya asilimia 100 ya chakula kinachopatikana nchini.
                                                  
Mara baada ya uhuru mwaka 1961, Serikali ilitoa kipaumbele cha kwanza katika kuendeleza kilimo kama uti wa mgongo wa uchumi, kutokana na ukweli kuwa sekta hiyo iliajiri zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wote.

Kati ya miaka ya 1961 na 1980, zilibuniwa  kaulimbiu na maazimio mbalimbali kama vile “Chakula ni Uhai”, “Siasa ni Kilimo”,  “Kilimo cha Kufa na Kupona”, “Mvua za Kwanza ni za Kupandia” hatua iliyolenga kuhamasisha maendeleo ya kilimo pamoja na kuhamasisha kilimo cha ujamaa.

Aidha kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya Sekta ya Kilimo mwaka hadi mwaka. Mwaka 2005/2006 bajeti ya Sekta ya Kilimo ilikuwa Shilingi Bilioni 233.3 na mwaka  2014/2015 bajeti ilifikia Shilingi Bilioni 1,084.7 ikiwa ni ongezeko la Shilingi bilioni 851.4.

Pamoja na Serikali kuanzisha mpango wa kukibadilisha kilimo kutoka kilimo cha kujikimu na kuwa cha kisasa na cha kibiashara kwa kutumia mitaji, teknolojia na ubunifu, sekta hiyo imeendelea kutawaliwa na wakulima wadogo wadogo ambao ni takribani asilimia 70 ya watanzania wote.

Upatikanaji wa mitaji yenye masharti nafuu kumetajwa kuwa ni moja ya changamoto zinazowakabili wakulima wadogo wadogo jambo linalowafanya wakione kilimo kuwa hakina tija huku wakulima wengine wakiishia kulima mazao ya chakula na si biashara.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo,  Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imekusudia kuleta Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini kwa wananchi.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Francis Assenga anasema TADB imejipanga kusaidia kutoa mikopo kwa Wakulima wadogowadogo walau laki tano (500,000) kupitia miradi ya Kilimo cha umwagiliaji hasa katika maeneo yaliyoainishwa kwenye Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Kilimo.

Kwa mujibu wa Assenga anasema Benki hiyo imeweza kuvijengea uwezo vikundi 336 vya wakulima wadogowadogo vyenye jumla wa wanachama 44,400 katika mikoa ya Iringa, Morogoro na Tanga.

Assenga anasema Benki hiyo imekuwa ikitoa mikopo ya muda mfupi; muda wa kati; na muda mrefu kwa Wakulima wadogo wadogo, wa kati na wakubwa, hususan kuziba pengo la upatikanaji wa fedha kwenye minyororo ya thamani katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na mazao ya misitu.

Kuhusu riba ya Mikopo hiyo, Assenga anasema kwa upande wa wakulima wadogo Benki hiyo imekuwa ikitoa riba ya asilimia 8-12 kwa mwaka, asilimia 12-16 kwa mashamba makubwa  na asilimia 15-18 kwa wanunuzi wa mazao ya wakulima wadogo.

Benki imepitia upya mpango mkakati wake katika kutoa mikopo ili kuweza kufikia wakopaji wengi zaidi na kuweza kufikia lengo la kuleta maendeleo katika sekta ya kilimo”  anasema Assenga.
Kwa mujibu wa Assenga Serikali ikishirikiana na TADB imefanya mazungumzo na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ambapo mkataba wa mkopo huo ulisainiwa mwaka 2016, na kiasi cha Tsh. Bilioni 200 zinatarajia kutolewa kwa ajili ya kukopesha wakulima.
Aidha Assenga alisema malengo ya Benki hiyo ni kupanua wigo wa eneo la huduma na kufika nchi nzima ambapo ofisi sita za kanda na mikoa zitafunguliwa ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wateja.
Anaongeza kuwa TADB imekusudia Kuboresha huduma kwa kuanzisha mazao maalum ya huduma za kibenki kwa wakulima wadogowadogo kulingana na mnyororo husika wa thamani na pia kuboresha huduma za kupitia taasisi za fedha zilizopo ili kufikia Wakulima wengi zaidi.
Akizungumzia kuhusu changamoto, Assenga anasema utoaji wa mikopo kwa wakulima wadogo wadogo umekuwa ukikabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya kukosekana kwa masoko ya uhakika, ambapo wanunuzi wengi wakubwa wamekuwa wakisita kusaini mikataba ya ununuzi wa mazao ili kutoa soko la uhakika.
Anaitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na kukosekana kwa uadilifu kwa baadhi ya wanufaika wa mikopo na Viongozi kutekeleza wajibu wao ikiwa ni pamoja na marejesho ya mikopo na kupeleka mazao ghalani wakati wa kuvuna.
TADB ina jukumu la kuboresha na kuinua sekta ya kilimo ili mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa uongezeke, hivyo ni wajibu wa benki hiyo kupunguza gharama za riba ili kutoa fursa kwa wakulima wote hususani wadogo kumudu mikopo hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.