Habari za Punde

Mradi wa Ujenzi wa Kijiji cha Utalii Matemwe Pennyroyal Yapeleka E limu ya Afya Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Na Salum Vuai, MAELEZO
WANAFUNZI wa skuli za Kijini na Mbuyutende katika kijiji cha Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja, wameanza kunufaika na mradi wa kutoa elimu ya usafi unaoendeshwa na kampuni ya Pennyroyal Gibraltar kupitia tawi lake la ‘Best of Zanzibar’.
‘Best of Zanzibar’ imeanzisha masomo hayo ya usafi wa mazingira na afya kwa wanajamii wa maeneo hayo, wakianza kwa wanafunzi wa skuli hizo kufuatia utafiti uliofanywa mwezi Oktoba mwaka jana kubaini changamoto mbalimbali za kiafya kijijini hapo.

Katika muendelezo wa mpango huo juzi, taasisi hiyo ilitoa elimu kwa wanafunzi wa skuli ya Kijini juu ya njia bora za kusafisha mikono kwa maji yanayotiririka na meno, sambamba na kuwagaia misuaki, dawa zake pamoja na sabuni.

Ofisa wa kitengo cha afya na mazingira katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) aliyeongoza wakufunzi sita wa mafunzo hayo Nahya Nassor Khamis, alisema lengo la mpango huo ni kuwapa elimu wazee wa kijiji, walimu na wanafunzi ili kuwanusuru wakaazi na hatari ya maradhi ya mripuko na mengine yanayosababishwa na uchafu ikiwemo kipindupindu.

“Changamoto katika vijiji hivi vya Kijini na Mbuyutende ni ukosefu wa elimu ya afya na usafi wa mazingira ambayo huchangia sana kuibuka kwa maradhi kama kipindundindu, magonjwa ya ngozi na matumbo,” alieleza Nahya.

Alisema chini ya usimamizi wa mradi wa ‘Best of Zanzibar’ na kampuni ya Pennyroyal inayoufadhili, wanakusudia kubadilisha tabia za wananchi wa hapo na kuwaepusha na maradhi yatokanayo na ukosefu wa elimu ya afya na mazingira.

Alieleza kuwa, mradi huo unalenga kuwafikia wanakijiji 7,500 wa kijiji hicho wakiwemo wanafunzi 809 wa skuli ya Kijini, ambapo wiki iliyopita, ulifanyika skuli ya Mbuyutende na kuwanufaisha wanafunzi 512.

Mwalimu Mkuu wa skuli ya Kijini Ulimwengu Mkadam Makame pamoja na walimu wenzake, walieleza matumaini yao kwamba ujio wa mradi huo utabadilisha mienendo ya wanafunzi na wanakijiji kwa jumla.

Alisema kimsingi, hali za wananchi wa Matemwe ni ngumu mno kutokana na kukabiliwa na umasikini mkubwa, hali aliyosema inajidhihirisha wazi katika muonekano wa watoto wao ambao ni wanafunzi wa skuli hiyo na nyengine za kijijini hapo.

“Hapa Matemwe, haishangazi kuona mwanafunzi anavaa sare mpaka inamchanikia mwilini kwani wananchi hawana kipato cha kumudu kuwanunulia sare kila baada ya muda mfupi,” alieleza.

Aliishukuru Pennyroyal kwa kubuni mradi huo, akiomba uwe endelevu na kuzifikia changamoto nyengine zinazokikabili kijiji hicho ikiwemo uhaba wa madarasa katika skuli hiyo.

Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi waliozungumza na gazeti hili, walieleza furaha yao kutokana na elimu waliyopewa, wakisema kuwa itawasaidia kuwajenga kiakili na kuwaongezea ufahamu katika masomo yao.

Amina Omar Mtwana na Mcha Hambal Makame wanaosoma kidato cha tatu, walisema usafi ni jambo la msingi hata katika kuchangamsha akili, hivyo wanaamini mradi huo utakuwa chachu ya kuwatuliza na kusoma kwa bidii.

Naye Mohammed Issa Khatib ambaye ni msimamizi wa mradi huo kutoka ‘Best of Zanzibar’, alisema kampuni ya Pennyroyal inakusudia kuzipatia ufumbuzi changamoto nyengine mbalimbali zilizomo kijijini humo ili kuwainua kimaisha wananchi wake pamoja na kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji.

Aliitaja mipango ya baadae kuwa ni pamoja na kuwaandalia masomo ya biashara wanawake na vijana wa Matemwe ili waweze kujiendeleza pamoja na kuongeza ujuzi wa ujasiriamali.

“Tunaamini kwamba kupitia elimu hii ya biashara na ujuzi wa kutengeneza bidhaa kama vile sabuni, vikapu na mafunzo ya kilimo, tutaweza kuwakomboa wananchi hawa na kuwastawisha kimaisha,” alifafanua Khatib.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.