Na Hanifa Salim, Pemba
BARAZA la Mji Chake chake Pemba, limewataka wamiliki wa
magari kuyatumia maeneo yalioandaliwa kwa ajili ya maegesho ya magari kwa
kufuata utaratibu unaotakiwa ili kupunguza msongamano wa magari katika mji wa
Chake chake.
Hayo
yalielezwa na Mkurugenzi wa Baraza la Mji huo, Nassor
Suleiman Zaharani, wakati alipokua katika ziara ya siku moja na Mkuu wa Mkoa wa
Kusini Pemba, ambapo akikagua maeneo ya maegesho ya magari katika mji wa
chake chake.
Alisema lengo la kuanzisha maeneo hayo ni kuondosha
msongomano wa magari uliopo katika mji wa chake chake kama alivyoagiza Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt, Ali Mohamed Shein.
“Tumeandaa
eneo la kupaki gari za Teksi, karibu eneo la Soko la Qatar ambapo litachukua gari 40 hadi 50 kwa wakati
mmoja, tumeandaa maegesho ya gari za Wesha na Ndagoni ambalo limegharimu milioni
6,400,000/= pamoja na eneo la maegesho
ya gari za keri lililopo katika mji wa Chake chake”, alisema.
Sambamba
na hayo, alisema Baraza la mji Chake chake limeandaa maegesho ya magari katika
eneo la nyumba za fleti Madungu ambapo litakua ni egesho la gari za Mkoani
ambapo litachukua gari 20 kwa wakati mmoja.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mwanajuma Majid Abdalla, alilipongeza
baraza la mji Chake chake kwa kufanya juhudi hiyo ili kuitekeleza kauli ya Rais
wa Zanzibar.
“ Mujue
wajibu wa kazi zenu na kuweza kusimamia tusiwe na muhali tutakapokua na muhali
hatutoweza kujenga nchi lengo letu ni kujenga nchi na kubadilisha mji wetu wa
Chake chake” alisema Mkuu huyo.
Hata
hivyo alilitaka Jeshi la Polisi kubadilika kwa kusimamia gari ambazo hupakiwa
pembeni mwa Mji wa Chake chake ili kuwadhibiti wanaoegesha magari katika mji huo
kwa kuweza kueka mji katika mandhari nzuri.
Nae,
Mkuu wa Wilaya ya Chake chake, Salama Mbarouk Khatib, aliahidi kusimamia na
kudhibiti watakao haribu mji wa chake chake kwa kuwachukulia hatua za kisheria
ili kuondoa malalamiko na kuleta mafanikio yaliokusudiwa.
Katika
ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa na Wilaya na watendaji wa baraza la mji walitembelea
egesho ya magari katika Mji wa Chake chake , maegesho ya gari ta TAX karibu na
Soko la Qatar, egesho la gari za Wesha na Ndagoni, Madungu katika egesho la
gari za Mkoani na kukagua Soko la Quweit lililopo Michakaini ambalo linaendelea
na ujenzi wake.
No comments:
Post a Comment