Habari za Punde

Viongozi wa ZFA Wilaya ya Magharibi Watakiwa Kufanya Maamuzi ya Haraka Kwa Wadau Wao.

Na. Mwinyimvua Nzuki.

Viongozi wa chama cha soka ZFA wilaya ya Magharibi ‘A’ wametakiwa kufanya maamuzi ya haraka na kutoa taarifa kwa wadau wao ili kuepusha malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

Akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya chama hicho na ZFA taifa, mjumbe wa kamati tendaji ya ZFA taifa Abdulghani Msoma alisema kufanya hivyo pia kutaongeza uaminifu miongoni mwa wadau na klabu zilizomo wilayani humo dhidi ya viongozi.

Msoma ambae ni miongoni mwa makocha maarufu nchini alieleza hayo baada ya kamati ya ZFA taifa kusikiliza lalamiko la timu ya Bumbwisudi Stars dhidi ya ZFA wilaya ya Magharibi ‘A’ kwamba imeipokonywa nafasi ya kushiriki katika hatua ya 12 bora ya ligi daraja la pili wilayani humo isivyo halali.

“Ninashukuru mmeonesha kuwa ni watu makini katika maamuzi na utendaji wa kazi zenu, niwaombe basi mjitahidi kufanya maamuzi sahihi na ya haraka kisha mtoe taarifa kwa umma ili kuondoa manung’uniko yasiyo ya lazima”, alisema Kocha Msoma.

Mwenyekiti wa ZFA hiyo iliyoanzishwa mwishoni mwa mwaka 2015 Kheri Adam Aliy alikieleza kikao hicho kuwa chama chake kimekuwa kikifanya hivyo mara kwa mara kupitia vikao vya vilabu na wadau wengine na kwamba madai ya timu hiyo hayakuwa halali.

“Bumbwisudi wanaelewa kila kitu kuwa wameshindwa kuendelea na mashindano kutokana na kuwa na pointi chache baada ya sisi (ZFA) kuiondoa mashindanoni timu ya Makadara City kwa mujibu wa kifungu cha 22(a)iii baada ya kushindwa kutekeleza adhabu ya kulipa faini iliyotozwa  kwa mujibu wa kanuni”, alieleza Aliy.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, Bumbwisudi ilipoteza pointi 3 ilizokuwa nazo kutokana na kushinda mchezo wake na Makadara hatua ambayo iliinufaisha timu ya Kibweni Shooting Stars iliyopoteza pointi 1 baada ya kutoka sare katika mchezo wao na kufanikiwa kucheza hatua ya 12 bora inayoendelea hivi sasa.

Mbali ya kufutiwa matokeo yote, Makadara pia imeteremshwa daraja moja chini na itashiriki ligi daraja la 3 msimu ujao uamuzi ambao ulifikiwa katika kikao cha Kamati Tendaji ya ZFA wilaya ya Magharibi ‘A’ kilichoketi Februari 27, mwaka huu katika ofisi za chama hicho Mwakaje.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.