Habari za Punde

Elimu Kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi Iwafikie Wananchi Kwa Wakati.

Na Ismail Ngayonga. Maelezo Dar es Salaam.                                                                
RIPOTI iliyotolewa na Idara ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa inasema maeneo mengi ya bara la Afrika kwa mwaka wa 2017 yataendelea kusumbuliwa na uhaba wa chakula na hatari ya baa la njaa na ukame.

Aidha taarifa hiyo inaongeza kuwa ifikapo mwaka 2050 katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, wastani wa mavuno ya mpunga, ngano na mahindi utashuka kwa asilimia 14, asilimia 22 na asilimia tano, kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Katika kipindi kichopungua miongo mitatu, dunia imekuwa ikikabiliwa na majanga mbalimbali ambayo yamesababisha hasara kubwa ya upotevu wa mali na maisha ya watu.

Kila mwaka mwaka takribani watu Milioni 200 duniani wanaathirika na ukame, mafuriko, vimbunga, matetemo, moto, na majanga mengine, na hivyo kuongeza kasi ya watu kuathirika kiuchumi na kuongeza idadi ya watu masikini duniani.

Kuwepo kwa majanga haya kunatokana na sababu mbalimbali zitokanazo na kuongezeka kwa shughuli za binadamu zinazoathiri mfumo mzima wa hali ya hewa ikiwemo ukataji wa miti, uvuvi usiozingatia utaalamu pamoja na matumizi mabaya ya ardhi.

Tanzania pia imekuwa ikikumbwa na majanga mbalimbali kama ukame, mafuriko, moto, vita vya wakulima na wafugaji, na milipuko ya mabomu ambapo majanga yote haya yalileta athari  kwa wananchi na mali zao.

Katika mwaka 2013/14 ukame ulisababisha upungufu wa chakula kwa watu828,063 katika Wilaya 54 za mikoa 14 nchini na Serikali ilitoa tani 26,663 za chakula cha msaada chenye thamani ya Tsh. Bilioni 2.2 kwa ajili ya kusafirisha chakula hicho kwa walengwa.

Sekta ya Kilimo ni uti wa mgongo kwa wananchi na uchumi wa Tanzania, na kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kumechangia kwa kiasi kushuka kwa uzalishaji wa kilimo na kutotabirika kwa mvua kumeathri wakulima.

Taarifa ya hali ya chakula ya mwaka 2016/17 iliyotolewa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inaonyesha kuwa kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara mikoa 15 na Halmashauri 43 zilibainika kuwa na maeneo yenye uhaba wa chakula kutokana na ukame uliothiri mazao.

Aidha taarifa hiyo inaongeza kuwa mvua za vuli zinazochangia asilimia 17 hadi 20 ya uzalishaji wa chakula, zilichelewa kuanza na kunyesha chini ya kiwango na kwa mtawanyiko usioridhisha katika maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka.

Hali hiyo inaelezwa kuathiri uingizaji wa mazao ya chakula kwa wingi sokoni hususani mahindi kutokana na wafanyabiashara kukodhi mazao hayo wakiwa na matarajio ya kupanda kwa bei.

Kwa kuzingatia hali ya mabadiliko ya tabia nchi na athari zake nchini, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inatekeleza Mpango wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabia Nchi Katika Kilimo (2014-2019) ili kukabiliana na viashiria vya janga la mabadiliko ya Tabianchi.

Viashiria hivyo ni pamoja na kuongezeka kwa joto, ukame unaokithiri, mvua zisizotabirika na za muda mfupi, mafuriko, wadudu na magonjwa pamoja vifo vya mifugo.

Mtaalamu wa mazingira katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Theresia Massoy anasema Mpango huo umekusudia kutoa kipaumbele katika  Kuboresha Matumizi Bora ya Ardhi na Maji katika Kilimo ikiwa ni pamoja na Kuwa mbinu mbalimbali za uvunaji na uhifadhi wa maji ya mvua.

Aidha anaongeza kuwa kupitia mpango huo, Serikali pia imekusudia Kuongeza Matumizi ya Kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi na kuboresha  mifumo ya kupambana na athari ikiwemo Kupanda mazao yanayohimili hali ya mabadilko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa Massoy anasema Wizara imepanga kushirikiana na Wataalamu wa kilimo katika Halmashauri nchini kwa kutilia mkazo na kuzijengea uwezo mbinu za kienyeji za uvunaji maji ya mvua kwa kuzingatia utafiti, sera ya umwagiliaji na ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi.

Massoy anasema kupitia mpango huo, Serikali imeendelea kuweka mkazo kwa wataalamu wa kilimo kuimarisha mfumo wa matumizi ya hifadhi ya maji yaliyovunwa wakati wa mvua katika shamba ili yaweze kutumika kipindi cha upungufu wa maji kwa kutumia matanki, malambo mabwawa na hata visima.

Kwa mujibu wa Massoy anasema katika kuongeza kasi ya matumizi ya mbinu za Kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, Serikali imeendelea kuzijengea uwezo halmashauri ili ziweze kuhuisha masuala ya kilimo kinachohimili mabadiliko tabianchi katika mipango, mafunzo na uhamasishaji.

“Katika kusisitiza na kutilia mkazo uwepo wa kuhuisha masuala ya kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi katika mipango ya Maendeleo ya Halmashauri (DADPs), tumeandaa mifumo ya uhamasishaji na motisha kwa wakulima ili kuzingatia faida,  mbinu na teknolojia za kisasa” anasema Massoy.

Massoy anasema malengo ya Serikali kupitia Mpango huo ni kuboresha ufahamu na mifumo inayolenga mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kuongeza utolewaji wa taarifa, mawasiliano na kujenga ufahamu wa jamii.

Hali ya hewa duniani inabadilika, hivyo uzalishaji wa chakula na kilimo ni lazima vibadilike ili kwenda sanjari na mabadiliko hayo.

Kuwekeza kwa wakulima wadogo kutasaidia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kutokana na umuhimu wa kundi hilo katika kilimo, ndio maana ajenda ya mwaka 2030 inatoa wito wa kutokomeza njaa pamoja na kuchangia kilimo endelevu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.