Habari za Punde

Rais wa Zanzibar Dk Shein Azungumza na Mkuu wa Majeshi Ikulu Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na  Mkuu mpya wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania Jenerali Venance S. Mabeyo alipofika Ikulu Mjini Zanzibar kujitambulisha kwa Rais leo, 15/03/2017.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na  Mkuu mpya wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania Jenerali Venance S. Mabeyo alipofika Ikulu Mjini Zanzibar kujitambulisha kwa Rais leo,[Picha na Ikulu,]

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                                                  15.03.2017
---
RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kwa kuendelea na kazi kubwa ya kuilinda Tanzania pamoja na mipaka yake yote.

Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania Jenerali Venance Salvatory Mabeyo, aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha rasmi kwa Rais.

Dk. Shein katika maelezo yake alimueleza Jenerali Mabeyo kuwa Jeshi la Ulinzi la Wananachi Tanzania (JWTZ), limeweza kujijengea sifa kubwa ndani na nje ya Tanzania kutokana na uwezo wake mkubwa unaoenda sambamba na nidhamu na heshima iliyojengeka ndani ya Jeshi hilo.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa ana imani na matumaini makubwa na uongozi wa Jenerali Mabeyo kuwa Jeshi hilo litaendelea kuimarika na litafanya mambo makubwa na kumuahidi kua ataendelea kutoa ushirikiano wake pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili Jeshi hilo lizidi kupata maendeleo.

“Nakuthibitishia kuwa tokea siku ulioapishwa nimepata matumaini makubwa kutokana na uongozi wako, kwani katika uongozi wangu tokea nikiwa Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nimefanya kazi na Wakuu wa Majeshi watatu na wewe utakuwa wanne na nimefanya kazi nao vizuri hivyo na wewe nakuahidi kuwa nitaendelea kufanya kazi vizuri na kukupa mashirikiano yote”,alisema Dk. Shein.

Sambamba na hayo, Dk. Shein aliendelea kutoa pongezi kwa Jeshi hilo kwa kuendelea kulinda amani na usalama huku akiahidi  kuendelea kutoa ushirikiano wake na Jeshi hilo ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano wake kwa Brigedi ya Zanzibar.

Nae Mkuu wa Jeshi la Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo alitoa shukurani kwa Dk. Shein na kumueleza kuwa Jeshi hilo limekuwa likipata mashirikiano makubwa kutoka kwake pamoja na kutoka kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Aidha, Jenerali Mabeyo alimpongeza Dk. Shein na kueleza kuwa ni kiongozi mwenye hekima na busara kubwa hali ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa katika kuiongoza Zanzibar.

Pia, Mkuu huyo wa Majeshi aliendelea kumueleza Dk. Shein kuwa Jeshi la Ulinzi la Wananachi Tanzania linathamini sana ushirikiano anaoutoa  Dk. Shein ikiwa ni pamoja na ushiriki wake kwa Chuo cha Taifa cha Taifa.

Pamoja na hayo, Jenerali Mabeyo alimueleza Dk. Shein kuwa Zanzibar imeendelea kutumika kwa vikao mbali mbali vya viongozi wa Majeshi ya Afrika ukiwemo Mkutano wa viongozi hao kutoka nchi za SADC kutokana na kuwepo kwa amani na utulivu pamoja na kuwa na vivutio mbali mbali kwa wageni.

Jenerali Mabeyo aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia, ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli tarehe 2 Februari na kuapishwa Februari 6 mwaka huu baada ya aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Davis Mwamunyange kustaafu.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.