Habari za Punde

Serikali Yawahakikishia Usalama Wawekezaji Katika Tasnia ya Habari.

Na Daudi Manongi-MAELEZO
SERIKALI itaendelea kuvilinda Vyombo vya Habari vilivyowekeza nchini zikiwemo Radio na Televisheni kwa kuwa mchango wao katika jamii ni mkubwa. 

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye katika ziara yake kwa Vyombo vya Habari vya E-fm, TV1 na Times Fm, leo Jijini Dar es Salaam.

 “Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati mikubwa ya kuwa karibu na Vyombo vya Habari nchini, kupitia Wizara yangu tunautambua uwekezaji huu mkubwa mlioweka katika Teknolojia na tunatambua gharama kubwa iliyotumika, hivyo Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano ili uwekezaji huu usonge mbele,”aliongeza Waziri Nape.

Aidha Waziri Nape alisisitiza kuwa uwekezaji uliofanyika kupitia vituo hivi vya Mawasiliano sio wa rahisi na ni vyema kuheshimu uwekezaji huu kwa kila namna kwani umeonyesha njia na ana imani kuwa wengi wataiga mfano huu wa uwekezaji.

Waziri nape alitumia fursa hiyo pia kuvishukuru Vyombo vya Habari nchini kwa kuanzisha vipindi ambavyo vinabeba ajenda ya viwanda na kutoa wito kwa vyombo vingi zaidi kubuni vipindi kama hivyo ili watanzania wengi wapate fursa zaidi ya kuelewa dhana nzima ya Serikali ya Awamu ya Tano.

“Serikali itaendelea kuwa karibu na nyie ili kutengeneza mazingira mazuri kati yetu na hii itasaidia hata ajenda mbalimbali za Serikali kuzifanya pamoja kwa kushirkiana na nyinyi kwa karibu na hivyo kuwafikia wananchi kwa urahisi.”Alisisitiza Waziri Nape.

Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kupitia Sheria na Kanuni zilizopo na kuzifanya marekebisho ili kutengeneza daraja zuri kati ya Serikali na wadau wa Habari ikiwa ni pamoja na kuboresha mahusiano katika kazi kwani Serikali inatambua kazi nzuri inayofanywa na vyombo hivyo.

Ziara hiyo ni muendelezo wa ziara za kikazi za Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye katika Vyombo vya Habari nchini kwa lengo la kujifunza na kuimarisha yaliyopo baina ya Serikali na Vyombo vya Habari nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.