Habari za Punde

Uamuzi Kesi ya Shkuba, Wenzake Kutolewa Kesho

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imeshindwa kutoa maamuzi kuhusu maombi ya Serikali ya Marekani ya kuwataka raia watatu wa Tanzania akiwemo mfanyabiashara bilionea, Ally Khatib Hajj ‘Shkuba’ kama waende nchini humo kusikiliza kesi za dawa za kulevya zinazowakabili, na kuahirisha zoezi hilo hadi kesho.
Katika usikilizwaji huo ambao wajibu maombi wanatetewa na jopo la mawakili watatu akiwemo Majura Magafu, wakili Kakolaki alieleza kuwa waziri mwenye dhamana alipelekewa maombi ya kutakiwa kwa Shkuba na wenzake Aprili 4, mwaka huu.
Maombi ya Marekani kuwahitaji Shkuba na wenzake, yaliwasilishwa na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Harryson Mwakyembe kupitia, Wakili wa Serikali Mkuu, Edwin Kakolaki yalianza kusikilizwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Cyprian Mkeha.
Baada ya kuwepo kwa mvutano huo wa hoja mahakamani hapo, Hakimu Mkeha kwa mara nyingine aliahirisha kesi hiyo hadi kesho kwa ajili ya kutoa uamuzi kama wajibu maombi wasafirishwe kwenda nchini Marekani kusikiliza kesi za dawa za kulevya zinazowakabili ama lah.
Shkuba alikamatwa na Serikali ya Tanzania mwaka 2014 kwa kusafirisha kiasi cha kilo 210 za Heroin, ambazo zilikamatwa Januari, 2012 huko mkoani Lindi na baadaye Serikali ya Marekani ilishikilia mali zake, kwa madai kwamba alikuwa na kesi ya kujibu nchini humo pia.
Mbali ya Shkuba, watuhumiwa wengine wanaotakiwa na Serikali hiyo ya Marekani ni mfanyabiashara Idd Mafuru na Lwitiko Adam.
Kabla ya kuwasilishwa kwa maombi hayo, Machi 9 mwaka jana, serikali ya Marekani kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Wizara ya Fedha inayoshughulikia udhibiti wa mali za nje (Foreign Assets Control-OFAC), ilimtaja Shkuba kuwa ni kinara mkuu wa Kimataifa wa usafirishaji wa tani za dawa za kulevya ikiwemo Heroin na Cocain kwenda Afrika, Ulaya, Asia na Marekani ya Kaskazini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.