Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Tanzania inauhitaji mkubwa wa nyumba kutokana na kasi ya ukuaji wa miji nchini ambapo inakadiriwa kuwa na mahitaji ya nyumba 26,840,909 ifikapo 2050 ili kukidhi mahitaji wa watu milioni 118.1.
Akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kufungua semina kuhusu makazi, ujenzi na maendeleo ya miji kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wawekezaji wa sekta ya Milki kutoka Japan Julai 28, jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi amesema kuna uhitaji mkubwa wa nyumba nchini ili kukidhi mahitaji watu katika maeneo mbalimbali nchini.
“Tanzania tuna uhitaji mkubwa wa nyumba kwa sababu ukiangalia miaka ya 1967, ukuaji wetu katika miji ulikuwa asilimia 6.2 tu, lakini katika sensa ya mwaka 2022 ukuaji katika miji yetu umekwenda asilimia 34.9 ambao ni ukuaji wa kasi kubwa sana na inatarajiwa kufikia asilimia 59 ifikapo mwaka 2050, hatua inayofanya nchi yetu kuwa moja ya nchi zenye miji inayokuwa kwa kasi katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara” amesema Waziri Ndejembi.
Akitolea mfano wa miji inayokuwa kwa kasi, Waziri Ndejembi amesema awali hali ya ukuaji wa miji nchini ilikuwa kwenye majiji ya Dar es salaam na Mbeya, kwa sasa hali ni tofauti ambapo miji Geita, Katavi na Mpanda inakua kwa kasi.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, mahitaji ya nyumba nchini yalikuwa 14,724,164 ambayo ni idadi ya nyumba zilizokuwepo na ambao zinahudumia wakazi 61.7 million kwa mwaka 2022, mwaka 2025 mahitaji ya nyumba ni 15,500,000 huku idadi ya watu ikiwa ni milioni 68.2 na mahitaji ya nyumba ifikapo 2030 yanatarajiwa kuwa 17,659,090 na idadi ya watu inatarajiwa kuwa milioni 77.7 huku mahitaji ya nyumba yanatarajiwa kuwa 26,840,909 ili kukidhi mahitaji ya nyumba kwa watu wanatarajiwa kufikia milioni 118.1 ifikapo mwaka 2050.
Ili kufikia mahitaji hayo, Serikali imeweka mazingira rafiki ya uwekezaji kwa kuwakaribisha wawekezaji mbalimbali katika sekta ya Milki nchini kurahisisha upatikanaji wa makazi ili Watanzania wapate nyumba za bei nafuu.
Hatua ambazo Tanzania imechukua ni pamoja na kuondoa kodi kwenye ujenzi wa nyumba za thamani ya chini ya Shilingi milioni 50 na kuzindua Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 Toleo la mwaka 2023 ambayo iliyozinduliwa Machi 17, 2025 na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatoa fursa kwa wawekezaji katika sekta ya Milki ili Watanzania wapate nyumba za bei nafuu.
Kwa upande wake Balozi wa Japan nchini, Mhe. Yoichi Mikami amesema semina hiyo ni muhimu itasidia kuboresha mahusiano baina ya Tanzania na Japan ambapo makampuni na wataalam baina mataifa hayo watashirikiana kuhakikisha kunakuwa na makazi nchini kulingana na mahitaji.
No comments:
Post a Comment