Habari za Punde

Wadau wa Elimu Waiunga Mkono Programu ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Kwa Vijana na Wazee.

Na Ismail Ngayonga. Maelezo Dar es Salaam
RIPOTI ya shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ya mwaka 2015 inaonyesha kuwa takribani watoto Milioni 58 wameshindwa kujiunga na shule na milioni 100  kati yao wameshindwa kuhitimu anagalau elimu ya msingi.

Taarifa hiyo inaongeza kuwa ukosefu wa usawa katika elimu umeongezeka, huku watoto maskini na wale walioko kwenye mazingira magumu ndio wanaobeba mzigo mzito zaidi wa uwezekano wa kutokwenda shule, mara nne zaidi ya watoto matajiri zaidi duniani.

Aidha ripoti hiyo ya dunia ya ufuatiliaji wa Elimu kwa wote inaendelea kueleza kuwa ubora mdogo wa elimu ya msingi kuwa ni miongoni mwa ni changamoto zinazosababisha mamilioni ya watoto kuhitimu shule bila ujuzi wa msingi. 

Hadi kufikia mwaka 2015 Jumuiya ya Kimataifa na Serikali mbalimbali duniani zimekuwa mstari wa mbele zimekuwa mstari wa mbele katika kuyafikia makundi ya walio pembezoni na walio kwenye mazingira magumu, yasiyo­kika kirahisi na ambayo bado hayajanufaika na haki.

Ili kukabiliana na changamoto hiyo, mwaka 1992 Taasisi ya Elimu ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) ilianzisha programu ya Elimu ya Sekondari kwa vijana na watu wazima waliokosa nafasi ya kuendelea na elimu ya Sekondari kwa sababu mbalimbali.

Kwa mujibu wa takwimu za TEWW za mwaka 2012 zinaonyesha kuwa Tanzania ina jumla ya vijana wa umri wa miaka 7-17 Milioni 3.5 waliopo nje ya shule, ambapo kati yao Milioni 2.5 wanahitaji elimu ya Sekondari na Milioni 1 wanahitaji Elimu ya msingi.

Naibu Mkurugenzi wa TEWW, Dkt. Kassimu Nihuka anasema tatizo la vijana na watu wazima waliokosa elimu ya sekondari ni kubwa sio kwa Tanzania pkee bali kwa nchi zote zilizopo katika ukanda wa kusini mwa jangwa la sahara.

“Vijana wanaomaliza elimu ya msingi na kupata alama ufaulu chini ya 100 (kati ya 250) wamekuwa wakiachwa kwenda sekondari katika mikoa mbalimbali isipokuwa wale ambao wazazi wao wana uwezo wa kuwapeleka shule za sekondari za binafsi ambazo gharama zake ni za juu” anasema Dkt. Nihuka.

Anaongeza kuwa programu iliyoanzishwa na TEWW imekusudia kuwawezesha wanafunzi waliomaliza darasa la saba ambao hawakupata nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari na wanahitaji kumaliza elimu hiyo.

Akifafanua zaidi Dkt. Nihuka anasema programu hiyo inaendeshwa katika majengo ya shule za msingi na sekondari za Serikali 83 na wadau 337 nchini, ambapo hadi kufikia sasa jumla ya vijana na watu wazima 95,140 wameweza kunufaika na masomo hayo kuanzia mwaka 2010 hadi 2016.

Aidha Dkt. Nihuka anaongeza kuwa programu hiyo pia imewalenga wanafunzi ambao wamemaliza masomo ya MEMKWA (Mpango wa Elimu ya Msingi kwa walioikosa) na wale waliomaliza masomo ya sekondari lakini hawakufanya vizuri na wangependa kurudia mtihani wa taifa wa kidato cha nne.

Kwa mujibu wa Dkt. Nihuka anasema kupitia programu hiyo, masomo hutolewa katika hatua kuu tatu ambazo ni pamoja na masomo ya kidato cha I na II, masomo ya kidato cha III na IV na hatua ya mwisho inabeba masomo ya kidato cha V na VI.

“Katika hatua ya kwanza, mlengwa anasoma kwa kipindi cha mwaka mmoja na hivyo kuwa na sifa ya kufanya mtihani wa maarifa, yapo masomo yanayotolewa katika hatua hii ni Historia, Jiografia, Kiingereza, Kiswahili, Hisabati, Biolojia na Uraia” anasema Dkt. Nihuka.

Dkt. Nihuka anasema mlengwa wa hatua ya pili anatakiwa kusoma kwa kipindi cha mwaka mmoja ambapo ataweza kuwa na sifa ya kufanya mtihani wa kidato cha nne uliondaliwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA).

Kuhusu hatua ya mwisho ya programu hiyo, Dkt. Nihuka anasema masomo mahsusi yanayotolewa katika tahasusi za HGL (Historia, Jiografia na Lugha), HKL (Historia, Kiswahili na Lugha), HGK (Historia, Jiografia na Kiswahili) pamoja na HE (Historia, Jiografia na Uchumi), na mlengwa katika hatua hiyo anaweza kusoma kwa zaidi ya mwaka mmoja hadi pale atakapokuwa amejindaa vya kutosha kufanya mtihani wa maarifa au ule wa NECTA.

Anaongeza kuwa masomo hayo yanatolewa kupitia mafunzo ya ana kwa wakati wa jioni kuanzia saa 9 alasiri hadi saa 12 jioni, ambapo mlengwa ataweza kujisomea moduli na vitabu na matumizi ya teknolojia za kujifunzia kama vile elimu mtandao kupitia machapisho huria ya kielimu.

Kuhusu gharama za masomo hayo, Dkt. Nihuka anasema viwango vya ada vinavyotozwa na TEWW katika elimu ya sekondari hutofautiana na vituo vinavyoendeshwa na wadau, ambapo kwa upande wa TEWW gharama za ada ni kati ya Tsh 150,000/- hadi 300,000 kutegemeana na mkoa husika na gharama zilizowekwa kwa mwaka.

Elimu na mafunzo bora ni mkakati wa kipaumbele kufikia malengo ya mipango ya maendeleo yaliyowekwa, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Mkakati wa Taifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA) pamoja na malengo ya Milenia vinaweka wazi umuhimu wa elimu  na mafunzo katika kufikia malengo ya mipango hiyo. 

Ni wito kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwahimiza wazazi na walezi kuwapeleka vijana wao waliokosa alama za ufaulu katika mitihani wa darasa la saba kutumia fursa ya TEWW ili kuwawezesha kupata elimu ya Sekondari.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.